Nchi nyingi duniani zimekuwa zikiingia katika machafuko kutokana na kauli za wanasiasa wanaoshindwa kufikia malengo yao ama wanaopinga matendo ya Serikali zao au kundi fulani.

Ni ukweli usiopingika kwamba silaha kubwa ya wanasiasa ni nguvu ya umma, hivyo wapo ambao wanaweza kuitumia vizuri na wengine wanaitumia vibaya kwani nguvu hii ni nadra sana kushindwa.

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa Julai 28, 2015 alijiengua CCM na kujiunga na Chadema baada ya kuenguliwa kugombea urais.

Julai 30 mwaka huo, Lowassa alichukua fomu kugombea urais kupitia Chadema na baadaye chama hicho kilimuunga mkono na kuungana na vyama vingine vitatu ikiwamo CUF, NLD na NCCR- Mageuzi katika muungano uliokuja kufahamika kama Ukawa.

Hakika alitoa upinzani mkubwa ambao haujawahi kutokea kwa chama tawala na alifanikiwa kujikusanyia kura zaidi ya milioni sita za Watanzania kura ambazo ni nyingi kwa upinzani kuwahi kupatikana katika uchaguzi wa kisiasa nchini.

Ushawishi wake pamoja na viongozi wenzake wa upinzani sio ulisaidia kuongeza idadi kubwa ya kura na kutoa upinzani kwa nafasi ya urais, pia uliwezesha kupata idadi kubwa ya wabunge na madiwani katika kambi hiyo.

Kampeni za Lowassa zilizokuwa na kaulimbiu ya mabadiliko, yeye binafsi hakuweza kutoa kauli za kejeli kwa CCM alikotoka licha ya kurushiwa ‘madongo’ mengi na chama chake hicho cha zamani.

Machi Mosi, Lowassa amerejea CCM akisema anarudi nyumbani. Ilikuwa ni habari kubwa ndani na nje ya nchi, lakini haikuwashangaza wengi kutokana matendo aliyofanya kabla ya kufikia uamuzi huo.

Haikushangaza pia kutokana na ukweli kwamba, Lowassa licha ya kuhamia upinzani siasa zake zilionekana ni tofauti na siasa za upande huo hasa kutokana na kulelewa katika misingi ya kisiasa ya CCM.

Lakini pia haikuwa ajabu kwa viongozi wa CCM Taifa kumpokea baada ya majadiliano ambayo yanaelezwa yalichukua saa nane, kwani Lowassa naye hakuwa na ugomvi wa moja kwa moja na viongozi hao tofati na wanachama wengine ambao wanaondoka na kuacha makovu makubwa ndani ya vyama vyao vya zamani.

Hata kwa upande wa Chadema, viongozi wake wa juu waliopata fursa ya kutoa maoni yao baada ya Lowassa kurejea CCM walimtakia maisha mema na kueleza wanathamini mchango wake wa 2015 na hakukuwa na aliyediriki kutoa maneno ya kashfa na kebehi kwake. Machi 9, Lowassa alirudi nyumbani Monduli akiwa CCM na kupata mapokezi makubwa yaliyotawaliwa na mbwembwe za hapa na pale kutoka kwa wafuasi wa CCM.

Baadhi ya viongozi na wabunge wa chama hicho waliopata fursa ya kuzungumza katika hafla ya mapokezi licha ya kumpongeza kurudi nyumbani, walirusha madongo na kejeli kwa Chadema.

Hata hivyo, alipopata fursa ya kuzungumza, Lowassa alionyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa kwa kuwapongeza wanaChadema akisema “asanteni sana.”

Pia alitumia fursa hiyo kushukuru kura milioni sita alizopigiwa na kueleza kuwa zilikuwa ni nyingi, si haba, na akataka waliompigia kumuunga mkono Rais John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Lowassa alitumia fursa hiyo pia kukemea siasa za ubaguzi na kuwataka Watanzania kurejea katika udugu, kwa madai kuwa mtu kuwa Chadema au CCM si uadui kama ilivyo kwa Uislamu na Ukristo.

Huyo ndiye Lowassa ambaye mara zote siasa zake hazitumii kejeli na badala yake hujenga hoja ya ushawishi kwa nini aliamua kutoka chama kimoja kwenda kingine.

Lowassa anaeleza kuwa amerejea CCM kwa kuwa anaridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli.

Vilevile, anakumbusha suala la amani na kuwataka Watanzania kuilinda akimalizia kwa kuwaacha vinywa wazi wahafidhina.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humfrey Polepole anamtaja Lowassa kama kiongozi aliyekomaa kisiasa na mathubuti ambaye ameweka pembeni siasa na kutanguliza utaifa mbele huki akisisitiza amani.

Tukio hili linatoa funzo kubwa kwa wanasiasa wengine kwanza ni kuwa na akiba ya maneno, lakini pia kutambua vyama vya siasa ni majukwaa tu ya kufikisha ujumbe kwa watu na hayawezi kuwajengea uadui katika jamii.

Lakini pia kila jambo lina wakati wake na sababu zake na kama jambo haliwezekani kulilazimisha huleta madhara makubwa zaidi.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha anapatikana kwa simu 0754-296503