In Summary
  • Kampuni hiyo yenye hoteli na kambi za kitalii 15 nchini na tano Kenya, imetambuliwa kwa kutimiza vigezo vya uwajibikaji na Shirika la Kimataifa la Fair Trade Tourism (FTT).

Arusha. Kampuni ya Asilia inayotoa huduma za ukarimu kwa watalii, imeshinda tuzo ya uwajibikaji katika uhifadhi wa mazingira, utamaduni na jamii inayoizunguka Afrika.

Kampuni hiyo yenye hoteli na kambi za kitalii 15 nchini na tano Kenya, imetambuliwa kwa kutimiza vigezo vya uwajibikaji na Shirika la Kimataifa la Fair Trade Tourism (FTT).

Mkurugenzi mkuu wa Asilia, Jeroen Harderwijk alisema: “Tunajivunia kutajwa na Fair Trade Tourism kama kampuni namba moja kwa uwajibikaji barani Afrika. Matokeo chanya kama haya ni mambo ambayo uongozi wa kampuni yetu unayakazia.”

Licha ya tuzo hiyo, Asilia ni kampuni pekee Afrika iliyothibitishwa na shirika la Global Impact Investment Rating System (GIIRS), lililoiweka miongoni mwa kampuni 10 bora matokeo chanya duniani.

Harderwijk alisema manufaa makubwa ya kuthibitishwa FTT ni kusaidia kuweka kiwango cha uwajibikaji, hivyo kwa pamoja wataendelea kujituma ili kuongeza kiwango cha kipimo hicho.

Asilia ni kampuni ya kwanza ya utalii barani Afrika kwa kupewa kiwango cha nyota tano, ambayo ilitangazwa kuwa moja ya kampuni bora duniani mwaka 2013.

Mwaka 2014, Asilia ilitambuliwa kama kampuni ya utalii kwa ajili ya biashara ya kesho (Tourism for Tomorrow Business Award.)

“Tunafanya kazi kwa karibu na jamii, Serikali, vyama vya kiraia na wenzetu katika sekta ya ukarimu kwa nia ya kufanikisha kila linalowezekana kwa watu wote kwa muda mrefu ujao,” alisema.