In Summary
  • Alitoa mfano wa mkuu mmoja wa wilaya aliyefikia hatua ya kumkadiria kodi mwekezaji baada ya kubaini kwamba alikuwa hatimizi wajibu huo wa kisheria.

Katika toleo letu la jana tulikuwa na habari ambayo kwa kiasi kikubwa ilimnukuu mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe akiwataka viongozi wa Serikali kuacha kutoa maagizo na kujichukulia hatua bila kuwasiliana na mamlaka husika katika uwekezaji.

Alitoa mfano wa mkuu mmoja wa wilaya aliyefikia hatua ya kumkadiria kodi mwekezaji baada ya kubaini kwamba alikuwa hatimizi wajibu huo wa kisheria.

Kwa msisitizo, Mwambe alisema kuna sheria, kanuni na taratibu za kufuata ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa mamlaka ambazo zinahusika moja kwa moja na masuala ya uwekezaji, hivyo ni vyema viongozi hao wanapokutana na changamoto kama hiyo wakatoa taarifa huko.

Kauli hiyo ya mtendaji huyo mkuu wa TIC imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya kukaririwa na vyombo vya habari akitoa amri ya kukamatwa kwa mkurugenzi wa kampuni ya Tudeley Estates Limited inayomiliki mashamba kwa madai ya kukwepa kodi ya Sh713 milioni kwa miaka saba.

Mbali na hatua hiyo, mkuu huyo wa wilaya pia aliamuru meneja wa kampuni hiyo, Trevor Gifford anyang’anywe hati ya kusafiria hadi pale fedha hizo zitakapolipwa.

Mwambe aliwataka viongozi wa Serikali ngazi zote kushirikiana lakini kila mmoja katika taasisi yake akisisitiza, “Tusiingiliane katika majukumu, kama ni vibali vya kuishi kamishna wa Uhamiaji yupo, kama ni vibali vya kazi, kamishna wa Kazi yupo.”

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu hasa kutoka kwa watendaji wa umma aghalabu wataalamu katika sekta mbalimbali kwamba baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitoa matamko ambayo yanaathiri utendaji wa taasisi na mihimili mingine.

Mathalani, Januari mwaka huu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma akitoa ujumbe kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria alisema, “Nawasihi viongozi wote wa Serikali wenye mamlaka za kikatiba na kisheria, wabaki ndani ya maeneo yao ya kikatiba na wajiepushe na kuingilia maeneo yaliyo ndani ya haki, hadhi na mamlaka ya Kikatiba ya Mahakama.”

Akaongeza kwamba kuanzia sasa (Mahakama) watakuwa wakali kwa mtu atakayeingia katika anga zao, huku akiwataka mahakimu na majaji kuchukua hatua kwa watu wanaodharau amri zao, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, akisisitiza kuwa mamlaka ya utoaji haki ni ya Mahakama pekee.

Tunaiona kiu ya kila kiongozi kumsaidia Rais John Magufuli katika kutimiza ahadi yake ya kuwaletea wananchi maendeleo na kupambana na dhuluma na ufisadi. Hata hivyo, pamoja na nia hiyo njema, baadhi yao katika kutekeleza hilo, wamejikuta wakiingilia maeneo mengine ambayo yanahitaji taaluma au usimamizi wa kisekta hivyo kuathiri lengo lililokusudiwa.

Wahenga wana msemo maarufu usemao, “Tunajenga nyumba moja, hakuna haja ya kugombea fito.” Tunaamini kwamba kama viongozi wakichukua nafasi yao usimamizi mafanikio yaliyokusudiwa yatafikiwa na pasi na shaka watakumbukwa kwa mchango wao.

Tunasisitiza katika nukta ya kushirikiana tena tukiongeza neno ‘kikamilifu’ lakini kila mmoja atimize wajibu wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.