In Summary
  • Programu hiyo ijulikanayo kama ‘Nitume’ inampa mteja fursa ya kuagiza bidhaa aitakayo kutoka popote nchini kisha kuletewa alipo na wahudumu.

Dar es Salaam. Kampuni ya Sihebs Technologies imezindua programu inayofikisha bidhaa mbalimbali mahali alipo mteja.

Programu hiyo ijulikanayo kama ‘Nitume’ inampa mteja fursa ya kuagiza bidhaa aitakayo kutoka popote nchini kisha kuletewa alipo na wahudumu.

Mwenyekiti mtendaji wa kampuni hiyo, Siwangu Mgata alisema programu hiyo inalenga kurahisisha biashara hasa kwa wateja wenye mambo mengi ambao wanakosa muda wa kufanya kila kitu kwa wakati.

“Kwa kutumia Google Maps, Nitume inatoa fursa kwa wateja kuagiza chakula kiwe cha mchana au jioni, matunda au dawa kutoka popote kisha kuletewa walipo,” alisema Mgata.

Google Maps itamuwezesha mteja kufuatilia ulipo mzigo wake kwani atakuwa na nafasi ya kujua ulipo mzigo wake kuanzia unapotoka dukani mpaka utakapomfikia.

Mgeta alisema programu hiyo imeanza kufanya kazi tangu Mei mwaka huu na tayari zaidi ya wafanyabiashara 50 wamejisajili ili kufanikisha mauzo ya bidhaa zao wakiwamo kutoka mikoa ya Mwanza, Dodoma, Morogoro na Arusha.

“Tunawalenga wajasiriamali wa kati wenye bidhaa za aina tofauti. Tunafikiria kupanua biashara nje ya Tanzania pia,” alisema.