In Summary
  • Hata hivyo, jukumu hilo la msingi limekuwa halisimamiwi na halmashauri nyingi za miji, manispaa na majiji. Huko ndiko uchafu unakozalishwa kwa wingi na kusababisha milipuko ya magonjwa.

Jukumu kubwa la Serikali za mitaa ni kuhakikisha kwamba maeneo ya makazi ya wananchi yanakuwa safi, kwa kuweka utaratibu wa kusimamia suala la usafi au kuwajengea uwezo makandarasi ili waweze kutekeleza wajibu wao kikamilifu.

Hata hivyo, jukumu hilo la msingi limekuwa halisimamiwi na halmashauri nyingi za miji, manispaa na majiji. Huko ndiko uchafu unakozalishwa kwa wingi na kusababisha milipuko ya magonjwa.

Ni halmashauri chache ambazo zimefanikiwa katika kuweka miji yao katika hali ya usafi. Mafanikio hayo yanatokana na kuweka taratibu nzuri na kushirikiana na wadau ambao ni wananchi wenyewe pamoja na makandarasi wa uzoaji takataka.

Hivi sasa, baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ni machafu kutokana na mgomo wa makandarasi wa taka unaoendelea. Ukipita baadhi ya maeneo ya Manzese, Mabibo na Mbezi utaona mlundikano wa taka ambao unaongezeka kila siku.

Jambo hili siyo tu linaharibu sura nzuri ya jiji la Dar es Salaam, bali pia linahatarisha maisha ya wananchi kutokana na uwezekano wa mlipuko wa magonjwa kama vile kipindupindu, kuhara au homa ya matumbo.

Sote tunafahamu kwamba huu ni msimu wa matunda na matunda huvutia nzi wengi, hivyo kukiwa na uchafu ambao hauzolewi ni hatari hasa kwa watoto wadogo ambao wanacheza sehemu yoyote bila kuchukua tahadhari.

Chanzo cha tatizo hilo tunaambiwa ni mgogoro wa kimasilahi kati ya manispaa za Kinondoni na Ubungo na makandarasi wa uzoaji taka.

Manispaa hizo zimeweka utaratibu wa kukusanya mapato ya takataka zenyewe, badala ya kuwaachia makandarasi kama ilivyo maeneo mengine ya Ilala na Temeke.

Wanadai kwamba wanatumia gharama kubwa kukusanya takataka, hivyo manispaa iwaache wakusanye tozo kwa sababu hazijawawezesha chochote katika kazi hiyo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aaron Kagurumjuli anasema fedha zozote zinazokusanywa kwa umma ni fedha za Serikali, hivyo lazima Serikali yenyewe ikusanye na si makandarasi kama wanavyotaka.

Pamoja na hoja za pande zote mbili, waathirika wakubwa wa mvutano huo ni wananchi. Taka zinazidi kuzalishwa, hakuna anayezoa na hakuna anayejali. Sikukuu zimepita bado takataka zipo.

Ninashauri Serikali za mitaa (hasa manispaa za Ubungo na Kinondoni) zikae na makandarasi kutafuta namna bora ambayo itakuwa na masilahi kwa pande zote mbili bila kumwathiri mwananchi mtaani.

Ukusanyaji wa takataka ni huduma na siyo chanzo cha mapato kama ambavyo halmashauri hizo zinataka kufanya. Hata baadhi ya halmashauri nchini zinatenga bajeti zake kwa ajili ya kukusanya takataka.

Kama lengo kuu ni kuona mji unakuwa safi, kwa nini manispaa zisisimamie uendeshaji wa shughuli hiyo kwa kuwaachia makandarasi washirikiane na watendaji wa mitaa ambao ndiyo wahusika wakuu?

Kama wananchi wameridhia kutoa kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kutupa taka na taka zinatolewa kwa wakati, kwa nini manispaa zisijivunie kwa utaratibu huo ambao hauzigharimu kwa namna yoyote ile?

Suala hili linahitaji jicho la manispaa pekee kwa sababu tayari asilimia 10 ya mapato yatokanayo na ukusanyaji wa takataka yanakwenda kwenye Serikali za mitaa.

Si busara kuacha mji unakuwa mchafu, kwa sababu manispaa zinataka kuongeza mapato yake kupitia fedha zinazotolewa na wananchi kwa makandarasi, kwa ajili ya huduma ambayo kimsingi ilipaswa kutolewa bure na manispaa hizo.

Nashauri manispaa za Kinondoni na Ubungo zikae na makandarasi wake wote na kuangalia namna bora ya kulipana.

Kama halmashauri itakusanya fedha hizo, lazima wakubaliane malipo na makandarasi hao bila kutegemea makusanyo ya fedha za takataka.

Utendaji wao wa kazi pia uwajali wananchi ambao ndiyo wanahitaji zaidi huduma hiyo. Busara itumike kumaliza tofauti hizo ili takataka ambazo tayari ziko mitaani zizolewe na mji uwe safi tena kama maeneo mengine.

Wananchi pia tujenge tabia ya usafi kwa kutambua madhara ambayo tunaweza kuyapata endapo takataka zitajazana kwenye maeneo yetu. Afya ni mali, tujali afya zetu kwa kuhifadhi taka.

Peter Elias ni mwandishi wa Mwananchi, anapatikana kwa simu 0762891422