Februari 19, Waziri wa Uwekezaji, Angellah Kairuki alisema Serikali inakusudia kuanzisha vituo vya pamoja katika mikoa na wilaya zote hapa nchini ili kuvutia uwekezaji.

Kairuki alisema hayo alipokutana na wajumbe wa bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ambapo alisema katika kufanikisha hilo wanafikiria kutumia ofisi za posta kama ambavyo inafanyika katika nchi jirani ya Kenya.

Alisema utaratibu wa vituo hivyo utakuwa sawa na wa Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), kwani vitasaidia katika utoaji wa vibali mbalimbali kwa wawekezaji zikiwamo leseni na ithibati.

Wazo hilo ni zuri hasa kwa kuzingatia kuwa hivi sasa azma ya Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaojengwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Lakini pia uwekezaji ukishamiri katika maeneo mbalimbali nchini, utapunguza changamoto za kiuchumi miongoni mwa watu na kurahisisha upatikanaji wa ajira.

Sio siri kuwa uchumi wa viwanda tunaoupigia chapuo sasa hauwezi kujengwa na Serikali pekee bali pia ushiriki wa sekta binafsi ambayo msingi wake mkuu ni uwekezaji wa ndani na ule wa kutoka mataifa mengine. Lakini ili yote haya yawezekane kunahitajika utaratibu mzuri kama huu wa kuvutia wawekezaji.

Wafanyabiashara na wawekezaji wengi ambao ni nyenzo muhimu ya kufikia uchumi wa kati, wamekuwa wakilalamikia baadhi ya mambo ikiwamo mazingira yasiyo rafiki ya uwekezaji.

Pamoja na mambo mengine mpango huu ukifanikiwa, sio tu utawapa urahisi wawekezaj, lakini pia upatikanaji wa vibali mbalimbali na leseni ambazo ni hatua za awali ya kufanya uwekezaji.

Imekuwa ni kiu ya muda mrefu kwa wawekezaji kupata huduma sehemu moja bila kuingia gharama za kusafiri kufuata ofisi nyingine mbali kwa kuwa gharama hizo zinaweza kuathiri mtaji wa uwekezaji.

Kutokuwa na kituo cha pamoja kwa wawekezaji, kumesababisha urasimu na wakati mwingine kukwama kwa mradi fulani wa uwekezaji kwa kuwa mwekezaji anachoshwa na mlolongo mrefu.

Wawekezaji hususani wa kigeni wamekuwa wakilalamika kuwa mizunguko hiyo inawagharimu fedha nyingi. Lakini pia wamekuwa wakikaguliwa mara mbilimbili tena na mamlaka tofauti. Serikali inayotaka kukua kiuchumi haina budi kuvutia uwekezaji kwa kuweka mazingira yanayovutia na kuondoa kila kero inayowakwaza wawekezaji.

Uwepo wa kituo cha pamoja cha uwekezaji katika kila wilaya ni hatua kubwa katika kuvutia uwekezaji hapa nchini. Pia, ni mpango utakaotatua changamoto za wawekezaji kwani vituo vitaondoa urasimu ambao umekuwa ukilalamikiwa hivi sasa.

Aidha, mpango huu utaziamsha halmashauri zilizolala kiuwekezaji, kwa kuwa zitaona aibu kuwa na kituo cha pamoja na uwekezaji bila kubainisha fursa za uwekezaji zinazopatika katika eneo hilo.

Utekelezaji wa mpango huu utavutia wawekezaji zaidi kuwekeza katika maeneo yote ya nchi kwa kuzingatia fursa zilizopo, kwa kuwa baadhi ya vikwazo vitakuwa vimeondolewa.

Maeneo ambayo yalikuwa yako mbali na ofisi za TIC yalikuwa yanaogopwa na wawekezaji kwa kuzingatia kuwa kutakuwa na usumbufu wa kupata vibali mbalimbali sasa.

Nionavyo mimi mpango huu unaweza ukavutia ujenzi wa viwanda vingi zaidi kama ambavyo Serikali inatamani.Kutekelezwa kwa mpango huu ni fursa kwa Serikali kuongeza mapato ya kodi na tozo mbalimbali kutokana na kukua kwa sekta ya uwekezaji.

Pia, halmashauri zitaongeza mapato yake ya ndani kwa kuwa katika maeneo yao kutakuwa na shughuli nyingi za kiuchumi tofauti na ilivyo sasa.

Kadhalika wananchi wataweza kupata ajira za moja kwa moja na za muda kutokana na uwekezaji utakaokuwa umefanyika, hivyo kwa namna nyingine Serikali itakuwa imepunguza tatizo la ajira kwa wananchi wake.

Aidha, kukuwa kwa uwekezaji huenda sambamba na kuongezeka kwa uzalishaji katika nchini hivyo pato la nchi litaongezeka na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi utaongezeka hali itakayoimarisha thamani ya shilingi yetu.

Kuimarika kwa shilingi kutarahisisha ununuzi wa bidhaa kutoka nje ya nchi kwa kuwa kiwango cha kubadilishia dola kwa shilingi kitapungua. Lakini pia bidhaa nyingi zitapatikana hapa nchini kwa bei pungufu tofauti na sasa ambapo zinatoka nje ya nchi.

Nafikiri Serikali itauchukulia kwa uzito wake na pengine kuharakisha utekelezaji wa mpango huu, ili wananchi waanze kunufaika. Na sio wananchi pekee mwishowe ni Taifa letu kukua kiuchumi. Ephraim Bahemu ni mwandishi wa masuala ya biashara wa Mwananchi anayepatikana kwa simu simu namba 0756-939401