In Summary
  • Meneja wa huduma za utalii mamlaka ya hifadhi Ngorongoro, Paul Fisso alisema tayari mikakati ya kuanzisha aina hiyo mpya ya utalii imeanza na maeneo ambayo utafanyika yatatangazwa.

Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), inakusudia kuanzisha utalii wa mpya wa kutumia baiskeli na kupanda farasi ndani ya hifadhi hiyo, ili kuwavutia watalii zaidi katika hifadhi hiyo.

Meneja wa huduma za utalii mamlaka ya hifadhi Ngorongoro, Paul Fisso alisema tayari mikakati ya kuanzisha aina hiyo mpya ya utalii imeanza na maeneo ambayo utafanyika yatatangazwa.

“Tutakuwa na maeneo maalumu ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, ambako watalii wataweza kuingia na kutembelea kwa baiskeli na kujionea vivutio na wengine wataweza kutumia farasi,” alisema Fisso.

Alisema sambamba na aina hiyo, utalii wa kutumia puto (baloon) unatarajiwa pia kuanzishwa katika mamlaka hiyo ambayo ni moja ya maajabu ya asili barani Afrika na eneo la urithi wa dunia.

“Lengo la kuanzisha utalii huu ni kuvutia watalii zaidi lakini kutasadia kuongeza siku za watalii kukaa Ngorongoro, hivyo wataongeza mapato ya Serikali,” alisema Fisso.

Meneja wa bodi ya utalii Mkoa Arusha, Willy Lyimo alisema ili kuongeza siku za watalii kukaa nchini na kujionea vivutio vingi ni muhimu wahifadhi kuendelea kuwa wabunifu kwa kuanzisha aina mbalimbali za utalii, kwa kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi lakini havitumiki.

“Bodi ya utalii tutaendelea kutangaza vivutio hivyo tuna imani watalii wengi zaidi watakuja Tanzania, kwa kuwa hakuna eneo jingine barani Afrika ambalo lina vivutio vingi vya asili kama Tanzania,” alisema.

Pia, Lyimo alisema TTB baada ya kufanikiwa kuongeza watalii kutoka mataifa ya Marekani, Uingereza, Ujerumani na Italia, sasa imepanua wigo wa kujitangaza katika mabara ya asia, Ulaya Mashariki na maeneo mengine muhimu.

Naye meneja wa kampuni ya Winglink Travel, Anwer Dhalla ambao ni mawakala wa utalii hivi karibuni walifanikiwa kuwaleta mawakala kutoka nchi za Ulaya Mashariki, alisema baada ya kurejea katika nchi zao mawakala hao wameahidi watakuwa mabalozi wazuri wa utalii.

Kampuni hiyo iliwaleta mawakala hao kwa kushirikiana na TTB, NCAA na shirika la hifadhi za Taifa (Tanapa).

Dhalla alisema mawakala hao walitembezwa hifadhi za Serengeti, Tarangire na Zanzibar ili kujionea vuvutio vilivyopo na kwenda kuvitangaza.