In Summary
  • Kila mahali katika nchi nzima, athari za mvua hizo zinaonyesha makali yake. Hakuna mahali paliposalimika, iwe ni barabara, madaraja, makazi, mashamba na hata mazao kuna mahali yameathiriwa.

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimeanika namna miundombinu yetu ilivyo, zikionyesha ni kwa namna gani kama Taifa bado tuna safari ndefu kufikia mafanikio ya juu ya kuwa na miundombinu madhubuti katika maeneo mengi nchini.

Kila mahali katika nchi nzima, athari za mvua hizo zinaonyesha makali yake. Hakuna mahali paliposalimika, iwe ni barabara, madaraja, makazi, mashamba na hata mazao kuna mahali yameathiriwa.

Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa athari za mvua hizi zimeonekana kwenye maeneo ambayo ni kama yamesahaulika ambako wananchi wanasumbuka na miundombinu iliyopo. Ndiyo maana tangu zilipoanza kunyesha, mitandaoni imekuwa ni jambo la kawaida kuona ama wananchi wanavuka mto kwa kutumia vyombo duni vya kuwavusha au watoto wadogo wanavushwa mito kwa msaada wa wasamaria wema.

Yote haya yanatokana na hali halisi ya miundombinu ama kutokuwapo katika maeneo wanayoishi au kuharibiwa na mvua. Mathalan, mwishoni mwa wiki iliyopita gazeti hili lilikuwa na picha iliyoonyesha watoto wadogo wakivushwa mto eneo la Mbande mpakani mwa wilaya za Temeke na Mkuranga kwa kutumia mbao zilizounganishwa kiujanjaujanja na msamaria mwema ili waweze kwenda shuleni.

Lakini pia takriban mwezi mmoja uliopita, gazeti hili lilikuwa na picha katika ukurasa wa kwanza iliyoonyesha wanafunzi katika kijiji kimoja wilayani Kisarawe wakivushwa mto ili waende shuleni. Hawa walikuwa wakivushwa kwa kutumia magogo.

Siyo wanafunzi tu wanaoteswa na tatizo hili, lakini pia hata watu wazima. Vilevile tatizo hili halipo vijijini tu, bali hata mjini, mfano ukiwa ni ule wa wakazi wa Kivule wilayani Ilala wanaolazimika kupanga foleni ili waweze kuvuka mto baada ya daraja walilolitarajia muda mrefu kutokamilika hadi sasa.

Jana, mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga wilayani Mkuranga, Amiri Mbamba aliagiza wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaolazimika kuvuka Mto Kizinga kutokwenda shule baada ya mto huo kujaa maji.

Mbamba alitoa tangazo hilo juzi jioni kwa kupita katika nyumba za eneo hilo na kuwasihi wazazi wasiwaruhusu watoto wao kutoka majumbani kwa ajili ya usalama wao. Mto Mzinga ulianza kujaa maji juzi saa tatu asubuhi, jambo lililowalazimu wavushaji eneo la Bonde la Mkoga kusitisha kazi hiyo waliyokuwa wakifanya kwa ujira wa kati ya Sh1,500 na 2,000 kwa kila mtu.

Tunajua kwamba tatizo la miundombinu inayohusisha vivuko na madaraja lipo kila kona nchini, lakini tunaamini kwamba ukubwa wa tatizo utakuwa wa aina yake vijijini ambako vyombo vingi vya habari havifiki kuonyesha hali halisi ilivyo.

Wakati katika picha pana ya nchini inadhihirisha kwamba nyakati hizi za mvua kutoka sehemu moja hadi nyingine hususan vijijini tatizo ni miundombinu, ni vyema sasa Serikali ikalitolea macho ili kuwawezesha wananchi kuunganishwa kwa urahisi katika maeneo yao.

Tunasema hivyo kwa sababu mafuriko yanapoathiri miundombinu inayowaunganisha wananchi yanakuwa na mchango mkubwa katika madhara ya jumla ya kiuchumi na kijamii, ikizingatiwa kwamba watu hawafiki kwa wakati katika sehemu zao za uzalishaji na pia zile zinazotoa huduma za jamii kama hospitali na shule.

Ni vyema Serikali kupitia vyombo vyake ifanye tathmini nchi nzima ili kuyabaini maeneo muhimu na makubwa ambayo huathiriwa na mvua, na hivyo kuathiri maisha ya watu wengi kwa wakati mmoja. Vinginevyo hali hii ya watoto kuwategemea wasamaria wema nyakati za mvua ili kufika shuleni, haitakwisha.