In Summary
  • Kwa bahati mbaya sana jamii haikuwahi kuelezwa ingechukua muda gani kuiva dawa hiyo ya kuulia mchwa kwenye halmashauri. Kilichoshudiwa viongozi serikalini walipofanya ziara mikoani na wilayani waligundua ubadhirifu mkubwa wa mali na fedha za umma pamoja na watendaji wezi wabadhirifu, wazembe na wasiotekeleza wajibu wao lakini waliishia kulalamika tu.

Katika kipindi fulani miaka iliyopita ilionekana kula fedha za umma ni ujanja. Na japokuwa waliokuwa wanatafuna fedha hizo walikuwa wakijulikana, waliishia kutajwa kuwa ni mchwa ambao dawa yao ilikuwa jikoni.

Kwa bahati mbaya sana jamii haikuwahi kuelezwa ingechukua muda gani kuiva dawa hiyo ya kuulia mchwa kwenye halmashauri. Kilichoshudiwa viongozi serikalini walipofanya ziara mikoani na wilayani waligundua ubadhirifu mkubwa wa mali na fedha za umma pamoja na watendaji wezi wabadhirifu, wazembe na wasiotekeleza wajibu wao lakini waliishia kulalamika tu.

Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC zilipogundua madudu kwenye halmashauri na mashirika ya umma “mchwa” hao hawakushughulikiwa.

Hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilipoonyesha kwa uwazi uzembe, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha na mali ya umma bado hakuna ufuatiliaji wa kina uliofanyika.

Taifa likabaki la watu walalamishi. Wakati wananchi walilalamika miradi ya maendeleo kukamilika nusunusu au kutokamilika kabisa huku fedha zilizotolewa na Serikali kuu au wafadhili zikiwa zimeisha, viongozi nao walilalamika kukithiri kwa mchwa huku wakisema dawa yao iko jikoni.

Tunafurahi kuona kwamba kwa sasa mchwa wanashughulikiwa. Fursa ya watu kuchota fedha za maendeleo au kuzitumia tofauti na malengo yake – mfano – badala ya kuzielekeza kwenye miradi watendaji wakaamua kugawana posho – zimeisha na sasa Watanzania wanaona wakishughulikiwa kikamilifu.

Hilo linaonekana kupitia ziara za Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika maeneo mbalimbali ambazo zimekuwa zikiacha ‘vumbi’ kwa viongozi wa umma kuwajibika.

Kuanzia Januari mwaka huu, baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa matumbo joto kutokana na kukamatwa na polisi au kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Wapo wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha na wengine kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Miongoni mwa waliofikishwa Takukuru ni mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji Musoma (Muwasa), ambaye alituhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji wilayani Bunda. Mkurugenzi huyo aliponzwa na kuchelewa kutekelezwa kwa mradi wa maji licha ya Serikali kutoa fedha naye akamlipa mkandarasi zaidi ya Sh7 bilioni.

Mwingine aliyefikishwa Takukuru ni meneja wa Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Mara, kwa kushindwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Butiama. Serikali ilitoa Sh600 milioni tangu Aprili mwaka jana kwa ajili ya ujenzi huo lakini hadi wakati wa ziara ya Waziri Mkuu alikuwa hajafanya chochote.

Mwezi uliopita akiwa mkoani Mwanza alimsimamisha kazi mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kuidhinisha malipo ya Sh279 milioni kwa kampuni ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

Kadhalika akiwa ziarani Mtwara, aliagiza Takukuru kumtafuta popote alipo aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Masasi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Rai yetu ni kwamba jukumu la kushughulikia wanaotumia madaraka yao vibaya lisisubiri viongozi wa juu tu. Tunashauri wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya na mikoa wafuatilie kwa karibu na kudhibiti kabla ya kufika huko.

Lakini pia tunatoa wito kwamba pamoja na kasi kubwa ya utendaji inayoshuhudiwa sasa na ufuatiliaji wa karibu, haki itendeke, watuhumiwa wapewe fursa ya kujieleza ili wasihukumiwe majukwaani kisiasa.