In Summary

Hata kama wapo wanaojaribu kuikwepa hatua za udhibiti zimewekwa.

Katika nchi nyingi kodi ni chanzo kikuu cha mapato ya Serikali na ni wajibu wa kila mwananchi kuilipa.

Hata kama wapo wanaojaribu kuikwepa hatua za udhibiti zimewekwa.

Serikali hutumia mamlaka za kodi zenye jukumu la kutunza kumbukumbu za malipo na kukusanya fedha zinazohitajika kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali.

Mapato haya hukusanywa kutoka vyanzo tofauti. Baadhi ni kodi ya majengo, ya ongezeko la thamani (VAT), ushuru wa forodha na ule wa stempu. Kuna kodi ya mapato pia ambayo hukatwa kwenye mishahara ya watumishi wote, faida ya biashara na uwekezaji.

Kwa utaratibu uliopo, mapato hayo ambayo hukusanywa kama kodi hutumika kugharimia shughuli za Serikali kama vile kulipa mishahara na marupurupu ya watumishi, uendeshaji wa shule, hospitali, ujenzi wa barabara au miundombinu mingine muhimu ya sekta tofauti.

Kwa ufupi kodi huwahudumia walipaji wa sasa na baadaye kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla huku ikitumika kama chombo cha kupunguza tofauti iliyopo kati ya masikini na matajiri.

Kodi huwaweka katika mzani sawa walio na wasio nacho kwani mwenye uwezo mkubwa hulipa zaidi na kinyume chake ingawa matumizi ya matunda ya kodi hizo kama vile barabara imara hutolewa kwa wote bila ubaguzi.

Nchini, jukumu la ukusanyaji wa fedha hizo za Serikali linatekelezwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) na matumizi ya kinachopatikana hutekelezwa na Serikali baada ya kuidhinshwa na Bunge.

Kwenye ukusanyaji wa kodi, ushirikiano unahitajika na kila mmoja anatakiwa kusimamia haki na kutekeleza wajibu wake kuzikabili changamoto zinazojitokeza katika ulipaji na ukusanyaji wa mapato hayo ambazo nyingi zinatokana na uelewa mdogo juu ya haki na wajibu alionao kila mmoja.

Ni muhimu ikaeleweka kuwa, katika utekelezaji wa jukumu la ukusanyaji wa mapato, TRA inao wajibu kisheria ambao inapaswa kuuzingatia wakati wote ikiwa ni pamoja na kutoa makadilio sahihi ya kodi kwa mujibu wa sheria na huduma bora kwa wateja wake.

Vilevile, TRA wanaowajibu wa kushughulikia malalamiko na hoja zote zinazotolewa na walipakodi na wadau wengine kwa heshima, kutoa elimu na ushauri kwa Serikali na taasisi zake kuhusu sera na utekelezaji wa sheria za kodi.

Mlipakodi anaowajibu wa kutekeleza ambao ni pamoja na kujisajili, kuwasilisha ritani na nyaraka zake zilizojazwa kwa usahihi na kulipa kodi aliyokadililiwa kwa wakati kama ilivyoainishwa kisheria.

Mlipakodi pia ana wajibu wa kutoa stakabadhi za mauzo na ankara za kodi za kielektroniki ambazo kila mteja wa biashara yake ana haki ya kudai stakabadhi hizo za ununuzi sanjali na kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA kutimiza wajibu wao kisheria bila kuwaingilia, kuwatisha, kuwadharau au kuwashawishi kwa namna yoyote ile kuenenda kinyume na utaratibu uliopo.

Hata hivyo, mlipakodi ana haki zake ambazo zinamlinda. Kwanza, anayo haki ya kutekeleza sheria ya kodi kwa uadilifu wakati wa kukadilia kiwango cha kodi anachostahili kulipa isipokuwa kama kuna ushahidi unaoonesha vinginevyo.

Pili, mlipakodi ana haki ya kupata faragha wakati wote pamoja na usiri wa taarifa zake binafsi na za biashara yake zinazopelekwa TRA isipokuwa kwa mamlaka zinazotambulika na kuruhusiwa na sheria zilizopo.

Anayo haki ya kupinga makadirio au maamuzi mengine yoyote yaliyofanywa na TRA katika mazingira ambayo haki hiyo inasimamiwa kisheria.

Kadhalika, kila mlipakodi anayo haki ya kupanga masuala yake ya kodi, kwa kuwatumia wataalamu waliothibitishwa ili kupata faida kwa kiwango cha juu kinachoruhusiwa na sheria za kodi.

Haki hizo na wajibu wa TRA zipo kwa mujibu wa sheria na huenda kila mtu angefanya vyema katika nafasi yake kusingekuwepo na mikanganyiko mingi kwa pande zote mbil katika suala la ukusanyaji wa kodi.

Kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo hakutakuwa na kukimbizana wala kukwepana kati ya mlipaji kodi na mkusanyaji.

Aidha, kanuni za kulipa kodi kwa mujibu wa mtaalamu wa kodi, Adam Smith ni pamoj ana kuwa rahisi kutekeleza wajibu huo. Adam anasema utaratibu wa kulipa ukishakuwa mgumu basi kodi hiyo haifai na inapaswa kufutwa mara moja.

Urahisi katika ulipaji wa kodi huepusha kero kwa wafanyabiashara na kutoshawishi ukwepaji miongo mwa walipaji bila kujali uwezo wake kiuchumi. TRA inapaswa kuyafanyia kazi maeneo yote yenye changamoto

Mwandishi anapatikana jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwa namba 0756939401