In Summary
  • Hii ni pamoja na madarasa bora, mabweni kwa ajili ya malazi pamoja na madawati ambayo Serikali na wadau wa elimu wamekuwa wakifanya kila jitihada kuhakikisha hakuna mwananfunzi anayekaa chini.

Maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma hutegemea aina ya mazingira anayoishi.

Hii ni pamoja na madarasa bora, mabweni kwa ajili ya malazi pamoja na madawati ambayo Serikali na wadau wa elimu wamekuwa wakifanya kila jitihada kuhakikisha hakuna mwananfunzi anayekaa chini.

Hilo limefanikiwa kwa asilimia kubwa japokuwa ripoti mbalimbali zimekuwa zikionyesha kuwapo kwa uhaba wa madawati kwa baadhi ya shule.

Mambo yote hayo kwa pamoja huchangia ustawi wa mwanafunzi awapo shuleni. Hata hivyo, kuna changamoto ambayo hivi karibuni imekuwa ikizikumba shule nyingi nchini. Jinamizi la moto limeendelea kuteketeza mali za shule na kuwaathiri wanafunzi kitaaluma.

Usiku wa kuamkia Agosti 29 ulikuwa wa huzuni kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari Mihayo iliyopo Tabora baada ya moto kuteketeza mabweni yao.

Kuteketea kwa mabweni hayo kumeleta athari nyingi na kubwa kwa wanafunzi. Julai mwaka huu, bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari St Joseph Rutabo mkoani Kagera lilitekea kwa moto majira ya usiku na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja.

Pia, Juni mwaka huu, Shule ya Sekondari Kazima iliyopo mkoani Tabora ilikumbwa na jinamizi hilo baada ya kuteketea kwa moto ambapo madarasa yaliungua. Kama haitoshi, Korogwe High School nayo iliteketea kwa moto mwezi Machi ambapo mabweni ya wasichana yaliungua kwa moto.

Hii ni mifano michache. Majanga ya moto yamekuwa yakiziandama shule nyingi huku hatari ya kupoteza maisha ya wanafunzi ikizidi kuwa kubwa.

Huenda kuna dalili za uzembe kwenye matukio haya ambayo mara nyingi yanasababishwa na kutokuwapo kwa vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuzimia moto.

Ni dhahiri kuwa shabaha ya Serikali ya kuimarisha elimu nchini haitaleta tija endapo masuala kama haya hayatapewa jicho la tatu.

Moja ya sababu za moto ni hitilafu za umeme ambazo kwa kawaida zinaweza kutokea kwenye nyumba au majengo ikiwamo mabweni na madarasa.

Lakini swali ni namna gani taasisi hizi za elimu zimejipanga kukabiliana na matatizo haya?

Waswahili wanasema, “Usipoziba ufa utajenga ukuta”. Wakati moto ukiteteketeza mabweni na madarasa, athari za moja kwa moja huwakumba wanafunzi ambao hupoteza muda wa masomo.

Lakini pia, wafanyakazi wakiwamo walimu huweza kuathirika kisaikolojia pale malengo na ratiba zao za kufundisha zinapovurugika. Hii inawakuta zaidi walimu wanaothamini muda.

Athari kubwa zaidi inakwenda kwa wazazi ambao jukumu lao ni kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji muhimu ya shule, ikiwamo mavazi na vitendea kazi kama vitabu na madaftari ambavyo pindi vinapoteketea kwa moto huwa mzigo kwao.

Huu ni wakati muafaka kwa wadau wa elimu kuona umuhimu wa kuchukua tahadhari sanjari na kuandaa mipango mathubuti ya kudhibiti majanga ya moto shuleni.

Mosi, viongozi wa shule wanatakiwa kuhakikisha miundombinu ya umeme katika majengo ni ya uhakika na inakaguliwa mara kwa mara.

Pili, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), linao wajibu wa kuzipa kiapumbele shule kwa kufanya uhakiki wa miundombinu ikiwamo usukaji wa nyaya, nguzo pamoja na kuchunguza matumizi yake.

Ni muhimu kwa kila shule kuhakikisha inakuwa na vifaa vya dharura vya kuzimia moto, vya kutosha na viwe vinafanya kazi ili kupunguza hatari ya kuenea kwa moto.

Aidha, wanafunzi waelimishwe kuhusu namna sahihi ya kutumia vifaa hivyo, hususan kwa kutumia wanafunzi wa kikosi cha skauti ili kuwa mbadala wa waokoaji na Jeshi la Zimamoto.