In Summary

Profesa Ole Gabriel alisema hayo alipotembelea shirika hilo na kuongeza kuwa ili wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta ya viwanda waweze kupata huduma muda wowote, ni lazima Tirdo wafanye kazi usiku na mchana.

Mapinduzi ya viwanda hayajaanzia katika mitambo, bali yanaanzia katika fikra za watu

Dar es Salam. Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Elisante Ole Gabriel, amelitaka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda nchini (Tirdo), kufanya kazi usiku na mchana ili wadau wa biashara na viwanda wapate huduma wakati wote.

Profesa Ole Gabriel alisema hayo alipotembelea shirika hilo na kuongeza kuwa ili wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta ya viwanda waweze kupata huduma muda wowote, ni lazima Tirdo wafanye kazi usiku na mchana.

“Tunahitaji sana utafiti wenu. Kutokana na umuhimu huo, nawaomba mfanye kazi saa 24 kwa siku saba za wiki, ikiwezekana Profesa Mtambo (Mkumbukwa) muweke zamu kwa wafanyakazi ili wadau wetu wa viwanda na biashara waweze kupata huduma wanapohitaji.

“Mapinduzi ya viwanda hayajaanzia katika mitambo, bali yanaanzia katika fikra za watu, kwa kubuni shughuli zitakazowaingizia kipato, lakini tumeona Tirdo inaisaidia sana Serikali kujua ni eneo gani tunatakiwa kuanzisha kiwanda kulingana na eneo husika,” alisema Profesa Ole Gabriel.

Alibainisha kuwa mikakati ya wizara kwa sasa ni kuhakikisha inaunganisha mnyororo wa thamani wa kilimo na viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo alisema silaha kubwa ya ushindani katika uchumi wa viwanda na biashara ni kutumia taasisi zinazofanya utafiti kuhusu maendeleo ya viwanda.

Profesa Mtambo pia alisema kwamba kupitia fedha za maendeleo walizopewa, Sh100 milioni zimetumika kununua mashine ya kisasa ya kupima sumu kuvu na kuangalia usalama wa chakula.

Awali, Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Tirdo, Dk Anselm Mosha alisema kwamba mashine hiyo itakuwa na uwezo wa kupima sumu kuvu kwenye vyakula vya nafaka kama, mahindi, karanga, ufuta, makopa ya mihogo na matunda.

“Pia, mashine hii inapima masalia ya viuatilifu katika mazao mbalimbali, hasa ya mbogamboga na matunda, lakini pia masalia ya sumu za dawa zinazotoka kwenye nyama na maziwa,” alisema Dk Moshi.