In Summary
  • Ili kupata kazi unayoipenda, ni lazima kuweka jitihada kubwa kwenye mahojiano, hasa kama yanafanyika kwa simu au Skype. Tumia dondoo hizi ili uweze kumvutia mwajiri wako mtarajiwa.

Mahojiano ya ajira kwa njia za mtandaoni yanazidi kuwa kitu cha kawaida. Hii ni kwa sababu njia hizi zinamuwezesha mwajiri kuchuja maombi ya kazi kwa urahisi na kwa gharama nafuu zaidi. Kama njia nyingine za mahojiano, njia ya simu au Skype ni namna moja ambayo mwajiri anajaribu kujibu swali la, “Je, Huyu ni mtu sahihi kwa kampuni yangu?”. Afisa uajiri wa BrighterMonday, Gizzel Mbaga anaelezea dondoo za muhimu za kufuata wakati wa mahojiano kupitia simu au Skype ili uweze kumvutia mwajiri wako mtarajiwa kwa kumuonyesha kuwa wewe ni mtu sahihi kwa kazi iliyotangazwa.

 

Ushupavu na Ujasiri

Kujielezea vizuri kwenye mahojiano ni jambo la muhimu. Utulivu na ubora wa sauti ni muhimu zaidi katika mahojiano ya simu au Skype. Mambo utakayo sema na jinsi utakavyo yasema yatapimwa kwa umakini na anayekuhoji. Kumbuka kuongea kwa sauti inayosikika na kueleweka kwa urahisi. Jielezee kikamilifu na kwa ufupi, hasa kama ni Skype amabapo spidi ya intaneti inaweza kubadilika ghafla. Hakikisha umekaa mkao mzuri wakati wa mahojiano, na mtiririko wa maongezi uwe wenye kueleweka.

 

Mahojiano Yabaki Kuwa ya Kitaalamu

Ni makosa kufikiri kuwa mahojiano kwa njia ya simu au Skype sio mahojiano rasmi. Epuka kutumia majina ya mtaani au majina yasiyofaa kama jina lako la Skype. Hapa ndio unakutana na mwajiri wako kwa mara ya kwanza, hivyo ni vyema kutumia jina lako halisi. Pia tumia picha rasmi kwa ajili ya wasifu wako wa Skype ili kumpa taswira nzuri mwajiri wako. Kwa simu za Skype ambazo zinahusisha video, vaa vazi la kikazi kama ambavyo ungevaa kwenye mahojiano ya ana kwa ana.


Tumia Mtandao Imara

Mtandao imara ni muhimu ili mahojiano yako yaende vizuri. Pitia na fanya majaribio ya vifaa vyako. Hii ni kuhakiki ubora wa sauti na video kwenye Skype. Hakuna kitu kinachokera kwenye mahojiano ya Skype kama mtandao unao kata kata. Fanyia majaribio kompyuta yako na kipaza sauti ili kuhakiki kuwa sauti yako itasikika vizuri. Kama utaunganisha kipaza sauti au kamera ya nje, basi iunganishe na uipangilie mapema kabla ya mahojiano.

 

Angalia Mazingira Yako

Afisa uajiri atakapo wasiliana na wewe ili kupanga muda wa mahojiano, mpe muda ambao utakuwa huru ili uweze kufanya mahojiano kwa umakini. Tafuta sehemu iliyo kimya ili uelekeze umakini wako wote kwenye mahojiano. Ukikaa sehemu yenye kelele, basi afisa uajiri anaweza kufikiri kuwa hauhitaji kazi iliyotangazwa. Hakikisha sehemu utakayokaa ina mwanga wa kutosha. Hakikisha mwanga unatokea mbele yako, ili sura yako ionekane vizuri. Na mwisho safisha na pangilia vizuri mazingira yatakayo onekana wakati wa simu ya Skype.

Shiriki Kikamilifu Katika Mahojiano

Usiogope kuendeleza maongezi kwa maswali au majibu yanayohusiana na ajira iliyotangazwa. Epuka miingiliano, hakikisha umefunga programu nyingine zote kwenye kompyuta yako. Hii itasaidia mtandao wako uwe imara wakati wa mahojiano kupitia Skype. Onyesha ari na shauku yako kwa kupata nafasi hiyo ya mahojiano. Usiogope kuonyesha ujuzi ulionao unao husiana na kazi. Epuka kuuliza maswali kuhusu mshahara au mafao mengine utakayopata kwenye kazi hiyo. Mahojiano ya simu/Skype ni kwa ajili ya kutathmini kama unafaa kwa ajili ya nafasi iliyotangazwa. Mchukulie afisa uajiri unayefanya nae mahojiano kama hadhira, hakikisha unamvutia ipasavyo.

Ijue Kampuni

Jifunze tamaduni, maadili na bidhaa au huduma za kampuni unayoomba kazi. Ni muhimu sana kufanya utafiti kuhusu kampuni unayotaka kuomba kazi ili wakati wa mahojiano uweze kuwashawishi kwamba unafaa kujaza nafasi iliyotangazwa. Waombaji ambao hawajafanya utafiti wao, wanaweza kuonekana kuwa hawafai kujaza nafasi iliyotangazwa. Ni rahisi kunadi ujuzi wako kama umefanya utafiti wako na unaijua kampuni vizuri.

Fanya Ufuatiliaji

Baada ya mahojiano kuisha, wasiliana na afisa uajiri. Lakini hakikisha ufuatiliaji wako sio wenye kukera, mfano kutumia mitandao ya kijamii kama LinkedIn. Barua pepe tu inatosha. Epuka kufuatilia kwa kutumia Skype, isipokuwa pale tu ambapo afisa uajiri amekuelekeza ufanye hivyo!

Katika soko la ajira lenye ushindani, ambapo kila mtu ana sifa zinazo hitajika, onyesha ubunifu wako kwa kufuata dondoo hizi, omba kazi unayotaka kupitia BrighterMonday