Zamani, iliaminika kazi ni kipimo cha utu. Ilikuwa huwezi kueleweka kama hujishughulishi. Hali imebadilika siku hizi hasa kwa vijana, wengi hawataki kuhangaishwa.

Kazi ina historia ndefu kama yalivyo maisha ya binadamu mwenyewe. Mababu zetu waliishi kwa kuwinda msituni na kutafuta chakula. Zama zimebadilika, sasa chakula kinanunuliwa. Na kila kitu kingine kinapatikana kutegemea fedha ulizonazo. Kazi za sasa zinafanywa tofauti na ilivyokuwa zamani.

Wakati mababu zetu walikuwa wanachimba mizizi kwa mawe, sasa hivi kilimo kinafanywa kwa mitambo ya kisasa…kuanzia kuandaa shamba, kulima mpaka kuvuna na kuweka mavuno husika kwenye madaraja tofauti.

Mababu zetu walikuwa na uwezo wa kutembea msituni kutafuta chakula bila uhakika wa kukipata, siku hizi unaenda sokoni ukiwa na uhakika wa kununua ukitakacho kwa asilimia 100. Chakula cha sokoni kinanunuliwa na fedha ambayo ni matunda ya kazi unayoifanya.

Pamoja na ukweli huo, lakini tupo kwenye zama ambazo vijana wengi hawapendi kufanya kazi. Hawapendi usumbufu wa kujishughulisha na wanaziogopa zaidi kazi zenye shuruba ambazo usipokuwa makini ni rahisi kukupa msongo wa mawazo. Hawako tayari kwa hilo. Wao wanataka maisha yasogee bila kuvuja jasho. Ikiwezekana, ndani ya kiyoyozi.

Vijana wanataka kazi ambayo haina usumbufu ingawa ukijiuliza ni ipi unaweza kufanya ukiwa umelala itakuchukua muda mrefu kupata majibu. Unaweza kuamini kazi hiyo haipo lakini wapo vijana wanaopingana na ukweli huo.

Najua vijana wengi kwa sasa wanapenda kuingia mitandaoni kuchati na kufuatilia habari za hapa na pale. Na wengine wangependa muda mwingi wautumie huku mitandaoni. Lakini, ukweli ni kwamba, umefika wakati wa kuachana na uzembe na kufanya kazi.

Vijana wanasahau kwamba vifaa vyote wanavyotumia kuanzia simu, tablet hata kompyuta mpakato ni matokeo ya kazi zilizofanywa na vijana wenzao wasiotaka njia za mkato kufanikisha ndoto zao.

Si hilo tu mitandao ya kijamii yenyewe mfano Facebook, instagram au Twitter ni matokeo ya juhudi za watu, tena vijana.

Kuna watu wamekaa na kujituma sana kufanikisha kuiunda. Mwisho wa siku wamatengeneza hivyo vifaa ambavyo vijana wa nchini hawataki kuviachia kwa kisingizio cha kwenda na wakati. Wao wanaita usasa.

Kuna baadhi ya shughuli vijana wa leo wanazidharau na kuziona hazina maana au si za viwango vyao. Vijana wengi hawapendi kilimo na wanakiona kama kazi ya watu wanyonge au waliokosa ajira.

Vijana wakumbuke na kufahamu, kazi ni kazi tu, na kila moja ni muhimu kwa ustawi wa nchi. Wao ndio wanaopaswa kujenga uchumi imara wa Tanzania lakini cha ajabu wanaopenda zaidi ajira za ofisini na wanapozipata hawaweki juhudi kutimiza majukumu yao.

Wanachelewa kazini na wakifika wanalipua majukumu waliyopewa. Sasa umefika wakati wa vijana kupenda nje ya ajira ili kuchangia kipato cha kaya.

Ifahamike, nyuma ya mafanikio makubwa kuna kazi imefanywa kwa ufasaha. Ukiwaona watu waliofanikiwa kiuchumi kama Aliko Dangote, Mo Dewji na wengine usifikiri wanakaa tu wakila bata. Hawa ni watu wa kazi. Vijana tukumbuke kazi ndio kipimo cha utu na hutufanya tujenge heshima yetu mbele ya jamii.

Hebu tupende kazi ili tuijenge Tanzania. Kila mmoja aanze kutimiza majukumu yake kwa viwango vya juu hata kama ni madogo kiasi gani kwani ukiyaweza madogo kwa utimilifu hata ukikabidhiwa makubwa zaidi, hakika utayamudu vyema.

Kama kweli wewe hupendi kazi, basi chukia na matokeo yake. Kama hupendi kazi basi usile. Chukia nguo nzuri na vitu vyote vya kisasa vinavyohitaji kununuliwa kwani vinahitaji ufanye kazi ili upate fedha.

Achana kabisa na mpango wa kuambatana na watu wa maana kwani ili uongee nao vitu muhimu ni lazima mkae sehemu yenye utulivu ambayo kwa namna yoyote utailipia tu.

Huwezi kuwa na rafiki atakayekuwa anagharamia mambo yenu kila siku halafu wewe ukawa mtumiaji tu. Kaa nyumbani kuanzia leo. Usitoke kwani kutoka kuna gharama ambazo zinakutaka ufanye kazi uweze kuzihimili.

Ikiwezekana usioe wala kuolewa kwa sababu utaongeza ugumu wa maisha yanayohitaji kusaidiana katika gharama zilizopo.

Mwandishi ni mhitimu wa chuo kikuu, muelimishaji wa masuala ya biashara na uchumi. Kwa ushauri na maoni, anapatikana kwa namba 0755848391