In Summary
  • Utafiti mdogo uliofanywa na gazeti hili kwenye masoko ya Kariakoo, Buguruni na Temeke umeshuhudia kushuka kwa bei ya zao hilo kwa mauzo ya jumla hata rejareja kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu.

Dar es Salaam. Kuanza kwa msimu wa mavuno ya karanga, kumeshuhudia bei ya zao hilo ikishuka jijini Dar es Salaam.

Utafiti mdogo uliofanywa na gazeti hili kwenye masoko ya Kariakoo, Buguruni na Temeke umeshuhudia kushuka kwa bei ya zao hilo kwa mauzo ya jumla hata rejareja kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu.

Hadi mwishoni mwa mwaka jana, gunia moja lenye ujazo wa kilo 100 lilikuwa linauzwa Sh300,000 bei iliyoshuka mpaka kati ya Sh190,000 na Sh200,000, wakati rejareja imeshuka kutoka Sh2,800 mpaka Sh2,000 kwa kila kilo moja.

Wakala wa muuzaji wa nafaka tofauti katika Soko la Temeke, Peter Kato alisema kushuka kwa bei ya karanga maeneo mengi nchini kunatokana na kuongezeka kwake baada ya kuanza kwa mavuno.

“Ni kawaida. Huu ni mssimu wa mavuno mzigo ni mwingi sokoni, bei itashuka zaidi kwa kuwa kuanzia mwezi ujao mpaka Agosti ni msimu mwingine wa mavuno,” alisema Kato.

Karanga hulimwa zaidi mikoa ya kanda ya kati; mikoa ya Dodoma na Singida na Kanda ya Ziwa inayojumuisha Mwanza, Kagera na Shinyanga. Hata Kilimanjaro, Mtwara, Tabora, Kigoma na nayo inafanya vyema kwenye kilimo cha zao hilo.

Licha ya mwenendo wa bei ulioshuhudiwa, hakukuwa na mabadiliko yoyote kwenye mahitaji ya karanga.