Siku ya mkesha wa Mwaka Mpya – 2019, nilipokea kazi mbili. Moja ilihusu taarifa ya kusambaza kwa wadau wa habari. Niliitendea haki na kuonyesha muhusika kwanini haikuwa kazi bora kutoka kwa mwandishi wa habari. Alikubaliana nami. Tuliitupa.

Niliahidi kufanya kazi ya pili siku iliyofuata. Haikuwezekana. Ninaifanya leo. Mwandishi anaomba msaada katika lugha ambayo haijahaririwa. Soma: “Mzee Ndimara, nisaidie. mkoani kwangu kuna tatizo la wanafunzi kukatisha masomo kwa ujauzito. Kwa mwaka huu (2018) peke yake watoto 1,907 wamekatisha masomo. Kuna wilaya moja ambako watoto waliokatisha masomo wanafikia 400 katika kipindi cha miezi sita tu.

“Ninataka kufanya habari ya uchunguzi… Tafadhali nisaidie pa kuanzia, maswali ya kuuliza na nani niwahoji. Nitashukuru.”

Twende hivi: Katika kufanya uchunguzi au hata kutoa taarifa yoyote ile, sharti utumie maneno – siyo yanayopepesa maana – bali yanayosema kitu kilekile unacholenga.

Hapa basi, kirai hiki, “kukatisha masomo kwa ujauzito” hakieleweki; hivyo hakina maana. Ni kuandika au kusema kwa mazoea tu. Jiulize: wamekatisha masomo kwa kuogopa ujauzito (unawatisha); kwa kuwapa wanafunzi ujauzito; au kuogopa kukamatwa kwa walichofanya kuhusiana na ujauzito? Humu kuna wanafunzi wa kiume na walimu.

Kwa upande wa wasichana, kukatisha masomo ni kwa kuogopa kufahamika kuwa wana ujauzito; kuogopa kutaja waliowapa ujauzito; kukwepa “aibu” ya kuwa na ujauzito darasani; kwa kutaka kuoelewa (baadhi huwa wamelipiwa mahari); kwa kufukuzwa na utawala wa shule; au wamepotezwa na watu wasiojulikana?

Kwa mfano, ukiandika moja kwa moja kuwa wasichana waliopata ujauzito (idadi) ndio wameacha shule, wamefukuzwa au wameolewa; unakuwa umeondoa mkanganyiko unaosababisha maswali yaliyoulizwa hapo juu.

Kwahiyo, kinachohitajika tangu mwanzo ni kubainisha unachotaka kufanya. Kwani kubainisha ni kufukua, kuchambua na kufafanua – kwa kina na umakini – kile unacholenga miongoni mwa vitu vingi vilivyoko mbele yako.

Ukiangalia kwa haraka, waweza kuona kwamba mwandishi anayetaka msaada hakuwa na sababu ya kuuliza, kwani tayari amegundua “kuna tatizo” na amelitaja. Aidha, ana tarakimu zinazoonyesha anachotaka kuandika juu yake.

Lakini anataka kujua mahali pa kuanzia, maswali gani ya kuuliza na nani hasa awahoji. Kwa haya matatu, tunamrejesha katika masomo ya awali yaliyowahi kutolewa katika safu hii.

Si una somo la kuandika juu yake? Umelipataje? Nini kimekusukuma kuona kuwa ni somo “muhimu” la kuandika juu yake? Kwanini hasa unataka kuandika juu ya hili? Unajua nini zaidi juu ya hili? Umuhimu wake ni nini? Kwa nani? Unalenga kupata matokeo gani?

Unasema ni tatizo: Ni tatizo kwa nani? Ni tatizo vipi? Kwa muda gani? Liliwahi kushughukikiwa? Na nani? Lini? Matokeo yake yalikuwaje? Halikuwahi kushughulikiwa? Nani walipaswa kulishughulikia? Kwanini hawakulishughulikia? Unataka kuandika ili iweje?

Muhusika anaomba, “Tafadhali nisaidie pa kuanzia.” Tuanze. Takwimu hizi umezipata wapi? Kwa nani – mamlaka ipi? Una uhakika gani kwamba ziko sahihi? Unamwamini aliyekupa taarifa hizi? Una uhakika wa ripoti ulimozichukua – ya nani, ya lini? Unahitajika utibitisho kabla ya kuzitumia. Unaandika “kuna tatizo la wanafunzi kukatisha masomo kwa ujauzito.” Lugha bwana! Humu hakuna maneno “kuwapa” au “kupata.”

Kwahiyo, “kukatisha masomo kwa ujauzito” yaweza kuwa na maana ya kujiandaa kupata ujauzito, kwa kuogopa ujauzito, kwa kufanywa wajawazito, kwa kuwapa wenzao ujauzito, kwa aibu ya kuwa wajawazito shuleni. Humu basi waweza kukuta wasichana na wavulana/wanaume (labda na walimu).

Achana na mzozo wa lugha. Njoo hapa. Unaandika, “Kwa mwaka 2018 peke yake watoto 1,907 wamekatisha masomo. Ili tarakimu hii iwe na maana, inabidi tuambiwe pia ambao wamesalia shuleni na katika madarasa yapi. Tulinganishe. Bila hivyo, kinachoonekana kuwa idadi kubwa kitakuwa mzaha.

Vivyohivyo, ili tuelewe uzito wa unachoita tatizo kwa watoto 400 kukatisha masomo katika wilaya moja na katika miezi sita tu, sharti tujue hiyo ni kati ya takwimu ipi kuu inayolinganishwa.

Ili takwimu hizi ziwe za maana, kuna haja ya kulinganisha idadi ya waliokatisha masomo; siyo tu kwa mwaka mmoja bali miaka miwili au mitatu iliyopita ili kujenga muktadha. Haitoshi kuranda tu tarakimu zisizofafanulika kiuchambuzi. Kwa mfano, kuliko kutaja tu “waliotoka” shuleni, ni busara kueleza kuwa miongoni mwa wanafunzi 15,700 katika mkoa fulani, 1,907 waliacha, waliachishwa au walifukuzwa shule “kuhusuana na ujauzito.”

Bali bila kutaja moja kwa moja kwamba “walipata ujauzito,” idadi hiyo inaweza kujumuisha walimu au wanafunzi wa kiume walioacha shule au ualimu kutokana na woga, shinikizo au kushitakiwa kwa kuhusishwa na ujauzito wa wanafunzi. Haiishii hapo. Kuna haja ya kujua walioondoka walikuwa darasa gani ili msomaji ajue mapengo yako eneo lipi na wahusika waweke wapi nguvu kukabiliana na tatizo analoona mwandishi.

Heri ya Mwaka Mpya 2019.