In Summary

Aidha, mtuhumiwa kutoonekana ana hatia ni haki ya msingi ya kisheria katika mashtaka ya jinai na inatambuliwa hivyo na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu chini ya Ibara ya 11.

Kesi zote zinazohusu makosa ya jinai inafahamika wazi kuwa mtuhumiwa anafikiriwa kuwa hana hatia hadi pale itakapothibitishwa pasi na shaka mahakamani.

Aidha, mtuhumiwa kutoonekana ana hatia ni haki ya msingi ya kisheria katika mashtaka ya jinai na inatambuliwa hivyo na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu chini ya Ibara ya 11.

Duniani kote wasimamizi wa sheria; polisi, wanasheria na watumishi wa mahakama kwa maana ya mahakimu na majaji wanajua hivyo.

Wajibu wa kisheria walionao polisi ni kuwakamata wale wote wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu kama vile wizi, uporaji, ulanguzi, ubakaji, biashara haramu ya dawa za kulevya na makosa mengine ya kijinai na wakishafanya kazi ya kuwakamata watuhumiwa, huandikisha maelezo ya matukio ya uhalifu wanaodaiwa kuutenda na kisha huwapeleka mahakamani.

Mahakama ndicho chombo pekee chenye mamlaka ya kumtia hatiani mtuhumiwa baada ya kusikiliza maelezo ya waendesha mashtaka na mashahidi wao kwa upande mmoja na utetezi wa mtuhumiwa na mashahidi wao kwa upande wa pili.

Huo ndiyo utaratibu wa kisheria, lakini katika siku za hivi karibuni baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa wamekuwa wakionekana kuchukua hatua zinazoonekana kwenda kinyume na utaratibu huo. Wameshuhudiwa baada ya kuwakamata watuhumiwa wakiwaita waandishi wa habari na kuwatangaza kuwa ni wahalifu.

Makamanda hao siyo tu huwatangaza watuhumiwa kuwa ni wahalifu, bali pia huwahoji hadharani kuhusu uhalifu wao, huku wakijua hawawezi kuwapa nafasi ya kujitetea kupinga tuhuma au kukubaliana na maelezo.

Wataalamu wa masuala ya kisheria wanasema hatua ya kuwahoji hadharani kwa kuuliza maswali yanayolenga kutaka wakiri kuwa ni wahalifu au wavunja sheria ni kama vile wanaendesha kesi wakati wajibu huo ni wa Mahakama.

Tunaamini, kwa sheria zilizopo, hawatakiwi kumuuliza mtuhumiwa kama amefanya kosa au hajafanya. Hilo liachwe lifanyike mahakamani na ndiyo maana mtuhumiwa akifikishwa kortini siku ya kwanza hakimu anamuuliza: “Unakiri au unakataa?”

Tunatambua uzito wa kazi ya maofisa wa polisi na tunaiheshimu maana bila uwepo wao, uhalifu ungekuwa wa kutisha na kusingekalika mitaani. Lakini tunapenda kuwakumbusha makamanda wote kwamba ugumu wa kazi yao usiwafanye wachukue hatua ambazo zinaibuka utata wa kisheria.

Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, pamoja na mambo mengine inatamka: “Ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa ana hatia ya kutenda kosa hilo.”

Kazi hiyo lazima ifanywe kwa weledi tena kwa kuzingatia utu na heshima ya watu. Wakati ni kweli kuna baadhi ya watu hukamatwa, hushtakiwa, hufungwa kwa uhalifu walioufanya na wakimaliza kifungo bado hurudia makosa, wapo wengi husingiziwa kufanya uhalifu au kutokana na kukosewa kwa utambulisho.

Watu waliokamatwa kwa kukosewa utambulisho wakitangazwa kuwa ni wahalifu wakati si kweli huwa wamevunjiwa heshima na wakiachiwa huru kutokana na kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiani, huwachukua muda mrefu kujenga upya haiba zao.