In Summary
  • Hata hivyo, Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache ambayo yana amani na utulivu, licha ya kuwapo kasoro ndogondogo zinazorekebishika.

Mataifa kadhaa barani Afrika bado yako katika misukosuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, vita vya kikabila na vita vya kugombea rasilimali na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Hata hivyo, Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache ambayo yana amani na utulivu, licha ya kuwapo kasoro ndogondogo zinazorekebishika.

Hali hii haijaja kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na misingi imara iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili; Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na mwasisi wa Zanzibar, Abeid Karume. Misingi iliyoachwa na waasisi hawa bado inaishi na inaendelea kujenga jina zuri la Tanzania nje ya mipaka ya nchi.

Kuna faida nyingi zinazopatikana kutokana na Taifa kuwa imara katika masuala ya amani.

Nchi inapokuwa na utulivu, mbali na uchumi wake kustawi, pia hufungua fursa muhimu za uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia ambao huleta ushirikiano baina ya nchi na mataifa mengine.

Faida zitokanazo, ikiwamo heshima kwa nchi yetu hujitokeza kwa namna nyingi na kuifanya nchi ionekane ya maana miongoni mwa nyingine duniani.

Mathalan, kutokana na hali hiyo Watanzania wengi wamewahi kuteuliwa kushika nafasi zenye hadhi kubwa kimataifa kama katibu mkuu wa OAU, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Makazi Duniani (UN-Habitat), mkuu wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika na nyinginezo nyingi.

Hata ushindi wa Jaji Imani Aboud katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu (AfCHPR) alioupata mwezi jana, mbali na weledi na ujuzi binafsi, kwa upande mwingine ni ishara ya heshima iliyonayo nchi yetu katika sura ya kimataifa.

Majaji kutoka nchi kadhaa walijitokeza kugombea nafasi hiyo, lakini ni Jaji Aboud alichaguliwa kwa kupata kura 47 kati ya 55 zilizopigwa na wasomi wenzake. Kura hizi zilipigwa katika mkutano wa 33 wa baraza la mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Afrika jijini Nouakchott nchini Mauritania.

Kutokana na uchaguzi huo, Jaji Aboud anachukua nafasi ya Jaji Solomy Bossa wa Uganda aliyejiuzulu, baada ya kuchaguliwa kuwa jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Katika uchaguzi huo, pia majaji wengine wanne wa mahakama hiyo walichaguliwa ambao ni Jaji Koko Ben (Kenya), Jaji Tchikaye Balise (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Jaji Anukam Stella kutoka Nigeria.

Jaji Aboud ambaye alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga atawakilisha Kanda ya Afrika ya Mashariki kwa miaka miwili katika mahakama hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa Mtanzania kuchaguliwa katika mahakama hiyo Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006 jijini Addis Ababa, Ethiopia na baadaye kuhamishiwa Arusha.

Jaji mwingine ambaye aliyewahi kuchaguliwa ni Jaji mkuu mstaafu Augustino Ramadhani, mmoja wa majaji wanaoheshimika katika ukanda wa Afrika na nje ya Afrika.

Ushindi huu pia ni Kazi nzuri ambayo inafanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga na wasaidizi kuendelea kuitangaza vyema Tanzania nje ya mipaka.

Kutambuliwa kwa majaji wa Tanzania kwenye vyombo vya haki za binadamu ni angalizo kwa nchi kuwa inapaswa kuendelea kuheshimu haki za binadamu na watu katika maamuzi mbalimbali na pia katika kutunga sheria mbalimbali za nchi.

Pia tunapaswa kutupia jicho katika masuala mbalimbali ya ukandamizaji demokrasia, haki na usawa wa watu ili kudhihirisha kile ambacho mataifa ya nje yanakiona kwetu kuwa hatuna madoa makubwa kama zilivyo nchi nyingine.