In Summary
  • Ubingwa wa Simba ulikuja baada ya watani wao, Yanga kupoteza mechi yao ya ugenini dhidi ya Prisons Mbeya.

Klabu ya Simba imemaliza ukame wa mataji ya Ligi Kuu Bara baada ya Alhamisi iliyopita kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa ligi hiyo.

Ubingwa wa Simba ulikuja baada ya watani wao, Yanga kupoteza mechi yao ya ugenini dhidi ya Prisons Mbeya.

Mabingwa hao wa Tanzania waliokuwa watetezi wa taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo, walipoteza jijini Mbeya kwa kufungwa mabao 2-0.

Kipigo hicho hakikutarajiwa na ndicho kilichotoa nafasi kwa Simba kubeba ubingwa wao wa 19 kwani hakuna timu nyingine ambayo ingefikia pointi za Simba iliyokuwa na pointi 65. Simba kwa sasa ina pointi 68 baada ya juzi kuilaza Singida United bao 1-0 kwenye Uwanja wa Namfua.

Matokeo ya juzi dhidi ya Singida ni mwendelezo wa faraja kubwa na jambo lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu na wadau wa Simba kwani mara ya mwisho timu yao kubeba ubingwa wa Bara ilikuwa msimu wa 2011-2012, hii ikiwa na maana huu ni mwao wa sita kwao.

Ushindi huo umeleta heshima kubwa kwa makocha walioiongoza timu hiyo katika mbio hizo za ubingwa na kufanikiwa kulibeba taji kabla ligi haijamalizika, kuanzia kwa Joseph Omog aliyeiongoza kwa duru la kwanza na Masudi Djuma na baadaye Mfaransa Pierre Lechantre waliomalizia safari iliyoanzwa na Mcameroon aliyefurushwa mwaka jana.

Tunaipongeza Simba kwa mafanikio iliyopata msimu huu kwani pamoja na kwamba imebakiza mechi mbili, lakini hadi sasa haijapoteza hata mchezo mmoja.

Pamoja na hayo yote, tunaamini mafanikio hayo yamekuja Msimbazi kutokana umoja na mshikamano wa wachezaji, wanachama na viongozi wao kwa jumla.

Lakini pia, kujituma kwa wachezaji na maandalizi mazuri yaliyofanywa na viongozi wao sambamba na kazi kubwa iliyofanywa na makocha katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Hata hivyo, tunaikumbusha Simba kuwa wasijisahau sana kwa kushangilia ubingwa mfululizo na kuacha kufanya mambo ya msingi.

Kutwaa ubingwa ni kama wamefungua mambo mengine makubwa ambayo yanatakiwa kutekelezwa kabla ya kuanza michuano hiyo baadaye Desemba.

Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho yataanza Desemba hadi Mei mwakani kwani Shirikisho la Soka Afrika (CAF), linaanzisha utaratibu wa mechi zake kuanza Septemba hadi Mei ya mwaka mwingine.

Hapa tuna mawili, kwanza; inatakiwa wachezaji waone fahari kucheza huku bendera ya Tanzania inapepea, na inatakiwa kujituma kuhakikisha timu zinapata ushindi ndani na nje.

Ushindi pekee na kujituma ndiko kutakakoipa heshima zaidi katika mashindano ya kimataifa.

La pili; Wachezaji wafahamu kuwa hiyo ni nafasi ya kujitangaza kimataifa.

Itakumbukwa Mbwana Samatta aliwatungua TP Mazembe akiwa Simba mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kiasi cha kuamua kumsajili.

Wachezaji wanatakiwa kuacha visingizio kwa kuwa haya ni maisha yao ya soka, na wanaweza kupata ulaji wakifika mbali Afrika.

Hatudhani kama ni jambo la kupendeza kama kuendelea kushangilia na hata ligi ikiisha kabisa kutumia muda mwingi kushangilia ubingwa badala ya kutengeneza kikosi matata cha Ligi ya Mabingwa .