In Summary

Shindano hilo lililoanza Aprili 1, 2018  na kuhitimishwa Juni 30, 2018  lililenga kuwafundisha wanafunzi utamaduni wa kuweka akiba na namna ya kuwekeza kwenye soko la hisa.

Dar es Salaam. Mwanafunzi wa chuo cha Mipango Dodoma,  Milembe Mataluma ameibuka mshindi wa shidano la uwekezaji kwa wanafunzi wa vyuo na sekondari lilikokuwa likiendeshwa na Soko la hisa Dar es Salaam (DSE).

 

Shindano hilo lililoanza Aprili 1, 2018  na kuhitimishwa Juni 30, 2018  lililenga kuwafundisha wanafunzi utamaduni wa kuweka akiba na namna ya kuwekeza kwenye soko la hisa.

 

Mataluma ameshinda baada ya kuwabwaga wenzake tisa walioingia fainali na kufanikiwa kupata zawadi ya Sh 2 milioni ambayo nusu ya fedha hizo zitatumika kununua hisa katika kampuni zilizoorodheshwa DSE.

 

Mshindi wa pili,  Wilson Mjarifu alipata Sh1.5 milioni huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Fredrick Jacob kutoka Mzumbe ambaye alinyakua Sh1 milioni.

 

Akikabidhi zawadi kwa washindi ofisa mtendaji mkuu  wa DSE, Moremi Marwa amesema bado kuna uelewa mdogo wa jamii kuhusu hisa na soko la mitaji.

 

Amesema ni sababu hiyo ndio imeisukuma DSE kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ikiwemo kupeleka mafunzo hayo vyuoni na katika shule za sekondari ili kuanza kuwajengea uelewa vijana tangu wakiwa chini kujua umuhimu wa soko hilo.

 

"Tumegundua wengi hawafahamu kuhusu soko la hisa hata wanafunzi wengi wanajifunza nadharia na wanaamini soko la hisa haliwahusu kabisa lakini ukweli ni kwamba kila mtu ana nafasi DSE,"

 

Amesema shindano hilo linalenga kuwafundisha wanafunzi utamaduni wa kuweka akiba na kujifunza namna ya kuwekeza kwenye soko la hisa.

 

Kuhusu shindano hilo Marwa amesema hii ni mara ya tano na mwaka huu zaidi ya wanafunzi 20,000 wa vyuo na 270 wa sekondari walishiriki.

 

Jumla ya wanafunzi 10 wa vyuo na 6 wa sekondari waliingia fainali ambapo kila kundi lilitoa washindi watatu waliokabidhiwa zawadi ya fedha taslimu.

 

Kwa upande wa sekondari, David Mugishagwe wa shule ya Sekondari Shaban Robert ndiye ameibuka mshindi wa kwanza na kujikanyukulia Sh1 milioni.

 

Nafasi ya pili imechukuliwa na Christopher Ngonyani wa Kibaha sekondari (Sh 600,000) wa tatu ni Price Abubakar Mushi kutoka Loyola sekondari aliyepata Sh400,000.

Tuzo ya Heshima imeenda kwa Laurent  Laurian aliyekua balozi wa soko la hisa mwaka 2017.

 

Laurent amepewa tuzo hiyo kwa kufanya kazi kubwa ya kuwaongoza washiriki zaidi ya 20,000 kwa kuwapa  elimu,kuhamasisha na kubuni mifumo ya ushiriki ya kiteknohama iliyowasaidia washiriki katika kufanya mijadala mbalimbali inayohusiana na shindano pamoja na soko la hisa.