Kila ifikapo Februari 4 ya kila mwaka huwa tunaadhimisha Siku ya Saratani Duniani. Tanzania kama zilivyo nchi nyingine nayo hushiriki maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yalifanyika Jumatatu ya wiki hii.

Neno saratani limetokana na neno la Kiarabu “sartan” na kansa imetokana na neno la Kiingereza “cancer”.

Saratani ni jina la jumla linalojumuisha kundi la magonjwa zaidi ya 100.

Ni aina ya ugonjwa unaotokana na seli za mwili zinazoanza kugawanyika na kukua bila utaratibu wa kawaida unaodhibitiwa na mwili.

Ukuaji huu huleta uvimbe mwilini unaozidi kuwa mkubwa hadi kubana viungo vya mwili kama neva, mishipa ya damu, ubongo, mapafu, maini, utumbo na kadhalika hivyo kuzuia visifanye kazi na kusababisha maumivu makali na hata kifo.

Vilevile saratani huenea au kusambaa kutoka kiungo kimoja cha mwili na kwenda kiungo kingine kupitia mfumo wa limfu (lymphatic system) na mfumo wa damu ambao kitaalamu huitwa (metastasis).

Ni vyema tutafakari kwa pamoja kuhusu ugonjwa huu na tutafute namna bora za kupambana nao.

Ugonjwa huu hatari wa saratani ambao unazidi kuongezeka na kugharimu afya na maisha ya watu, unaathiri nguvu kazi na kuongeza kiwango cha umasikini kwa familia, jamii na hata Taifa.

Ugonjwa huu huathiri kiungo chochote cha mwili mfano mapafu, mifupa, matiti, shingo ya kizazi, tezi dume, koo la chakula, ngozi, shingo na kichwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), saratani imeathiri watu milioni 18.1 na kusababisha vifo takribani milioni 9.6 duniani kwa kipindi cha mwaka 2018.

Kutokana na ufuatiliaji huo wa WHO uliofanyika kwenye nchi 185 katika aina 36 za saratani, mwanamume mmoja kati ya watano na mwanamke mmoja kati ya sita wanakadiriwa kupata saratani katika maisha yao.

Na mwanamume mmoja kati ya wanane na mwanamke mmoja kati ya 11 wanaweza kufa kutokana na saratani.

Kwa maana nyingine saratani ni ugonjwa usioambukiza ambao unaongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani ikilinganishwa na Ukimwi, malaria na kifua kikuu yakijumuishwa kwa pamoja.

Kwa nchi yetu hakuna taarifa rasmi za kitafiti zinazoonyesha ukubwa halisi wa ugonjwa huu ingawa kuna taarifa zitolewazo na hospitali za kanda kama KCMC, Bugando, Mbeya na Muhimbili.

Kutokana na vyanzo hivi, inakadiriwa kuwa saratani inaongezeka kwa kasi ambapo watu zaidi ya 35,000 hugunduliwa kuwa nayo na zaidi ya 21,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.

Inaelezwa pia kwamba, asilimia 26 tu ya wanaogunduliwa kuwa na saratani ndio hufika hospitali kwa ajili ya matibabu na katika hawa, zaidi ya asilimia 80 hufika wakati ugonjwa umeshafika katika hatua za juu yaani hatua ya tatu na ya nne na kufanya matibabu kuwa magumu zaidi.

Miongoni mwa vihatarishi vya saratani ni maambukizi (infections) ambapo inakadiriwa zaidi ya asilimia 66 ya saratani zinachangiwa na maambukizi au vya virusi ama ya bakteria.

Vihatarishi vingine ni pamoja na unywaji pombe uliopitiliza, uvutaji wa sigara, uzito uliopitiliza, mionzi hatarishi itokanayo na jua hasa kwa wenye ulemavu wa ngozi, masuala ya jenetikia, lishe duni na wakati mwingine hali inayoambatana na umri mkubwa (kuanzia miaka 50).

Dalili za ugonjwa wa saratani zinafanana na magonjwa mengine, jambo ambalo huchangia ucheleweshwaji wa ugunduzi. Vilevile dalili za saratani iliyopo katika eneo moja huweza kutofautiana na saratani iliyopo katika eneo lingine. Miongoni mwa dalili za ujumla ni uvimbe usio na sababu (swelling), maumivu (pain), kufifia kwa uwezo wa kuona, kukumbuka au kusikia kama saratani husika ipo kwenye eneo la kichwa, kutokwa na damu kama saratani imetengeneza kidonda, kushindwa kumeza chakula ikiwa saratani ipo katika koo la chakula na kidonda kisichopona.

Zipo njia mbalimbali za kitaalamu za kufanya uchunguzi ili kugundua ugonjwa huu na namna za kuutibu.

Saratani kama yalivyo magonjwa mengine yasiyoambukiza tunaweza kujikinga kwa kuepuka vihatarishi ama vipekelezi vyake.

Hii ni pamoja na kubadili mifumo mibaya ya maisha kama uvutaji sigara, unywaji pombe uliopitiliza, kujikinga dhidi ya mionzi hatari ya jua, kula mlo kamili na kufanya mazoezi ya mwili.

Pia tuepuke mahusiano katika umri mdogo na kujenga tabia au utamaduni wa kupima afya zetu mara kwa mara. Hii itasaidia mwili kuwa imara na kujijengea kinga ya kuweza kupambana na magonjwa mengine yasiyoambukiza hasa satarani.

Mwandishi wa uchambuzi huu ni mtaalamu wa mionzi na tiba kutoka Ocean Road, anapatikana kwa simu namba; 0766-277335