Miongoni mwa magonjwa yanayoitesa jamii kwa sasa ni saratani ambayo imegawanyika katika makundi tofauti ikiwamo ile ya uzazi, koo na matiti. Juhudi kubwa zimeendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao takwimu zinaonyesha umekuwa ukiongezeka kwa kasi.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) na lile la Afya Duniani (WHO), kila mwaka inakadiriwa kuwapo kwa wagonjwa wapya milioni 18.1 duniani kote na kati yao zaidi ya milioni 9.6 hufariki dunia.

Hata hivyo, licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa bado saratani imeendelea kuisumbua jamii kwa kuwa wagonjwa wapya wamekuwa wakigundulika kila uchao.

Inawezekana kupatikana kwa wagonjwa wapya kunasababishwa na msisitizo au elimu inayotolewa kwa jamii katika kukabiliana na ugonjwa huo, hivyo kuna haja ya kuboresha eneo hilo.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema yapo mambo mbalimbali ambayo iwapo mtu atayazingatia, bila shaka uwezekano wa kujikuta akipatwa na saratani utapungua na iwapo jamii itafanya hivyo kwa ujumla wake, basi itakuwa salama zaidi.

Wakati jana Watanzania tuliungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Saratani, ni muhimu na vyema kwa kila mtu kujiwekea utaratibu wa kuhakikisha anaifahamu vyema saratani ili aweze kuchukua hatua za kukabiliana nayo.

Mojawapo wa mambo ya msingi kufahamu ni kwamba, hakuna sababu maalumu inayochangia au kusababisha saratani, lakini matumizi ya vinywaji fulani kwa wingi au aina mwenendo fulani wa maisha huchangia uwezekano wa kukumbwa na ugonjwa huo.

Baadhi ya mambo hayo ni uvutaji wa sigara, unywaji pombe na ulaji wa aina fulani za vyakula vikiwamo vyenye mafuta mengi ambavyo pia vinaelezwa kuchangia katika magonjwa ya moyo. Ni muhimu pia kuzifahamu dalili za saratani japo zile za kawaida kama uvimbe usiokwisha, mabadiliko ya ngozi, unyong’onyevu, maumivu yasiyoelezeka, joto kali mwilini na kupungua kwa uzito wa mwili bila sababu za msingi.

Mbali na hayo, ni muhimu pia kufahamu kwamba saratani si ugonjwa wa kuambukiza na hivyo uwezekano wake wa kuambukiza ni mdogo.

Tunaamini kwa kuyafahamu mambo hayo muhimu japo kwa uchache unaweza kuwa mwongozo wako katika kujilinda dhidi ya saratani na kuwalinda wengine.

Kwa kuwa “hali ya hatari” dhidi ya saratani inaweza kubadilishika, ni vyema tukabadilisha mfumo wa maisha hususan katika ulaji wa vyakula, unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji sigara. Si hivyo tu, ni vyema kila mtu kuanzia sasa akauona umuhimu wa kubadilika ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Watanzania tuungane katika mapambano dhidi ya saratani, tukiunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali na wadau wengine ambazo ni pamoja na huduma za uchunguzi na matibabu katika maeneo mbalimbali nchini kwa kufika vituo vya afya kupima.

Pia, ni vyema tukajijengea utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili, kula vyakula bora na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Kwa upande wake, Serikali iongeze kasi ya kutoa elimu hususan kwa wananchi waliopo maeneo ya pembezoni ambao inawezekana wako hatarini zaidi kutokana na umbali uliopo kati yao na vituo vya huduma za afya.

Pia, ni vyema Serikali ikaendelea kusogeza huduma za upimaji na matibabu ya saratani karibu na wananchi ili kuwafikia watu wengi na kuondoa uwezekano wa mtu kuchelewa kugundulika au kuanza tiba kutokana na umbali wa kufika sehemu ya huduma ya afya.