Kuhakikisha kuwa kila mmoja bila kujali maumbile, jinsia yake au hali yake kiuchumi ana nafasi sawa ya kupata elimu bora bado ni changamoto duniani kote.

Lengo namba 4 la Maendeleo Endelevu kuhusu elimu linasisitiza kuwa ujumuishaji na usawa katika utolewaji wa elimu ndio msingi wa elimu bora.

Lakini kumekuwa na uelewa tofauti katika jamii na hata miongoni mwa watekelezaji wenyewe kuhusu dhana ya elimu jumuishi.

Elimu jumuishi ni mfumo wa utoaji elimu unaozingatia na kukidhi mahitaji binafsi kwa kila mwanafunzi katika ujifunzaji, ambao mtoto mwenye ulemavu na asiye na ulemavu wanajifunza pamoja katika darasa moja.

Elimu jumuishi haimaanishi tuwe na shule maalumu kwa watoto wenye mahitaji maalumu pekee, shule kama hizi zinawatenga watoto wenye changamoto na ambao hawana changamoto.

Lakini pengine jambo kubwa zaidi ni kuwa kwa kufanya hivyo tunawatenga na jamii ambayo tayari ni jumuishi ambayo watakuja kuishi wakimaliza masomo yao.

Watoto wenye mahitaji maalumu wakimaliza shule hawatakuja kuishi katika jamii yenye mahitaji maalum kama shule walizotoka za vitengo bali, wataishi katika jamii jumuishi.

Elimu jumuishi inalenga kutoa elimu kwa watoto wote katika shule moja bila kujali wana hali gani au upungufu gani. Kupitia darasa jumuishi watoto wanajifunza kuishi pamoja; wasio na mahitaji maalumu huwaona wenye mahitaji ni wanadamu kama wao lakini pia wenye mahitaji maalumu hujiona kuwa ni sehemu ya jamii ambamo watakuja kuishi baada ya kumaliza elimu yao.

Hivyo, shule inayotoa elimu hiyo inapaswa kuwa na mazingira rafiki kwa watoto wa hali zote, yaani miundombinu mizuri, madarasa yanayofikika kirahisi yasiyo na ngazi ndefu, barabara za shule zisizo na vikwazo kama mashimo au mawe.

Aidha, inapaswa iwe na walimu wenye ujuzi wa kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu, vifaa pamoja na vitabu stahiki vya watoto.

Darasa jumuishi pia linapaswa kuwa darasa lenye watoto wasiozidi 35 miongoni mwake wakiwamo wenye mahitaji maalumu wasiozidi watano.

Pia, mpangilio wa madawati darasani uwape fursa watoto wenye mahitaji maalumu. Pia panapaswa kuwapo walimu wasaidizi kwa watoto wakati mwalimu wa somo anafundisha.

Je, kwa upande wa Tanzania hali ikoje? Nadhani ni wachache watakaobisha kuwa kundi la watoto walemavu bado linakabiliwa na changamoto nyingi.

Kwa mfano ripoti ya HakiElimu ya mwaka 2018 imebainisha changamoto nyingi katika utolewaji wa elimu jumishi hasa kwa watoto wasioona na wenye uoni hafifu.

Mazingira ya shule nyingi si rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu. Mathalani, madarasa yana ngazi ndefu ambapo mtoto mlemavu hawezi kuingia au kutoka kirahisi. Pia kuna upungufu wa vifaa na vyoo pamoja na walimu wenye taaluma ya elimu maalum. Pia walimu hawana miongozo ya kufundisha darasa jumuishi.

Mathalani, Shule ya Sekondari Mkolani, iliyopo wilaya ya Nyamagana Mwanza inajulikana kuwa inatoa elimu jumushi.

Shule hii ina watoto wenye wenye mahitaji maalum ambapo wengi wao ni watoto wenye ualbino na watoto wenye changamoto za uoni.

Kwa kweli mazingira ya shule hii si mazuri kwa watoto wenye mahitaji maalum. Miundombinu yake hasa madarasa yana ngazi ndefu, bweni lipo nje kidogo ya shule ambapo kuna kolongo kubwa lenye mteremko mkali linalotenganisha mabweni na madarasa.

Mtu unajiuliza, hivi wakati linajengwa wahusika hawakujua kutakuwa na watoto wenye mahitaji maalum?

Katika hali kama hii tuna haki kweli ya kujitapa kuwa tuko pamoja na watoto wenye mahitaji maalumu katika utolewaji wa elimu?

Elimu jumuishi ya kweli ingemaanisha kuwa si watendaji tu bali pia na jamii ingezingatia dhana na malengo ya elimu jumishi.

Pia, Serikali na wadau wangewatimizia watoto hawa mahitaji yao ili waweze kujifunza shuleni na kupata elimu bora kama watoto wengine, na hapangekuwa na wazazi wanaoendelea kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum.

Kama mazingira yangekuwa rafiki, wazazi wengi wasingesita kuwapeleka watoto hao shule na kufuatilia maendeleo yao kwani watoto hawa wameonyesha uwezo mkubwa wanapopewa nafasi..

Bado tuna safari ndefu kuifikia elimu jumuishi. Kila mmoja wetu inampasa awajibike.

Peter Letema ni mhasibu katika shirika la HakiElimu. Anapatikana kwa baruapepe; [email protected]