In Summary
  • Taarifa za hesabu za fedha ambazo zimetolewa leo Julai 30, 2018 na benki nyingi zinaonyesha kuongezeka kwa mali na amana za wateja licha ya baadhi kutofanya vizuri.

Dar es Salaam. Robo ya pili ya mwaka huu (kati ya Aprili -Juni) imekuwa ya neema kwa sekta ya benki nchini kutokana na kuongezeka kwa amana na mali za benki, taarifa ya fedha zimeonyesha.

Taarifa za hesabu za fedha ambazo zimetolewa leo Julai 30, 2018 na benki nyingi zinaonyesha kuongezeka kwa mali na amana za wateja licha ya baadhi kutofanya vizuri.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ziliongezeka kwa asilimia 6.6 kufikia Sh1.93 trilioni kwenye robo ya pili ya mwaka unaoishia Juni 30, 2018 kutoka Sh1.81 trilioni katika robo ya kwanza inayoishia Machi 31.

Wakati ongezeko hilo likiwa hivyo, amana za wateja zikiongezeka kwa asilimia 9.7 kufikia Sh1.37 trilioni kutoka Sh1.25 trilioni kwa kipindi hicho.

Mali za Benki ya CRDB ziliongezeka hadi kufikia Sh5.92 trilioni kwenye robo ya pili ya mwaka kutoka Sh5.89 trilioni kwenye robo ya kwanza. Amana za wateja ziliongezeka kufikia Sh4.33 trilioni kutoka Sh4.28 trilioni katika muda huo.

Benki nyingine zilizoonyesha ongezeko la mali pamoja na amana za wateja zilikuwa Benki ya Posta (TPB), Azania; Barclays, Yetu Microfinance, Mkombozi, NIC, Benki ya Biashara ya Afrika, Standard Chartered, Amana, Equity na I&M.

Licha ya benki nyingi kuonyesha ufanisi mzuri kwa kipindi hicho, kuna baadhi zilizoonyesha upungufu wa mali pamoja na amana za wateja.

Miongoni mwa hizo ni mali za First National Bank (FNB) ambazo zilipungua kwa asilimia 6.3 kufikia Sh259.5 milioni kutoka Sh276.9 milioni katika robo ya kwanza, wakati amana za wateja zikipungua mpaka kufikia Sh124.9 milioni kutoka Sh276.9 milioni kwa kipindi hicho.

Benki nyingine ni Benki ya Maendeleo pamoja na Ecobank.