In Summary
  • Wengi watakumbuka michuano hii ilivyokuwa miaka ya kuanzia 1970 hadi takribani miaka ya mwanzoni mwa 2000. Michuano hii ilivutia wadau wengi na ilishabihiana kwa ubora na michuano ya Cecafa kwa timu za Taifa.

Michuano ya Cecafa inayoendelea hapa nchini jijini Dar es Salaam imekosa msisimko uliozoeleka na hili linadhihirishwa na idadi ndogo ya watazamaji wanaoingia uwanjani kushuhudia mechi hizi zinapofanyika.

Wengi watakumbuka michuano hii ilivyokuwa miaka ya kuanzia 1970 hadi takribani miaka ya mwanzoni mwa 2000. Michuano hii ilivutia wadau wengi na ilishabihiana kwa ubora na michuano ya Cecafa kwa timu za Taifa.

Katika mashindano yote hayo, hali imekuwa tofauti na binafsi naona kuna sababu nyingi zilizotufikisha hapo.

Uongozi wa juu wa Cecafa kutokuwa wabunifu

Michuano ya Cecafa iwe katika ngazi ya mataifa au klabu imekuwa na changamoto kubwa ya kupata udhamini. Binafsi naona hili linachangiwa na sekretarieti ya Cecafa inayongozwa na katibu mkuu kutokuwa na mikakati ya kiubunifu kuvutia wadhamini wa kutosha.

Hili linaweza kuchangiwa na ama uongozi wa Cecafa kutokuwa na mipango endelevu, kutotimiza masharti ya wadhamini baada ya kuwa wamekubaliana au fedha inayokuwa imetolewa kutotumika ipasavyo.

Ni kutokana na kutokuwa na ufadhili huo kwa muda mrefu, mashindano haya yameshindwa kuwa na ratiba inayotambulika kama ilivyokuwa miaka ya zamani ambako kila mdau wa mpira wa miguu alijua Cecafa ngazi ya klabu au timu za Taifa itafanyika lini.

Kutokana na kasoro hiyo, vyama vya mpira vya nchi husika vinashindwa kuyaingiza mashindano hayo kwenye kalenda zao ambazo zingewezesha klabu vya nchi hizo kujipanga hususani vile ambavyo vimekuwa mabingwa.

Mataifa ya ukanda huu kutokuwa na mipango stahiki ya kuendeleza mchezo huu

Ukanda huu ndiyo ulioko nyuma katika maendeleo ya soka Afrika na hili linadhihirishwa na timu za ukanda huu kutofanya vizuri katika kufuzu fainali za Chan, Afcon na Kombe la Dunia na hata katika ngazi ya klabu (mashindano ya klabu bingwa na kombe la washindi). Kutofanya vizuri kwa timu zetu kunaendelea kupunguza uwezekano wa mashindano ya Cecafa kupata wadhamini. Ni vyema Cecafa kwa kushirikiana na wadau ikaweka mkakati maalumu ya kutuondoa hapo tulipokwama. Naamini hilo likifanyika, timu zetu zitafanya vizuri na wadhamini watapatikana.

Muda wa mashindano

Mashindano ya Cecafa hayana ratiba maalumu, huenda kwa kubahatisha na pale ambako mdhamini hupatikana, taarifa hutolewa muda mfupi kabla ya mashindano kuanza.

Hali hiyo inakuwa kero kwa timu ambazo zinatakiwa kushiriki, hususan ngazi ya klabu kwa sababu huwa na mipangilio yake na idadi ya wachezaji wanaowatumia kwenye klabu kwa msimu huwa ni ndogo (isiyosidi 30) ambao wanatakiwa washiriki ligi za nyumbani, za kimataifa na wengine timu zao za Taifa.

Klabu huamua ama ishiriki kwa kuwatumia wachezaji wasiokuwa tegemo au kujitoa katika mashindano. Hali zote hizo zinapunguza mvuto wa watazamaji kwenda viwanjani kuangalia mashindano hayo. Aidha, Cecafa walijua huu ni msimu wa Kombe la Dunia ambao wachezaji wote mahiri duniani wanashiriki, hili limepunguza pia idadi ya watazamaji kwenda kuangalia mechi za Cecafa kwa sababu huamua kukaa nyumbani kuangalia michuano hiyo nambari moja duniani.

Kwa kuangalia upungufu huo, ni vyema Cecafa ikajitathmini na anguko hilo la mpira wa miguu katika ukanda huu ili msisimko uliokuwapo urudi tena na hadhi ya ukanda huu irejee.