In Summary

Uber ni kampuni ya kimataifa inayowaunganisha abiria na teksi zilizopo karibu kwa kutumia mtandao, huku ikitoa gharama za safari husika hivyo kuondoa haja ya kufanya makubaliano kati ya wahusika.

Dar es Salaam. Kutokana na kusuasua kwa usafirishaji baharini, kampuni ya Allcargo Logistics ya nchini India inapanga kutumia teknolojia kama ya Uber kusafirisha makontena kwenye meli za mizigo.

Uber ni kampuni ya kimataifa inayowaunganisha abiria na teksi zilizopo karibu kwa kutumia mtandao, huku ikitoa gharama za safari husika hivyo kuondoa haja ya kufanya makubaliano kati ya wahusika.

Mfumo unaotumiwa na kampuni hiyo umeondoa ulazima wa madereva teksi kusubiri wateja vituoni, huku ukiimarisha usalama wa mteja na dereva kwa kuwa kila mmoja anapaswa kujisajili kwenye App yake.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Shashi Kiran Shetty alisema teknolojia ndiyo suluhisho pekee ya kukabiliana na kushuka kwa biashara.

“Mpango wetu ni kuwasaidia wateja wetu kusafirisha mizigo yao kutoka popote walipo duniani kwenda watakako. Kampuni zinazotumia teknolojia kama Uber zimefanikiwa,” alisema Shetty. Taarifa zilizoripotiwa na mtandao wa bloombergquint.com, zinasema faida ya Allcargo ambayo ni kampuni tanzu ya ECU Worldwide imepungua kwa robo nne kati ya tano zilizopita hivyo kuhitaji mikakati mipya.

ECU Worldwide ni kampuni kubwa ya usafirishaji makontena ambayo haina meli, lakini inawaunganisha wasafirishaji na meli zilizopo kama Uber inavyowaunganisha madereva na abiria.

Teknolojia hiyo itakuwa na manufaa si India pekee hata nchini, ambako wakati fulani meli huwa chache kuliko mizigo iliyopo.

Msimu wa mauzo ya korosho mwaka jana, kampuni za Vietnam zilishindwa kusafirisha mzigo walioununua kutoka mkoani Mtwara kutokana na meli kujaa.