In Summary
  • Ujumbe huo haukuishia hapo, unaendelea kueleza kwamba “Matokeo yake yatajionyesha baada ya muda, mbumbumbu hao wakishahitimu. Wagonjwa watafia mikononi mwa madaktari, majengo yataanguka mikononi mwa wahandisi, pesa zitapotelea mikononi mwa wachumi, utu utapotea mikononi mwa viongozi wa dini, na haki itapotelea mikononi mwa mahakimu.”

Moja ya maandiko ambayo yamekuwa yakisambaa katika mitandao ya kijamii katika siku za karibuni yanasomeka, “Kwenye geti la Chuo Kikuu cha Cape Town nchini Afrika Kusini kuna maandishi yasemayo ‘Ukitaka kuangamiza taifa lolote duniani huhitaji kutumia silaha za nyuklia wala mabomu ya atomiki. Njia nzuri ya kuangamiza taifa ni kuharibu mfumo wa elimu. Ruhusu mbumbumbu waonekane wamefaulu na wasonge mbele.”

Ujumbe huo haukuishia hapo, unaendelea kueleza kwamba “Matokeo yake yatajionyesha baada ya muda, mbumbumbu hao wakishahitimu. Wagonjwa watafia mikononi mwa madaktari, majengo yataanguka mikononi mwa wahandisi, pesa zitapotelea mikononi mwa wachumi, utu utapotea mikononi mwa viongozi wa dini, na haki itapotelea mikononi mwa mahakimu.”

Baada ya yote hayo, ukahitimisha kwa kusema, “Kuchezea elimu ni kuangamiza taifa.”

Juzi, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), lilieleza namna lilivyobaini mtandao wa wizi wa mitihani ya Taifa ya Darasa la Saba uliohusisha baadhi ya shule za mikoa mitatu nchini hali iliyoilazimu kufuta matokeo ya shule hizo na kuziagiza kufanya upya mitihani hiyo Jumatatu na Jumanne ijayo katika vituo watakavyopangiwa.

Jambo la kushangaza na kusikitisha zaidi ni kwamba katika mtandao huo, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma imetajwa kuhusika na shule zake zote za msingi kuingia katika kashfa hiyo. Shule nyingine zilizotajwa kuhusika ni Kondoa Integrity iliyopo, Kondoa pia mkoani Dodoma; Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za Dar es Salaam pamoja na Alliance, New Alliance na Kisiwani za Mwanza.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alikaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba uongozi wa Idara ya Elimu ya Halmashauri ya Chemba ulipanga kufanya udanganyifu kupitia kwa waratibu wa elimu kata, walimu wakuu na wasimamizi ili kuhakikisha ufaulu unainuka kwenye halmashauri yao kwa kuunda makundi maalumu ya WhatsApp kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano.

Japokuwa Serikali imeshatangaza kuchukua hatua kadhaa za kinidhamu dhidi ya wahusika ikiwamo kuwavua madaraka na kuwasimamisha kazi Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Chemba, Ofisa Taaluma (Msingi), Mratibu wa Elimu Kata ya Farkwa, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Farkwa, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugenika na waratibu elimu kata, tunadhani ipo haja ya kuchimba zaidi mzizi wa tatizo hili na kuung’oa ili usiote tena.

Kwa jinsi Dk Msonde alivyoeleza namna mtandao huo ulivyonaswa ukihusisha mawasiliano baina ya wahusika kutoka shule moja hadi nyingine, tunadhani kwamba ipo haja kwa vyombo vya kitaalamu vya uchunguzi kuendelea kuanzia hapo kwani shaka yetu ni kwamba huenda wapo ambao hawakutajwa lakini walihusika.

Tunaitaka Serikali kulichukua suala hili kwa uzito mkubwa kabisa kwani kama andiko lile tuliloanza kulirejea katika maoni haya linavyobainisha, tukichelea kuchukua hatua stahili kukomesha vitendo hivi, tutaliangamiza Taifa.

Aidha, tunataka hili liwe fundisho kwa Necta na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya mitihani kuhakikisha linaziba kila aina ya mwanya unaoweza kusababisha uvujaji wa mitihani kwa mosi; kutoa viapo kwa wote wanaokabidhiwa dhamana hii na pili; kupendekeza adhabu kali kabisa kwa wanaothibitika kukiuka. Tusichezee elimu.