Tanzania imepoteza dhahabu, mwamba na nguzo. Buriani Reginald Mengi, kimsingi wewe ulikuwa ni nguzo iliyosimama imara na vyema katika kila sekta. Tangu Mengi alipofariki dunia Mei 2 huko nchi za Falme za Kiarabu, jijini Dubai, kila mmoja ameyakumbuka aliyofanya wakati wa uhai wake.

Kwa mazuri aliyoyafanya Mengi, kama waandishi wangeweza kuyakusanya na kuyachapisha basi huenda kila gazeti lingejaza kurasa zake zote.

Pamoja na kuacha alama zisizofutika katika maisha ya watu, kuna kitu cha muhimu na kinachodumu zaidi ambacho tajiri huyu ametuachia.

Nacho ni kitabu chake cha; ‘I can, I must, I will’ kwa lugha ya Kiswahili: ‘‘Ninaweza, Lazima nifanye, Nitafanikisha’ Ilikuwa ni Julai 2, 2018 wakati Mengi alipozindua kitabu chenye historia ya maisha yake na safari yake ya kimaendeleo.

Nimekisoma kitabu chake mara tu baada ya kuzinduliwa Julai mwaka jana. Jambo la kwanza ni kichwa cha habari cha kitabu hicho ambacho mara moja kinakupa mwongozo na matumaini, ‘Ninaweza, Lazima nifanye, Nitafanikisha’

Mengi mwenyewe alisema kuna maana kubwa katika jina la kitabu hicho, ambayo ni kuwa na moyo wa uthubutu, kupiga moyo konde pindi unapoianza safari na pia kusimamia yale matarajio yako hadi uyakamilishe.

Katika kitabu kile, ameonyesha namna alivyoiona ndoto yake, kupata uthubutu wa kuifanikisha ndoto hiyo na kisha kusimamia ndoto hiyo.

Mengi mara kadhaa amekuwa akisema kuwa; “Nimezaliwa katika umaskini wa kutupwa, lakini jambo hilo hata siku moja halikunikatisha tamaa.” Katika kitabu hicho, anasema alianzisha Kalamu Company Limited, wakati bado akiwa mwajiriwa wa C& L Expatriates Company.

Alikutana na vikwazo vingi, lakini kilichomfanya asirudi nyuma ni ile dhana aliyojijengea ya: “Ninaweza, Lazima nifanye, Nitafanikisha”

Baada ya kampuni ya Kalamu kuendelea vyema, aliacha kazi ya kuajiriwa na kubaki akiisimamia kampuni yake. Anaeleza kuwa inahitaji uthubutu wa hali ya juu, kuacha kazi na kusimamia biashara yako.

Madini mengine ametuachia Mengi ni pale aliposema katika kitabu chake kuwa; “Ninaamini biashara siyo kwa ajili tu ya kupata faida tu bali pia kwa ajili ya majukumu ya kijamii kama vile ujasiriamali wa kijamii.” Alitoa mfano namna alivyotembelea Kijiji cha Mbokomu Korini. Kilikuwa na kikundi cha wanawake waliokuwa na miradi yao binafsi ya kiuchumi kwa ajili ya kujiendeleza.

Alipotembelea kikundi hiki aliwasaidia katika mradi wao wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Msaada huo ulitolewa kwa kuwanunulia ng’ombe wa maziwa, vifaa pamoja na gharama za kujifunza ufugaji wa ng’ombe.

Anasema msaada ulikuwa ni mdogo lakini matokeo yalikuwa makubwa. Wanawake hao waliweza kujenga nyumba zao wenyewe, kusomesha watoto na kuboresha maisha yao kwa ujumla.

“Ujasiriamali wa kijamii na kusaidia miradi ya kukuza na kuiendeleza jamii ndivyo vinatambulisha maisha yake,” anasema Mengi. Kingine cha kujifunza ambacho ameandika kwenye kitabu chake ni namna alivyochagua watu wa kufanya nao kazi.

Anasema anaamini licha ya kipaji na uwezo kuwa vya muhimu katika kazi lakini uaminifu, kujituma na kujitoa ni muhimu zaidi kwake.

“Naamini uwezo mkubwa unaweza kuendelezwa/kujengwa lakini huwezi kujenga uaminifu na kujitoa sana kwa mtu,” anasema Mengi ambaye amewataja Zoeb Hassuji wa Bonite Bottlers Limited na Joyce Mhaville wa ITV na Radio One kama wakurugenzi wake bora zaidi wanaofanya vizuri na wenye sifa hizo.

Urithi mwingine aliotuachia kupitia kitabu hiki ni kutoa nafasi ya kusikia nini wengine wanasema. Anasema inamaanisha kusikiliza wateja au watu unaofanya nao kazi au wakati mwingine hata washindani wako wa kibiashara ni njia bora sana ya kufanikiwa.

Leo Mengi hayupo duniani, lakini kupitia kitabu hiki, vijana wengi zaidi wanaweza kujifunza na kuwa na uthubutu, kujiamini, upendo na ustahamilivu kama aliokuwa nao.

Kubwa kuliko yote ambalo linawafanya wengi wamlilie Mengi, ni upendo wake kwa jamii. Atakumbukwa kwa upendo wake kwa walemavu na wasiojiweza.

Pia, kwa Watanzania walio na nafasi, waandike historia zao kitaaluma au za maisha ili kuwahamasisha wengine.

Tuendelee kuzienzi moja ya kauli zake za mwisho aliposema: “ Naomba nichukue fursa hii kuwaomba Watanzania wenzangu kuufanya mwaka 2019 kuwa mwaka wa maridhiano na kusameheana. Chuki ni mzigo mzito mno kuubeba mioyoni mwetu, njia pekee ya kusonga mbele ni kusameheana na kudumisha upendo.”

Mwandishi wa uchambuzi huu ni mfanyakazi wa Tamwa