In Summary
  • Miongoni mwa maelekezo aliyoyatoa ni pamoja na kuwaagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe na wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango kukutana haraka ili kumaliza kilio cha kodi kwenye vifaa vya ujenzi.

Akiwa mjini Mwanza juzi kushuhudia utiaji saini wa mikataba minne ya ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo ya Serikali, chelezo na ukarabati wa meli za Mv Butiama na Mv Victoria, Rais John Magufuli alizungumza mambo mengi na kutoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali.

Miongoni mwa maelekezo aliyoyatoa ni pamoja na kuwaagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwelwe na wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango kukutana haraka ili kumaliza kilio cha kodi kwenye vifaa vya ujenzi.

Rais Magufuli alitoa muda wa wiki moja kwa mawaziri hao kukutana kumaliza tatizo la Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwenye miradi ya ujenzi akisema inachelewesha na kukwamisha maendeleo.

Alisema suala la msamaha wa Vat ni kikwazo kwa miradi ya maendeleo akitoa mfano kuwa unakuta miradi iko tayari kutekelezwa, lakini linakuja suala la Vat linaloikwamisha.

Kisha akaagiza akisema, “Waziri (wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Kamwelwe), kaeni na waziri wa Fedha mlimalize hili na limalizike ndani ya wiki moja.”

Tunapongeza kauli ya Rais katika suala hili ikizingatiwa kwamba miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu kama barabara, madaraja, reli na hata ile ya majengo imekuwa ikikumbana na kadhia ya vifaa vinavyopaswa kutumika kukwama kwa sababu ya kodi.

Mfano wa hivi karibuni ni ule uliotolewa na mmoja wa maofisa wa kiwanda kimoja cha uzalishaji wa saruji katika mkutano ulioitishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya ambaye alieleza juu ya kodi kubwa wanayotozwa pale wanapoingiza vitu vinavyotumika kutengenezea saruji kutoka nje, jambo ambalo husababisha uzalishaji ama kuwa mdogo au kutokidhi.

Pia, baadhi ya mawakala wa vifaa vya ujenzi wamekuwa wakilalamika kupanda kwa bei ya vifaa hivyo kunakotokana na wao kuvipata kwa bei kubwa, hivyo wanapoviuza wanapata wateja wachache.

Ni kutokana na hali hiyo, ndiyo maana katika siku za karibuni bei ya bidhaa na vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa ajili ya ujenzi vimepanda na hivyo kuathiri shughuli zao kujiendeleza kiuchumi.

Sambamba na hilo, wananchi wamekuwa wakilizwa na bei ya vifaa vya ujenzi ambayo imepanda kutokana na kutozwa kodi kubwa inayoathiri uendelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi.

Mei 6, 2014 aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alishauri kupunguzwa au kuondolewa kwa kodi katika vifaa vya ujenzi ili Watanzania wengi waweze kujenga nyumba bora.

Akizungumza katika maonyesho ya makazi jijini Dar es Salaam ya Darproperty, Profesa Tibaijuka alisema uwepo wa kodi kubwa unasababisha watu wengi kushindwa kujenga nyumba bora na imara.

Waziri huyo alisema kodi hiyo ikipunguzwa itasababisha hata benki zinazotoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kupunguza riba na hivyo kusaidia sekta ya makazi kukua zaidi.

Wakati tukimpongeza Rais kuwataka mawaziri wa wizara hizi mbili kukutana ili kupata ufumbuzi juu ya kodi kwa vifaa vinavyotumika kwa ajili ya ujenzi miradi ya maendeleo, tunaishauri Serikali kuliangalia suala hili pia kwa upande wa wananchi ili waweze kujiendeleza na kuwa na makazi bora.

Kama alivyoshauri wakati huo Profesa Tibaijuka, tunaamini kwamba iwapo kodi itapunguzwa zaidi katika vifaa vya ujenzi, Watanzania wengi watamudu kumiliki makazi bora zaidi na hiyo itakuwa ni sifa ya ziada kwa Taifa letu kuwa lenye watu wanaoishi kwenye nyumba bora.