In Summary
  • Mtu anapofariki dunia ndugu, jamaa na marafiki zake wa karibu hujitokeza kwenye msiba na kusimamia shughuli zote hadi msiba unapomalizika. Wengi huchanga ama kuchangishana fedha nyingi kwa ajili ya mazishi. Bajeti kubwa ama fedha nyingi hutumika hata kinyume na makadirio kwa kuwa watu wengi hujitoa kwa hali na mali.

Ndugu, jamaa ama rafiki zetu wanapofariki dunia tunakuwa na huzuni na majonzi tele. Mara nyingi umuhimu wa mtu huonekana dhahiri kipindi ambacho hayupo. Unaweza usione umuhimu wake awapo hai, bali anapofariki duni utaanza kuona upungufu sehemu fulani na ndipo umuhimu wake unaanza kuonekana.

Mtu anapofariki dunia ndugu, jamaa na marafiki zake wa karibu hujitokeza kwenye msiba na kusimamia shughuli zote hadi msiba unapomalizika. Wengi huchanga ama kuchangishana fedha nyingi kwa ajili ya mazishi. Bajeti kubwa ama fedha nyingi hutumika hata kinyume na makadirio kwa kuwa watu wengi hujitoa kwa hali na mali.

Wafiwa hufarijika wanapopewa pole na kuwaona ndugu pamoja na marafiki wengi ambao hawakuweza kuonana kipindi kirefu. Lakini msiba unapomalizika na matanga ya ndugu kumalizika, huzuni na majonzi zaidi hutawala kwa wafiwa kwa kuwa wanabaki peke yao.

Watu wengi, hususan wa mjini wapo ‘bize’ sana na mambo yao binafsi. Ni baadhi tu ya ndugu ambao huwa na utaratibu wa kutembeleana au baadhi hujitokeza pale wanaposikia mtu anaumwa. Mara nyingi ndugu wengi hukutana kwenye misiba au kutambulishana kwa kuwa msiba humgusa kila mtu tofauti na sherehe, mtu ana hiyari ya kwenda au kutokwenda.

Unafiki wa kwenye msiba unatokea kipindi aliyefariki alipokuwa mgonjwa kwa muda mrefu, ndugu wa karibu walihitaji zaidi msaada wa ndugu na marafiki ili kunusuru maisha ya ndugu yao, lakini watu hawakushtuka wala kujigusa.

Unakuta ndugu wa karibu walihangaika kuomba fedha za huduma, matibabu ama dawa lakini wengi huwa hawajitoi kwa namna moja ama nyingine. Familia na baadhi ya ndugu ndio hubeba jukumu hilo la kuhakikisha mgonjwa anapata nafuu.

Suala la kujitoa katika matatizo hususan ya ugonjwa ni jambo jema na la kutia faraja. Mgonjwa anapotembelewa na rafiki, ndugu na jamaa hufarijika. Mgonjwa hupata tumaini jipya la maisha hata kama hali yake ikiwa mbaya. Pia, watu wanaomtembelea mgonjwa mara kwa mara akiwa hospitali ikitokea amefariki dunia hujaribu kuvuta picha ya jinsi walivyokuwa wakizungumza naye na kucheka, hivyo huwa na uchungu zaidi ya wale ambao hawajawahi kuonana nao miaka mingi.

Watu ambao walikuwa ‘bize’ na shughuli zao wanaposikia habari ya msiba wa ndugu aliyeugua utawasikia wakisema “mimi nitagharamia kununua jeneza”; mwingine atasema “mimi nitatoa usafiri” na mwingine “mimi nitagharamia picha.” Yamkini mgonjwa alikosa fedha kidogo tu kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji watu hao walishindwa kujitoa, lakini waliposikia habari za kifo wametoa mamilioni ya fedha.

Kwa nini fedha zote hizo zisingetolewa mwanzo ili kunusuru maisha ya mpendwa wao?

Wengine utawasikia wakidai “tulijuana na marehemu siku nyingi, alikuwa mtu wa watu”.

Kama kweli alikuwa mtu wa watu ulikuwa wapi au ulimsaidiaje uliposikia taarifa ya ugonjwa wake?

Unafiki ni kitu kibaya sana katika jamii yetu. Tunapaswa tuwe na upendo wa dhati kwa kusaidiana katika shida na raha. Tusiwe na urafiki wa kusaidiana katika msiba.

Jambo lingine linalosikitisha katika msiba ni kwamba, wengi huwa karibu sana na familia iliyofiwa, lakini wakishamaliza kuzika hautawaona tena wakirudi kuja kuiangalia familia hiyo, yaani inakuwa kama aliyefariki dunia aliwaambia “mkishanizika msigeuke nyuma.” Tuache unafiki, kama tumeamua kusaidia basi tujitoe kwa moyo, tusijitoe kwa kujikweza.