Mimba za utotoni bado limeendelea kuwa tatizo sugu nchini.

Pamoja na Serikali, asasi zisizo za kiserikali na wadau wengine kuguswa na hata kubuni mipango na mikakati mbalimbali, mimba za utotoni zinabaki kuwa miongoni mwa changamoto tete zinazolikabili Taifa letu kwa miaka nenda rudi.

Tunaweza tusiwe na takwimu za hivi karibuni zaidi, lakini taarifa za Mei mwaka jana kwamba wasichana 18,000 wenye umri wa chini ya miaka 18 katika Mkoa wa Tabora pekee walipata mimba katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huo, zinabaki kuwa kielelezo cha kuonyesha ukubwa wa tatizo hili ambalo sio tu linaathiri mustakabali wa wahusika, lakini hata Taifa nalo linayumba.

Hili bila shaka sio suala dogo na katu hatupaswi kulipa kisogo kwa vile tu limekuwapo kwa siku nyingi huku likionekana kama ada au jambo la kawaida kwa baadhi ya watu. Ni suala kubwa na linalogusa jamii pana ya Watanzania.

Ni kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, tunaona umuhimu wa haraka wa wadau wote kuamka na kuingilia kati suala hilo kabla halijaleta madhara makubwa zaidi. Tunaposema wadau tunamaanisha Serikali na vyombo vyake, wazazi, walimu, asasi zisizo za kiserikali na vyombo vya habari na kila anayeguswa na madhara yatokanayo na mimba za utotoni.

Haipendezi mimba za utotoni kuwa wimbo wa kila siku. Tungependa kuwashauri wadau kutafuta kiini cha tatizo ili wimbo huu hatimaye upotee katika masikio ya Watanzania. Tunapaswa kujiuliza kwa nini takwimu za mimba za utotoni kila siku zinaongezeka badala ya kupungua.

Ni bahati mbaya kwamba jamii inalitazama jambo hili baada ya madhara kutokea na watoto kupata ujauzito, lakini kiini cha tatizo lenyewe kinaachwa bila kufanyiwa kazi.

Ni mara chache kama jamii tumekuwa tukijadili matatizo yanayowasibu watoto kike, yakiwamo ya mila, umaskini wa wazazi, desturi na imani zinazowalazimisha kuolewa mara tu wanapovunja ungo na kunyimwa elimu na mara nyingine kukosa matunzo stahiki kulingana na maumbile yao na hivyo kujikuta wanalazimika kuwategemea wanaowaingiza kwenye mitego ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Tunatambua kuwapo kwa jitihada za dhati zikiwamo zinazofanywa na Serikali. Imani yetu ni kuwa juhudi hizo zinatakiwa kuwa za kina, haraka na zinazoonekana ili kuokoa maisha ya watoto hawa wa kike ambao maisha na ndoto za maisha yao zinaharibiwa na hatimaye kuwa mzigo kwa Serikali.

Mpaka Mei mwaka jana, takwimu za mimba za utotoni kwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19, zinaonyesha tatizo hilo lipo kwa wastani wa asilimia 27 kitaifa.

Hii ni kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Hizi si takwimu za kubeza wala za kutamkwa jukwaani kisha zikaachwa zipotee hewani. Mimba za utotoni zinapaswa kumgusa kila mmoja wetu, ndio maana pamoja na mambo mengineyo tunasisitiza ushirikishwaji na utoaji wa elimu kwa jamii pana zaidi. Imani yetu ni kwamba ikiwa tutajikita katika kubadili fikra na mitazamo, mimba za utotoni zinaweza kutokomezwa.