In Summary
  • Kila mkataba unaoufanya duniani, zipo sheria zinaousimamia. Hata kwenye ajira, kuna sheria zinazosimamia suala hilo ili kulinda haki zako. Mkataba ni muhimu sana kabla hujaanza kazi.

Kazi ni mbaya ukiwa nayo, usipokuwa nayo ni nzuri sana. Mara nyingi kauli hii inapaswa kuzingatiwa na watu wote wanaoingia kwenye mkataba wa ajira.

Aina ya mkataba wa ajira humpa mfanyakazi na mwajiri fursa ya kufahamu haki na wajibu wake hivyo kujenga mazingira mazuri ya utekelezaji kwa kulinda maslahi ya kila upande.

Mkataba wowote ni lazima uwe ni makubaliano ya pande mbili, wenye malipo na lengo halali unaowahusisha watu wenye uwezo na sifa kwa hiari yao. Kama kimojawapo kati vigezo hivyo kitakosekana kinaweza kuifanya ajira kuwa kuwa batili.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004, kuna aina tatu za mikataba ya ajira ambayo ni usiokuwa na muda maalum, wa muda maalum kwa wataalam na kada ya uongozi pamoja, na wa kazi maalum.

Mkataba usiokuwa na muda maalum huonyesha tarehe uliyosainiwa lakini hauelezi utaisha lini. Mkataba wa muda maalum kwa kada ya uongozi huwahusisha zaidi waajiriwa wanaoshika wadhifa wa juu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mkataba wa kazi maalum hukamilika pindi shughuli husika inapofika tamati. Hii, kwa mfano, yaweza kuhusu utekelezaji wa mradi.

Bila kujali aina ya mkataba, jambo muhimu kuzingatia ni kuhakikisha kabla ya kuanza kazi, kuna mkataba wa maandishi uliosainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa.

Mkataba ndio unaoeleza aina ya shunguli utakazofanya, mipaka yako, mkuu wako wa kazi, malipo na haki zako za msingi pamoja na namna ya kuvunja mkataba bila kusahau masuala mengine muhimu ambayo hamuwezi kukubaliana kwa maneno.

Tatizo kubwa la mkataba wa maneno ni ugumu wa kuuthibitisha. Kukosekana kwa maandishi kunahatarisha ulinzi na usalama wa haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa. Usikubali kuanza kazi bila mkataba.

Usikubali kusaini mkataba bila kuusoma na kuuelewa na ni muhimu kujua umeingia mkataba wa aina gani kati ya aina hizo tatu ili ujue haki na wajibu wako kisheria na namna masilahi yako yatakavyolindwa.