In Summary
  • Mfano wa rasilimali hizo ni ruzuku itolewayo kwa kila shule, walimu wenye sifa na wazoefu, idadi ya vitabu, majengo na uwepo wa teknolojia wezeshi katika kujifunza.

Kutokuwapo kwa usawa katika kujifunza maana yake ni kutokuwa na uwiano ulio sawia wa rasilimali za kielimu, huduma na katika matokeo ya kujifunza.

Mfano wa rasilimali hizo ni ruzuku itolewayo kwa kila shule, walimu wenye sifa na wazoefu, idadi ya vitabu, majengo na uwepo wa teknolojia wezeshi katika kujifunza.

Hii ndio hali halisi ya elimu wanayopata watoto wetu wa shule za misingi na sekondari hasa zile za umma.

Elimu aipatayo mtoto anayesoma shule ya umma iliyoko kijijini si sawa na ya yule anayesoma katika darasa hilo hilo kwenye shule ya mjini.

Tumekuwa tukishuhudia namna watoto katika shule binafsi wanavyofanya vizuri katika mitihani, kwa kuwa shule hizo zina miundombinu mizuri na vifaa vya kujifunzia.

Ripoti ya utafiti wa Uwezo iliyoko Twaweza isemayo “Je, Watoto Wetu Wanajifunza? Iliyotoka mwaka 2017, inaonyesha bado hakuna usawa kwenye matokeo ya kujifunza, vifaa na huduma zipatikanazo shuleni.

Tafiti hiyo inaeleza kuwa, miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka tisa hadi 13 nchini, asilimia 38 hawawezi kufanya majaribio ya darasa la pili, huku tofauti kubwa ikionekana kwenye wilaya.

Wakati Wilaya ya Iringa Mjini, ikiongoza kwa ufaulu wa asilimia 75 ya watoto wenye umri wa miaka tisa hadi 13, kwa kuwa na uwezo wa kufaulu majaribio ya kusoma Kingereza na Kiswahili na kufanya hesabu rahisi, Wilaya ya Sikonge ilifanya vibaya kwa kupata asilimia 17.

Kimkoa, asilimia 64 ya wanafunzi mkoani Dar es Salaam wenye miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio yote matatu, lakini kwa upande wa wenzao mkoani Katavi ni asilimia 23 pekee ya watoto wanaoweza kufaulu majaribio hayo

Aidha, taarifa ya Twaweza ya hivi karibuni iliyotolewa kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa eneo analoishi mtoto lina mchango mkubwa kwenye matokeo ya kujifunza kuliko umasikini na mambo mengine yaliyokuwa yakiainishwa hapo awali.

Watoto wanne kati ya 10 (sawa na asilimia 42) kutoka kaya masikini sana walifaulu majaribio yote matatu ukilinganisha na karibu watoto sita kati ya 10 (asilimia 58) kutoka kaya zenye uwezo.

Pia takwimu zinaeleza kuwa mkoani Kilimanjaro wanafunzi 26 wanatumia choo kimoja, lakini mkoani Geita ni wanafunzi 74 au mara tatu zaidi ya wanafunzi.

Vilevile, asilimia tano ya shule mkoani Geita zinatoa huduma ya chakula cha mchana wakati mkoani Kilimanjaro ni asilimia 79.

Japokuwa ipo sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu suala zima la usawa katika kupata huduma ya elimu bora, takwimu hizi zinatoa fursa kwa watunga sera kuelekeza juhudi na rasilimali kwenye maeneo ya pembezoni zaidi na kwa watoto wenye uhitaji zaidi.

Kimsingi, matabaka katika kujifunza yanajitokeza kwenye mlolongo wa vizazi; ambapo matokeo ya tafiti yanaeleza kuwa, watoto watatu kati ya wanne (74%) ambao mama zao wana elimu ya sekondari au elimu ya juu, walifaulu majaribio yote matatu ukilinganisha na asilimia 46 ya watoto ambao mama zao hawakusoma.

Ukiangalia takwimu hizi na nyinginezo ambazo makala haya haikuweza kuzitaja, utagundua kuwa kukosekana kwa usawa kwenye mfumo wa elimu, kunajidhihirisha katika matokeo ya kujifunza, mgawanyo wa rasilimali na upatikanaji wa huduma muhimu shuleni kama vile maji safi na salama, chakula na umeme.

Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa watoto na wilaya za mwisho haziachwi nyuma.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini na kukubalina kutekeleza malengo endelevu ya milenia(SDGs) na miongoni mwa malengo hayo ni lengo namba nne linalohusu utoaji wa elimu bora.

Katika kuhakikisha lengo hili linafanikiwa na watoto wote wanakwenda shule na kupata elimu bora, Rais John Magufuli, alitangaza kufuta michango shuleni ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo.

Pamoja na elimu kutolewa bure, bado kuna changamoto hivyo ni vizuri Serikali kwa kushirikiana na wadau wasaidiane kuangalia namna ya kupunguza au kumaliza kabisa changamoto zinazochangia kuwapo kwa pengo katika kujifunza kati ya wanafunzi wa eneo moja na jingine.

Hii itafanya watoto wote kupata elimu bora, na hatimaye mafanikio mazuri kielimu na kiuchumi kwa wote nchini bila kujali maeneo wanayotoka au familia wanazoishi.

Tukiwa na wasomi walioelimika barabara katika kila kona ya nchi, watatupeleka mapema kwenye nchi ya viwanda kama ilivyo ndoto yetu kama taifa.

Greyson Mgoi ni ofisa wa mawasiliano wa Uwezo-Tanzania, Twaweza. Anapatikana kwa barua pepe: [email protected]