In Summary
  • Awali, BMT ilitisha uchaguzi wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Februari 24 mkoani Dodoma na kuteua kamati ya muda kusimamia kazi za kiutendaji za BFT.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT), limetangaza tarehe ya uchaguzi wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), ambao umepangwa kufanyika Julai 7, mwaka huu.

Awali, BMT ilitisha uchaguzi wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Februari 24 mkoani Dodoma na kuteua kamati ya muda kusimamia kazi za kiutendaji za BFT.

Tarehe ya uchaguzi wa BFT ilitangazwa wiki iliyopita na Katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja.

Mbali na kutangaza tarehe ya uchaguzi, BMT imetaja kamati mpya ya kusimamia ngumi za kulipwa nchini itakayokuwa na wajumbe sita.

Wajumbe walioteuliwa ni Mwenyekiti, Emmanuel Saleh, Joe Enea (Makamu), Yahaya Pori (Katibu), Habibu Kinyogoli, Fike Wilson na Dk Killanga M Killanga.

Moja ya kazi ya kamati hiyo ni kuratibu mkutano wa kujadili rasimu ya katiba na kuandaa mkutano mkuu wa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Dodoma.

Kitendo cha BMT kutangaza tarehe ya uchaguzi ni jambo la faraja kwa familia ya ngumi ambayo muda mrefu imekosa viongozi thabiti wa kuongoza taasisi hiyo.

Uchaguzi wa Jula 7 ufungue sura mpya kwa kupata viongozi makini watakaokuwa na dhamira ya dhati ya kurejesha hadhi ya mchezo huo nchini.

BMT haikukurupa kusitisha uchaguzi wa Februari 24, bila shaka ilibaini uozo ndani ya shirikisho hilo kabla ya kupiga nyundo.

Nampongeza Kiganja kwa moyo wa ujasiri wa kuwangoa vigogo wa shirikisho hilo ambao walikuwa wamejimilikisha taasisi hiyo.

Mbali na kudumu muda mrefu BFT, lakini vigogo hao walikosa ubunifu na walinya kazi zao za kiutendaji kwa mazoezi hatua iliyodumaza ngumi.

Pia viongozi hao walishindwa hata kuwa na programu endelevu ya kuibua vipaji vipya kwa kuandaa mashindano mbalimbali kuanzia ngazi za chini ili kupata msingi mzuri wa mabondia chipukizi ambao watakuwa tegemeo la Taifa.

BMT imeonyesha njia, ni wajibu kwa wapiga kura kuchagua viongozi waliokidhi viwango na wenye weledi wa kufufua masumbwi na siyo vinginevyo.

Ni ukweli usiopingika uchaguzi wowote ule kila mpiga kura anakuwa na upande wake, lakini kwa hatua iliyofikia BFT ni vyema wakatathini kuhusu mweleleo wa mchezo huo nchini kabla ya kuchagua.

Wakati mwingine tumekuwa tukiwatolea macho viongozi wa vyama vya michezo na klabu, lakini kiini cha matatizo na wapiga kura.

Baadhi ya viongozi wa vyama au klabu hawaguswi kwa kuwa wanajua itakapofika wakati wa uchaguzi wataingia madarakani kwa kuwa wamewaweka kiganjani wapiga kura. Idadi kubwa ya wapiga kura hawachagui viongozi bora, badala yake wamekuwa wakichagua bora viongozi hata kama wanajua udhaifu wa viongozi wanaowapigia kura.

Ni vigumu kupokea mabadiliko, lakini wakati mwingine hakuna namna zaidi ya kuchukua uamuzi mgumu kubadili viongozi waliokaa madarakani muda mrefu bila kuleta mafanikio.

Kwa muda mrefu Tanzania imeshindwa kutamba katika mashindano ya kimataifa katika michezo mbalimbali ukiwemo ngumi.

Hivi karibuni wanamichezo wa Tanzania walirejea mikono mitupu katika michezo ya Madola iliyofanyika katika mji wa Gold Coast, Australia.

Hakuna sababu za msingi zilizotolewa kuhusu kuboronga Tanzania katika michezo hiyo zaidi ya viongozi na wanamichezo wenyewe kutoa visingizio vilivyozoeleka kila siku.

Mabondia waliokwenda ‘kutalii’ katika michezo hiyo ni Ezra Paul, Kassi Mbutike, Haruna Swanga na bondia mkongwe katika mashindano ya kimataifa Selemani Kidunda ambao wote walidundwa.

Ingawa maandalizi yetu yamekuwa ya zimamoto, lakini tumekosa mabondia hodari ambao watakuwa chachu ya kuiletea Tanzania medali katika mashindano ya kimataifa.

Kimsingi hatuna viongozi wanaoguswa na mchezo wa ngumi ambao wanataka kuurejesha katika hadhi yake kama zamani ambapo Tanzania ilikuwa kinara wa masumbwi kwa nchi za Afrika.

Huwezi kupata ladha ya ngumi kama ilivyokuwa miaka ya 1970 hadi 1980 ambapo Tanzania ilijivunia mabondia nyota waliokuwa na ngumi nzito kama kina Koba Kimanga au Timothy Kingu.

Tanzania ya leo huwezi kuwapata tena kina Benjamini Mwang’onda, Stanley Mabesi, Joseph Marwa, Somwe Patauli, Lucas Msomba na George Sabuni.

Pia Habibu Kinyogoli, Emmanuel Mlundwa, Zacharia na Michael Yombamba, Makoye na Willy Isangura, Nassor Michael, Onesmo Ngowi, Charles Mhilu ‘Spinks’, Emmanuel Kimaro ‘Sugar Ray’ na familia ya Matumla.

Tanzania bado ina nafasi nzuri ya kufanya vyema katika mashindano ya kimataida endapo tu viongozi wa vyama na klabu wangekuwa na dhamira ya kuleta maendeleo. Naamini muda wa kufanya mabadiliko upo endapo Watanzania watakuwa na dhamira.