In Summary

Mijadala, misukosuko imeibuka kwa baadhi ya wabunge wa nchi hizo wakati wa vikao vya bajeti

EAC. Jana macho na masikio ya wananchi yalikuwa kwa mawaziri wa fedha wa nchi za Afrika Mashariki ambao walikuwa gumzo kila kona ya nchi zao wakisubiriwa kwa hamu kusoma bajeti kuu ya mwaka 2018/2019.

Nchi hizo ambazo zimeweza kusoma bajeti hiyo ni pamoja na Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda.

Kwa nchi zote hizo sekta ya kilimo imepewa kipaumbele katika bajeti hiyo.

Mbali ya sekta hiyo, pia sekta zingine ambazo zilipewa kipaumbele ni pamoja na afya na elimu.

Hatua hiyo ni baada ya kila wizara kuwakilisha makadirio ya matumizi na mapato huku ikiibuka mijadala mizito ambayo wakati fulani ilisababisha mvutano kwa wabunge wa nchi hizo.

Nchini Kenya bajeti hiyo ilisomwa saa tisa alasiri na Waziri wa Fedha, Henry Rotich ambayo kwa jumla ilikuwa ni ya Sh66 trilioni (Ksh3 trilioni).

Bajeti ya Kenya ilijikita zaidi kwenye ajira na kilimo.

Mwaka jana, Waziri Rotich aliondoa kodi ya mahindi yanayoagizwa kutoka nje ili kurahisisha uagiza wa bidhaa hiyo. Pia aliondoa kodi ya utengezaji wa dawa za kuua wadudu na magari ya utalii yanayotengenezwa nchini Kenya.

Kama moja ya njia ya kuzuia uchezaji kamari, Serikali iliongezea kodi ya sekta hiyo hadi asilimia 50 kutoka asilimia 7.5.

Kadhalika, Uganda nako Waziri wa Fedha, Matia Kasaija alitangaza bajeti akitenga Sh16 trilioni (Ush32.7 trilioni), huku vipaumbele vikielekezekwa kwenye sekta za utalii, miundombinu, elimu, michezo, afya, ulinzi na kilimo.

Waziri wa Fedha wa Rwanda, Dk Uzziel Ndagijiman alitaja vipaumbele vya bajeti ya nchi hiyo akidai itajikita kwenye kilimo na viwanda.

Alisema bajeti imeongezeka kwa asilimia 16 ikilinganishwa na iliyopita ya mwaka 2017/2018.

Waziri huyo alisema bajeti kuu ya mwaka huu wa fedha itakuwa Sh6 trilioni (Rwf2.4 trilioni).

Alisema bajeti hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Julai Mosi imelenga kuinua uchumi.

Dk Ndagijiman alisema uchumi wa Rwanda unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.2.