In Summary
  • Jumuiya hiyo ilikutana ikiwa ni takriban miezi kadhaa tangu Serikali ilipoandaa na kuja na mpango huo kwa kukusanya maoni ya wafanyabiashara kutoka kwenye jumuiya tofauti ili kuboresha mazingira ya uanzishaji, usimamizi na uendelezaji wa biashara.

Juzi, jumuiya ya wafanyabiashara nchini ilipendekeza mambo 10 yatakayosaidia utekelezaji wa mpango wa uboreshaji mazingira ya uwekezaji nchini.

Jumuiya hiyo ilikutana ikiwa ni takriban miezi kadhaa tangu Serikali ilipoandaa na kuja na mpango huo kwa kukusanya maoni ya wafanyabiashara kutoka kwenye jumuiya tofauti ili kuboresha mazingira ya uanzishaji, usimamizi na uendelezaji wa biashara.

Serikali ilifanya hivyo kutokana na malalamiko yaliyokuwapo pamoja na ripoti ya urahisi wa ufanyaji biashara inayotolewa na Benki ya Dunia (WB), kila mwaka iliyoonyesha Tanzania inashuka kwenye msimamo huo. Katika mkutano wa juzi, wafanyabiashara kupitia jumuiya yao walipendekeza kuwapo kwa nidhamu ya utekelezaji kwa watakaopewa dhamana ya kuboresha mazingira ya uanzishaji, usimamizi na uendelezaji wa biashara.

Pia, walipendekeza uandaliwe mpango kazi na kuweka vipaumbele katika mabadiliko yatakayofanywa, kufanya tathmini ya mabadiliko ya sera, uendelevu wa utekelezaji wa maazimio yatakayopitishwa na kuwapo kwa mfumo wa kisheria wa kusimamia mabadiliko yatakayofanyika.

Vilevile, wadau hao walipendekeza kuwapo kwa kikosi kazi kitakachojumuisha sekta binafsi na ya umma, kanuni zinazotekelezeka na kuzingatia maoni ya mwongozo huo kwenye bajeti ya Serikali.

Kutokana na maoni ya wadau yaliyomo kwenye mwongozo huo ambao uliwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri mwishoni mwa Mei, Serikali inatarajia kuondoa matakwa yanayojirudia baina ya mamlaka za usimamizi na sera zinazokinzana. Hili ni jambo mojawapo ambalo lilikuwa likilalamikiwa mara kwa mara na wafanyabiashara.

Kimsingi, utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji nchini umekuja katika kipindi muafaka baada ya changamoto na malalamiko kutoka kwa wadau ambao ni wafanyabiashara, kukithiri. Mathalan, yamekuwapo malalamiko mengi juu ya kubambikiwa kodi kubwa na mamlaka zinazohusika, ukaguzi katika maeneo ya biashara zao kufanywa na mamlaka zaidi ya moja, ulipaji wa tozo na ushuru katika taasisi tofauti ili wapatiwe vibali vya uendeshaji shughuli zao badala ya kufanyika sehemu moja, na pia kuwapo kwa kero katika ufuatiliaji wa vibali na leseni katika taasisi tofauti.

Kwa ujumla, pamoja na mfumo huu kuwakera wafanyabiashara wengi, lakini mamlaka zinazohusika na hasa Serikali ilikuwa kimya kwa muda mrefu wakati vilio vya wadau hawa muhimu vikisikika.

Kama wasemavyo wahenga hakuna marefu yasiyo na ncha. Ndivyo ilivyo pia kwa wadau hawa ambao hatimaye kilio chao kimesikika na kufanyiwa kazi, na sasa wanasubiri neema ili mpango husika uanze.

Hata hivyo, licha ya matumaini makubwa waliyonayo, bado kuna suala la utekelezaji wa mwongozi huo ambapo tunashauri uwepo mfumo jumuishi baina yao na Serikali. Tunasema hivi kwa sababu imekuwapo mipango na sera nyingi za Serikali ambazo zilishindwa kutekelezeka kutokana na kutokuwapo kwa mfumo jumuishi baina yake na wadau husika, na hivyo mafanikio yaliyotarajiwa kutofikiwa.

Kwa hili tunaiomba Serikali, kama wanavyosema wadau hawa, uwepo mfumo utakaozifanya pande hizi mbili kushirikiana kwa karibu, kwa kuhakikisha kuwa kila kilichokubalika kinatekelezwa na upande husika, kwa wakati na kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

Ni vyema sasa malalamiko ya mara kwa mara yanayotolewa na wadau wa sekta hii na zingine tofauti yakasikilizwa na kutengenezewa miongozo ya utekelezaji ili kupata matokeo chanya na endelevu.

Ukitekelezwa kwa ufanisi, mpango huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na kimataifa.