In Summary
  • Denise anajadili “magazeti ya karatasi” yanayochapishwa viwandani, akisema yamejaa taarifa za mitandao ya intaneti.

Wiki tatu zilizopita, Denice Simba Stephano, aliyejitambulisha kuwa mmoja wa wasomaji wa magazeti yanayochapishwa na Mwananchi Communications Limited (MCL), aliandika kwenye mtandao wake wa Facebook: “Tatizo la magazeti (siku hizi) ni kwamba mengi hutoa muhutasari tu wa mambo ambayo tayari umesoma katika mitandao ya kijamii; tena ya siku iliyopita…hakuna kipya na unashindwa kuyanukuu kwa marejeo maalumu katika kazi za kisomi….” Alisisitiza kwamba magazeti ni masikini wa taarifa na habari za uchunguzi.

Denise anajadili “magazeti ya karatasi” yanayochapishwa viwandani, akisema yamejaa taarifa za mitandao ya intaneti.

Akiwa ametandaza nakala za gazeti la Mwananchi mbele yake, Denice anaungwa mkono na mchangiaji mmoja anayeandika kuwa, “ndiyo maana siku hizi sinunui magazeti.”

Hizi ni kauli za jumlajumla tu. Hazihitaji magazeti maalumu. Hata kuwapo kwa nakala za Mwananchi mbele ya mtoa hoja hakuonyeshi iwapo gazeti hili ni moja ya yale yanayolalamikiwa au pekee la kitaaluma la kupigia mfano.

Nilimjibu Denice.

Niliandika, “Denice usiandike kwa haraka na harakaharaka. Vitu vipya vipo; ingawa hakika umesema kweli kwamba tunahitaji taarifa na habari zilizofanyiwa uchunguzi.”

Baada ya hapo niligeukia upande wa taarifa za mitandaoni; kwamba kama ni ufupi, taarifa za mitandaoni ndizo fupi na zisizo na chembe ya uchunguzi.

Hizi niliziita taarifa za “fasta-fasta” (haraka, papohapo) zitokanazo na matukio.

Nilihitimisha kwa kuandika kuwa fasta-fasta hii tayari imemeza baadhi ya magazeti yachapishwayo viwandani ambayo hakika ni yaleyale ya mitandaoni (online).

Kama gazeti la kiwandani litakuwa limenukuu fasta-fasta ya mitandao ya Blogu, Facebook, Twitter, Instagramu na mingine; basi hata lile la mtandaoni litakuwa limejaa fasta-fasta ileile.

Kuna haja ya kuangalia upya hata ile fasta-fasta inayolalamikiwa.

Siyo kweli kwamba vipande vidogo vya taarifa kwenye twitter havina maana.

Hapana. Kwa wenye ujuzi wa kutumia mtandao huo, kinachowekwa pale ni kielekezi kwenda kwenye kazi kuu, yenye kina na hata uchunguzi ulioshiba.

Ndivyo ilivyo pia kwa baadhi ya mitandao mingine kwenye mtandao mkuu wa intaneti.

Hapa unaonjeshwa au unatekenywa; na kuelekezwa kule ambako unaweza kupata kilichoshiba.

Hivyo ndivyo wanavyoandika wenye vitu muhimu vya kusambaza; au mijadala mirefu inayoshirikisha watu wengi.

Ninafahamu blogu zenye taarifa nyingi za uchunguzi. Wanaotaka zisomwe, huandika kidogo katika twitter na kuweka kiungo ambacho ukikifuata, unakwenda moja kwa moja kwenye kazi kuu, kubwa, nzito, inayothaminika na kunukulika kwa shabaha za kitaaluma.

Kwahiyo, siyo kila kidogo kwenye mtandao ni cha hovyo na kisicho na mafao. Hapana.

Bali Denice analalamikia taarifa au “habari” fupifupi zisizo na maelezo kamili; zisizo na kina; zisizo za uchunguzi – zile za kutupatupa tu matukio na mara nyingi bila muktadha.

Anachojadili ni matokeo ya uhuru wa kuwasiliana uliokuja kwa njia ya teknolojia. Hili tulilijadili wiki mbili zilizopita. Mazingira basi, ambamo watu “wengi” wana vyombo vya kurushiana salamu, kupelekeana hoja au taarifa; na kurushiana matukio; sharti uandishi wa zamani wa habari ufe.

Kwanini? Kwa sababu, kila mwenye chombo kiwezacho kupeleka taarifa au ujumbe, ni ripota (reporter) – anaripoti. Haripoti kwa chombo cha habari – gazeti, redio, televisheni. Anaripoti kwa wenzake – mmojammoja, katika makundi na kwenye mitandao yake.

Anafikiri. Anajadiliana na wenzake. Anasambaza maoni yake na hata yale ya wenzake.

Anaripoti tukio lolote lile na kulitolea maoni yake; kama aonayo na kama ambavyo angetaka. Hapitishi taarifa zake kwa yeyote.

Ni moja kwa moja kwenye mtandao wake na ile anayoshiriki.

Huu basi ni ulimwengu wa maripota. Katika hali hii, lazima wanaojiita, wanaoitwa, wanaotambulika kwa vyeti na kazi kuwa ni maripota, watafute njia mpya ya kufanya kazi yao. Siyo kwamba kazi yao imevamiwa.

Hapana. Fursa imepatikana kwa wengi kuripoti. Kuripoti nje ya taaluma. Iwapo vinavyoripotiwa kwa mtindo huu vitafanywa kuwa taarifa na habari za magazetini – yawe ya viwandani au mitandaoni – akina Denice hawatapata cha kunukuu kwa ajili ya kukamilisha kazi zao za kisomi au kitaaluma.

Hata wasomaji wa kawaida hawatapata mnofu wa taarifa.

Huo ndio mwanzo wa mjadala kuwa “Ripota” (reporter); siyo “Mwandishi wa Habari” (journalist). Wewe unasemaje?