In Summary
  • Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto duniani kote ikiwamo katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, Asia na hata nchini Marekani, wameathirika na tatizo hilo.

Unaweza kudhani ni afya bora kwa mtoto, lakini kumbe ni janga la siku za usoni. Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imeeleza kuwa unene kupita kiasi kwa watoto umeongezeka mara 10 zaidi katika kipindi cha miongo minne.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto duniani kote ikiwamo katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika, Asia na hata nchini Marekani, wameathirika na tatizo hilo.

Unene kupita kiasi kwa watoto ndicho chanzo cha maradhi ya moyo, kisukari na hata saratani. Wakati ripoti hii ikitolewa ni wakati sahihi sasa kwa wazazi na Taifa kujitathmini na kuangalia ukubwa wa tatizo hili hapa nchini.

Lakini kabla ya Serikali kuchukua hatua yoyote, wajibu mkubwa anao mzazi au mlezi. Walezi na wazazi wengi wanadhani mtoto akiwa mnene kupita kiasi ni dalili ya afya njema na hufanya juhudi kubwa kumlisha vyakula, lakini kiafya si sahihi.

Kuna uzito unaofaa kwa mtoto, lakini unapozidi basi maradhi kama saratani, kisukari na ya moyo humnyemelea. WHO inaeleza kuwa unene kupita kiasi husababisha vifo milioni 1.5 kila mwaka.

Huenda ni wazazi wenyewe wanawanunulia watoto wao vyakula hivyo au mazingira ya shule yanayomchochea mtoto kupenda vyakula vya aina hiyo, lakini kimsingi mzazi ana nafasi kubwa ya kubadilisha hili.

Pamoja na nafasi ya mzazi lakini mtindo wa maisha umesababisha watoto wengi kula vyakula kama baga, soda zenye sukari nyingi na pizza vinavyouzwa kila mahali na kwa bei nafuu siku hizi, na ambavyo vipo katika makundi ya vyakula visivyo na afya au junk food.

Lakini kama WHO wasemavyo, unene huo ni janga kubwa kwa kizazi kijacho kinachotegemewa kuongoza, kusimamia uchumi na kutoa huduma. WHO imesema watoto milioni 192 wana unene kupita kiasi duniani. Hii ina maana kuwa baada ya miaka mitano au kumi watoto hawa watakuwa wanaugua magonjwa ya moyo, saratani au kisukari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtindo wa maisha unachangia janga hilo kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, siku hizi wanafunzi wengi hawatembei kwa miguu kwenda shule, bali wanapanda magari ya shule.

Katika shule hasa za binafsi ni aghalabu watoto hawapati mazoezi mepesi.Kwa mfano hawafanyi usafi kama kufagia, kudeki au kufyeka kama ilivyokuwa enzi zetu. Haya yote yanatajwa kusababisha mtoto awe mzembe na kunenepa kupita kiasi.

Kibaya zaidi, watoto hao wakirudi kutoka shule, wazazi hawawapi mazoezi au kuwatengenezea mazingira ya kuwajibika. Wakirudi shule wanaketi mbele ya luninga kuangalia katuni. Wataalamu wanasema kuwa sababu mojawapo ya watoto na hata watu wazima kuongezeka uzito ni kutumia muda mwingi katika luninga.

Hebu angalia mazingira haya; asubuhi mtoto anaamka anakunywa juisi badala ya chai, anakula corn flakes (mahindi ya kukaushwa) na maziwa. Mchana mtoto huyo anakunywa soda, anakula chipsi kuku. Akipata nafasi ya mapumziko atakula ice cream au pipi ama keki kwa wingi au pengine biskuti. Usiku ukifika atakula wali na nyama au chipsi tena.

Kwa mazingira haya, bila shaka tunazalisha watoto ambao ni wagonjwa watarajiwa. Si suala la udhanifu, bali ukweli ni kuwa takwimu za watoto wenye kisukari zinaongezeka katika hospitali nyingi hapa nchini. WHO inasema magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kisukari, saratani, moyo na figo na mishipa ya damu yanasababisha vifo kwa asilimia 63.

Kwa tathmini ya haraka, tatizo la unene kupita kiasi linawaathiri zaidi watoto walio mijini ukilinganisha na wale wa vijijni na ndipo tunaporudi palepale kwenye mada ya mtindo wa maisha.

Kwa mfano, asubuhi mtoto wa kijijini atakunywa chai na mihogo au na maandazi, lakini mchana atakula ugali wa dona na mchicha au kisamvu huku usiku pengine wali na maharage au ugali na sukuma wiki. Kwa mazingira ya kijijini, vyakula vya karibu anavyokutana navyo ni embe, chungwa, mihogo mibichi, maboga au viazi vitamu. Kama ni nyama basi ni ya kuku wa kienyeji.

Mtoto wa kijijini atakwenda shule kwa baiskeli au atatembea kwa miguu, atarudi nyumbani saa sita kula na jioni atatembea tena kurudi nyumbani. Haya ni mazoezi tosha kwake na wala si adhabu, bali ni afya. Atakwenda kukata kuni au nyasi na siku za Jumamosi ataambatana na wazazi shambani. Kimsingi mtoto huyu atakuwa imara kimwili.

Ni wakati sahihi sasa kwa wazazi, kuangalia namna bora ya kuwalisha watoto ili tuepuke maradhi. Tuwaandalie mazingira mazuri kiafya ili wawe wakakamavu kimwili. Inasikitisha iwapo tunaandaa Taifa la kesho ambalo tayari limeathiriwa na maradhi chekwa. Wazazi wawape watoto mazoezi ya viungo na wapunguze kuweka vinywaji vya sukari kwa wingi katika majokofu. Pia wawasimamie watoto katika mlo sahihi ikiwamo matunda na mboga za majani.

0713-235309