In Summary

Uchangiaji huo ulifanyika jana katika viwanja vya Msimbazi Centre kwa kushirikiana na Hospitali ya Mloganzila.

Dar es Salaam. Wafanyakazi wa Benki ya Biashara ya Mkombozi wameungana na Watanzania wengine kuchangia damu ikiwa ni sehemu ya Siku ya Wachangia Damu Duniani inayoadhimishwa leo.

Uchangiaji huo ulifanyika jana katika viwanja vya Msimbazi Centre kwa kushirikiana na Hospitali ya Mloganzila.

Akizungumza wakati wa uchangiaji huo, mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, George Shumbusho alisema upungufu wa damu ni tatizo kubwa Tanzania na duniani kote.

Alisema jitihada zinazofanywa na kitengo cha damu salama zimewasaidia watu wengi wenye uhitaji wa damu hasa wakati wa ajali, uzazi na upasuaji.

“Tuna kila sababu ya kusimama kwa umoja kuhakikisha kitengo cha damu salama kinafikia malengo yake ya kuhakikisha kuna damu ya kutosha nchi nzima. Njia bora ya kufanya hivyo ni kwa kujiunga na familia ya wachangia damu kwa kupitia makundi ya kijamii na taasisi mbalimbali. Hii itahakikisha kitengo hiki kina damu ya kutosha ili kuokoa maisha ya wengi zaidi,” alisema.

Aliwapongeza Watanzania wengine waliojitokeza katika uchangiaji huo wa damu huku akiwataka wasaidie katika kueneza ujumbe huo ili watu wengi zaidi wajitokeze kuchangia damu.

Mkazi wa Kinondoni, Abdallah Mwakipeo alisema mwamko wa uchangiaji damu bado uko chini nchini na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kila mara kuchangia damu kwenye hospitali na vituo vya afya.