In Summary
  • Vidonda kwenye kona za midomo ni ile hali ya kuwa na malengelenge katika midomo ambayo hupasuka katika nyakati tofauti tofauti na hata kutoa damu ama maumivu. Inaelezwa na wataalamu wa afya kuwa hali hii inapoanza kutokea huweka utandu wa alama nyeupe zisizouma katika kona za midomo, kitaalamu Perleche au Angular stomatitis.

Vidonda pembeni ya mdomo vyaweza kusababishwa na vitu vingi. Ili kujua nini chanzo chake, mwandishi wa makala haya anadadavua kwa undani.

Vidonda kwenye kona za midomo ni ile hali ya kuwa na malengelenge katika midomo ambayo hupasuka katika nyakati tofauti tofauti na hata kutoa damu ama maumivu. Inaelezwa na wataalamu wa afya kuwa hali hii inapoanza kutokea huweka utandu wa alama nyeupe zisizouma katika kona za midomo, kitaalamu Perleche au Angular stomatitis.

Unaweza kupata tatizo hili katika upande mmoja wa mdomo au zote mdomo katika wakati mmoja au tofauti.

Alama na dalili

Muathirika anaweza kuanza kutokwa na damu upande mmoja wa mdomo, au mwingine hutokewa na malengelenge kwenye kona za midomo.

Dalili nyingine ni kupasuka midomo, kuwashwa kwenye kona za midomo, maumivu kwenye kona hizo, hali ya wekundu au weupe kwenye kona za midomo na kuvimba kwa kona hizo.

Chanzo cha ugonjwa

Tatizo hilo mara nyingi husababishwa na muunganiko wa vitu kadhaa ambavyo kwa pamoja husababisha kuwapo kwa unyevunyevu wa muda mrefu kwenye maeneo ya kona za midomo pamoja na maambukizi ya bakteria au fangasi.

Kwa mfano ingawa vidudu vya fangasi huwa vipo tu na havina madhara yoyote kinywani, lakini fangasi hao wanaminika kuchangia kutokea kwa ugonjwa.

Hii inatokana na ukweli kwamba miongoni mwa waathirika wa ugonjwa wa vidonda kwenye kona za midomo ni fangasi wengi,

Kwa watu waliopona ama kupata nafuu, fangasi huwa kwa kiwango kidogo. Halikadhalika, baadhi ya bakteria wa makundi tofauti huwa wapo.

Hivyo ni sahihi kusema kuwa mchanganyiko wa bakteria na fangasi unapopata mazingira ya unyevunyevu usiokwisha husababisha ugonjwa huu, ukiacha sababu nyingine.

Sababu hatarishi

Lakini pia inaelezwa zipo sababu hatarishi zinazosababisha mtu kuugua vidondo hivyo.

Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na tabia ya kujilamba midomo, kinywa kutokua na mate, mpangilio mbaya wa meno, upungufu wa virutubisho mwilini na maradhi ya kinasaba kama ya Down syndrome

Sababu nyingine ni kama mtu ana ugua maradhi ya saratani yaliyo katika hatua ya mwisho, matumizi ya meno ya bandia yanayoumiza sehemu za ndani za kinywa, matumizi ya dawa zinazopunguza kinga ya mwili, kisukari na uvaaji wa vifaa maalumu vya kurekebisha mpangilio mbaya wa meno.

Uhusiano wa vidonda na maradhi mengine mwilini

Watu wanapaswa kutambua kuwa ugonjwa huu unaweza kuwa dalili ya maradhi mengine mwilini.

Maradhi hayo ni kama ya upungufu wa vitamini B, upungufu wa madini ya chuma na zinki, uwapo wa maradhi yanayoshambulia mfumo wa kinga ya mwili kama vile kisukari au maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) na upungufu wa damu.

Changamoto za ugonjwa huo

Kila maradhi yaingiapo mwilini huwa na changamoto zake pindi mtu anapoonza kuugua.

Miongoni ni mtu kuanza kuhisi midomo yake inkuwa mikavu au anapata maumivu mdomo kama ya kuungua au anahisi ladha mbaya kinywani.

Na wakati mwingine humfanya mgonjwa ale chakula kwa shida. Hali hiyo ikiendelea kwa muda humfanya mtu kukosa lishe na kupungua uzito.

Matibabu

Matibabu ya ugonjwa huo hukumbana na mambo mengi ikiwamo usugu na uwezekano wa kujirudia baada ya muda fulani.

Hiyo ni kwasababu ugonjwa huo ni matokeo ya vitu kadhaa vinavyoweza kuukumba mwili wa mtu.

Hata hivyo, tunaelezwa kuwa matibabu ya ugonjwa huu kama yalivyo maradhi mengine, hulenga kuondoa kisababishi cha ugonjwa.

Unaweza kuutibu baada ya uchunguzi wa kimaabara ambao utaonyesha kuwa bakteria au fangasi ndiyo sababu.

Hivyo, dawa za kupambana na vijidudu hivyo huweza kuwa suluhisho au kama hali hiyo imesababishwa na upungufu wa madini, au damu, mgonjwa anaweza kupatiwa damu husika na kwa kiwango kinachostahili hivyo kuweza kuutibu.

Lakini pia kama vitakuwa vimesababishwa ba maradhi mengineyo yakiwamo kisukari, utatakiwa kudhibiti maradhi hayo ili kusaidia kuondoa tatizo.

Lakini pia kama hali hiyo imekupata baada ya kuanza kutumia vifaa maalumu vya kurekebisha mpangilio mbaya wa meno au meno ya bandia yanakuumiza, rudi tena kwa daktari wako ili arekebishe hali hiyo ambayo itasaidia kukuondolea tatizo la vidonda hivyo vya pembeni yam domo.

Dk Ezekiel Onesmo anapatikana kwa simu namba 0683-694771