In Summary
  • Hatujapata taarifa kutoka kata nyingine zinazofanya chaguzi lakini habari zilizothibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambaye ni msimamizi wa uchaguzi, Elias Ntiruhungwa ni kwamba mawakala 16 wa mgombea wa Chadema, Charles Mnanka walijikuta hawana mtu wa kuwaapisha.

Mwishoni mwa wiki iliyopita zilisambaa habari kuhusu danadana zilizoanza kupigwa katika mchakato wa kuwaapisha mawakala watakaoshiriki kusimamia uchaguzi mdogo kata ya Turwa wilayani Tarime, Mara.

Hatujapata taarifa kutoka kata nyingine zinazofanya chaguzi lakini habari zilizothibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambaye ni msimamizi wa uchaguzi, Elias Ntiruhungwa ni kwamba mawakala 16 wa mgombea wa Chadema, Charles Mnanka walijikuta hawana mtu wa kuwaapisha.

Mawakala hao walifika ofisi ya msimamizi wakiwa na barua za utambulisho na picha kama sheria na kanuni zinavyoelekeza, lakini hawakumkuta ofisa yeyote wa uchaguzi wala hakimu wa kuwaapisha.

Ntiruhungwa anasema mawakala hao wasingeapishwa mwishoni mwa wiki kwa sababu ilikuwa mapumziko na hakukuwa na hakimu na kwamba aliwaelekeza kuwasilisha fomu zao za utambulisho na picha mbili za pasipoti ofisini ili wapangiwe siku ya kuapishwa.

Pia, Ntiruhungwa alisema hadi mwishoni mwa wiki ofisi yake ilikuwa haijapokea barua za utambuisho na orodha ya mawakala kutoka Chadema wakati maofisa wa chama hicho kikuu cha upinzani wakidai kwamba barua na orodha ya mawakala 13 na wengine watatu wa akiba ipo ofisini kwa msimamizi huyo. Majibizano haya yanatupa shaka na yanakumbusha yaliyotokea katika uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni Februari mwaka huu.

Katika uchaguzi ule uliofanyika kujaza nafasi ya mbunge wa CUF aliyejiuzulu na kujiunga na CCM, mawakala wa Chadema walililalamikia kitendo cha kuapishwa bila ya kupewa hati zao za viapo.

Katika kushinikiza kupewa viapo hivyo, Chadema waliandamana wakitaka kwenda ofisi ya msimamizi wa uchaguzi ambako walitawanywa katika tukio ambalo mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini alipigwa risasi wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya waandamanaji.

Imani yetu ni kwamba tatizo la Turwa litatatuliwa mapema ili kuhakikisha kwamba haki inatamalaki katika uchaguzi huo.

Aidha, tunawasihi wasimamizi wote uhakikisha wanatenda haki. Tunawakumbusha wasimamizi wote zinakofanyika chaguzi ndogo, ziwe za madiwani au ubunge kuzingatia haki.

Wagombea nafasi za udiwani wamependekezwa na kupitishwa na vyama kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi na wakishinda wanapaswa kuwatumia wananchi wote bila upendeleo na kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi ya juu.

Tunajua hakuna uchaguzi unaomalizika bila lawama, lakini ni vyema wakurugenzi wakatimiza wajibu wao kwa haki - katika hili wawaapishe mawakala kwa haki - ili wasilaumiwe. Tunajua kwamba wakurugenzi wanapigiwa kelele na vyama vyote lakini ni jukumu lao kuhakikisha siyo tu wanatenda haki, bali haki ionekane kuwa imetendeka.

Tunawaomba wakurugenzi waonyeshe weledi wao katika kusimamia ukweli ili anayeibuka mshindi, ashinde kwa haki na anayeshindwa akubali matokeo.

Tunamalizia kwa kuwapa wakurugenzi ambao ni wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ushauri unaotokana na vitabu vya dini usemao “Haki huinua Taifa; bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.”

Kwa msingi huo, tunawasihi wasiruhusu vitendo vinavyokiuka haki ili kuwafurahisha watu kwani yanaweza kuzua balaa na sote tukabaki tunalia.

Kwa msingi huo tunaamini kwamba watafanya kazi kwa kuzingatia uzalendo wao kwa taifa hili na kwa mujibu wa Katiba na sheria tulizojiwekea.

Wahenga walisema kutenda kosa si kosa, bali kurudia kosa, tuikatae ile kadhia iliyotokea Kinondoni kujirudia katika chaguzi hizi.