Tanzania ni nchi yenye mfumo unaoruhusu ushindani katika mambo mengi yakiwamo ya ulinzi kwa nia ya kuleta unafuu kwa wananchi na jamii kwa ujumla.

Kwa mfano, upo mfumo wa vyama vingi ambao lengo lake ni ushindani wa vyama kutangaza sera zao ili kuonyesha ubora katika masuala ya demokrasia na utawala bora.

Hali kadhalika upo ushindani katika biashara mbalimbali na ndiyo maana zingine zinasimamiwa na bodi maalumu za kuratibu ushindani huo.

Pia upo ushindani katika kazi za kutoa huduma kwa jamii zikiwamo za afya, elimu na hata ulinzi wa mali za watu mbalimbali.

Kumekuwapo na mwelekeo wa kutaka sekta binafsi ipambane kivyake, kana kwamba haihitaji mkono wa Serikali katika kuifanya isimame.

Na hapa ndipo napoitazama sekta ya anga, ujenzi na kuona kuwa taasisi za umma zinashikwa zaidi mkono na kuwaacha wawekezaji binafsi wanasuasua. hali hii ikiendelea hivi hapana shaka hata mapato ya Serikali yatokanayo na kodi yatapungua na uchumi unaweza kuyumba.

Katika kutekeleza vizuri fursa ya ushindani kwenye sekta ya ulinzi, Serikali iliruhusu kuanzishwa kwa kampuni binafsi zinazosimamia ulinzi wa mali za umma, kampuni binafsi na hata maduka, nyumba za kuishi, hoteli na mashamba.

Fursa ya kuruhusu kampuni nyingi za ulinzi ilitoa mwanya pia kwa Jeshi la Kujenga Taifa kuanzisha kampuni ya Suma JKT ambayo pamoja na mambo mengine inafanya kazi katika sekta mbalimbali ikiwamo ya ulinzi.

Usajili wa Suma JKT ulifuata sheria kama kampuni zingine za ulinzi zikiwamo za New Imara Security, Vigillant Security, Meridian Security, Retired Army Security, Pentagon Security, Kemacha Security, Ilonjesi Security na nyingine nyingi.

Hivyo usajili wa Suma JKT ni sawa kabisa na usajili wa kampuni zingine.

Masharti ya kusajili kampuni za ulinzi yapo mengi yakiwamo kusajiliwa Brela, kuajiri askari, kuwa na leseni ya halmashauri, kulipa kodi TRA na pia kuhakikisha walinzi wanalipiwa mafao kwenye mifuko mbalimbali na kulipa kodi ya huduma, askari wote wanakuwa na sare pamoja na uhusiano wa karibu na Jeshi la Polisi.

Kampuni nyingi za ulinzi zimetimiza masharti ya usajili na katika kutafuta kazi za malindo kila kampuni inahangaika kwa kujieleza mbele ya wahitaji huduma huku bei ya ushindani ikiongoza.

Kwa mfano zipo kampuni zinazokubali kupata hata malindo yanayotoa Sh150,000 kwa askari mmoja. Hii maana yake ni kwamba mlinzi atalipwa Sh100,000 na Sh50,000 ni za uendeshaji wa kampuni.

Pia zipo kampuni zinazokubali malindo ya Sh200,000 hadi 500,000 huku zingine zikitaka ya Sh800,000 na kuendelea hadi zaidi ya Sh1 milioni.

Ieleweke kwamba kampuni binafsi za ulinzi kwa miaka mingi zilikuwa zikipata malindo katika mashirika mbalimbali ya umma yakiwamo ya Bandari, Posta, TTCL, TRA na hata majengo ya iliyokuwa mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF, PPF na LAPF.

Kwa miaka mingi Suma JKT imekuwa ikishindana na kampuni hizo zote kutafuta masoko, lakini kwa sasa imekuwa tishio baada ya kuchukua malindo mengi ya umma kwa madai ya kuwapo maelekezo.

Kimsingi ni sawa kwa Serikali kuiangalia Suma JKT kuipa kazi, lakini ikumbukwe kwamba kampuni zingine nazo zipo kisheria. Hali kadhalika Suma nayo ni miongoni mwa kampuni ambazo bei za ulinzi zipo juu ukilinganisha na kampuni nyingi, hivyo maelekezo hayo iwapo ni kweli yanaweza kuumiza baadhi ya mashirika ya umma.

Serikali ikumbuke pia kwamba kampuni binafsi za ulinzi zimefanya kazi vizuri na zinaweza kulipa kodi na michango mbalimbali ya maendeleo ya ulinzi nchini.

Kampuni hizo zinafanya kazi kwa uaminifu na kusaidiana na polisi katika kulinda usalama wa raia na mali.

Hivyo ipo haja ya kuruhusu ushindani wa bei za ulinzi ushike hatamu badala ya kuagiza malindo ya taasisi za umma yote yachukuliwe na kampuni moja pekee ili ajira za walinzi ziendelee kudumu kwa wote.

Lakini kama wapo viongozi wa taasisi za umma ambazo zilikubali kuzilipa kampuni za ulinzi fedha nyingi kuliko uhalisia, Serikali haina budi kuwachukulia hatua za kinidhamu wahusika badala ya kuzuia kampuni binafsi kufanya kazi nazo.

Mwandishi ni mdau wa maendeleo, anapatikana kwa simu namba 0767-338897