In Summary
  • Bila kupata haki, duara la umasikini halitakuwa na mwisho na wanawake na wasichana hawatakuwa na nafasi ya kujiinua na familia zao kutoka kwenye umasikini. Lazima tulenge katika njia bunifu za kuhakikisha usawa kamili na upatikanaji wa haki kwa wote.

Upatikanaji wa haki kwa wote maana yake ni kuwa na idara ya mahakama ambayo huwahudumia na kuakisi kila mmoja katika jamii. Makundi yote kama wanawake, wafanyabiashara ndogondogo, maskini vijijini na mijini na wengineo lazima wapate kuwakilishwa katika mahakama. Usawa wa kijinsia katika mfumo wa sheria si jambo la kuchagua iwapo kweli tumedhamiria kuwepo kwa haki kwa wote. Bila kupata haki, duara la umasikini halitakuwa na mwisho na wanawake na wasichana hawatakuwa na nafasi ya kujiinua na familia zao kutoka kwenye umasikini. Lazima tulenge katika njia bunifu za kuhakikisha usawa kamili na upatikanaji wa haki kwa wote.

Mahakama zina wajibu muhimu katika kulinda hali za wanawake, hususani katika mashauri yaliyoanzishwa na wanawake. Hii inajumuisha mashauri ya sheria za familia, kama vile masuala yanayohusu kurasimisha ndoa au talaka, kuamua atakayewatunza watoto na kuomba ulinzi dhidi ya ukatii. Nchi nyingi Afrika zimekuwa zikiongoza jitihada za kukuza usawa wa kijinsia katika mifumo yao ya sheria.

Mahakama maalumu kama vile mahakama za familia, pia na vitengo vya jinsia ndani ya mahakama kama vile Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (Tawla), wanaweza kutumia watendaji wa mahakama waliopewa mafunzo kuhusu usawa wa kijinsia na sheria zinazowajali wanawake. Kwa ubia na Benki ya Dunia, Tanzania kwa sasa inatekeleza maboresho ya mahakama kuifanya kulenga wananchi na mradi wa utoaji haki ambao chini yake Tanzania itakuwa moja ya nchi za mwanzo kujaribisha programu bunifu ya haki kwenye magurudumu.

Programu hii inahusisha mahakama zinazotembea na kuchukua huduma za mahakama moja kwa moja kwa makundi hatarishi kama vile wanawake, wafanyabiashara ndogo ndogo na masikini vijijini. Kwa kutumia mabasi, gari ndogo za abiria au magari mengine yaliyoundwa kama mahakama zinazotembea kwenye maeneo ya vijijini na mijini, mradi huu ni sehemu muhimu ya uboreshaji wa mahakama unaozingatia haki za mwananchi na mradi wa kutoa huduma za mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Itawezesha upatikanaji salama na unaofanya kazi wa huduma za sheria na kusaidia kuhakikisha walengwa wanazitumia. Kwa kuimarisha utawala wa sheria na kupunguza ukosefu wa usawa, upatikanaji wa haki unaruhusu watu wote kutumia mfumo wa sheria kupigania maslahi yao na kuhakikisha usimamizi wa sheria. Hii haihusu tu kuwashtaki wenye makosa ya jinai. Pia ni kuhusu kuwawezesha wanawake na kushughulikia masuala ya msingi yanayohusu ukosefu wa usawa wa kijinsia ambao upo katika jamii zote. Wakati huohuo, upatikanaji wa mfumo wa sheria ni sehemu muhimu ya ujasiriamali wa wanawake na ajira, kwani huathiri uwezo wao wa kusafiri, uwezo wa kufanya maamuzi na matumizi mazuri ya sheria na kanuni.

Wakati kupanua upatikanaji wa haki ni hatua ya kwanza, lazima tuende mbele zaidi. Lazima tuhakikishe kwamba upatikanaji huu unajitafsiri kuwa haki inayofanya kazi. Ili kuwalinda wanawake, tunahimiza Serikali kuanzisha mahakama mahususi na taratibu za mashauri ya ukatili wa kijinsia. Kuanzisha taratibu zinazoharakisha na kuruhusu amri za kulinda kwa mashauri ya ukatili huweza kufanya mfumo wa mahakama kuwajali zaidi wakati zikiwapa wanawake kujiamini zadi kwamba inaweza kusaidia.

Ukatili huwaathiri wanawake na wasichana wa rika zote, bila ya kujali mahali, kiwango cha kipato au hadhi katila jamii. Inaweza kudhoofisha uwezeshaji wao kiuchumi kwa kuzuia ajira na kuzuia upatikanaji wa rasilimali fedha. Nchini Tanzania, utafiti wa hivi karibuni umeonyesha wanawake wanaojihusisha katika ajira rasmi zinazolipa ujira ambao wanakumbana na ukatili mkali wa mwenza wanakuwa na kipato asilimia 60 chini ya wanawake ambao hawakumbani na ukatili kama huo. Katika moja ya ripoti zake, Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC) cha Tanzania, kimeona wanawake nchini kwa kawaida hunyimwa haki ambazo hupewa na sheria za kimataifa na za ndani. Ukiukwaji huu hutokea kwa sababu ya sheria za mfumo dume, na desturi za kimila zikiwa katika duru za umma na binafsi..

Mahakama ya Tanzania inapanga kuanzisha ‘kituo kimoja cha huduma’ kitakachojikita katika kushughulikia mashauri ya mirathi na familia katika kituo kimoja cha mahakama na taratibu zinazoharakishwa kutoka kufungua jalada hadi hukumu ya mwisho. Kwa kuanzisha mahakama mahsusi na taratibu, mahakama itahakikisha kwamba mashauri yanashughulikiwa vya kutosha na zinatoa uhakikisho mkubwa kwa wanawake kwamba kuleta mashauri mahakamani kutasababisha matokeo ya haki na yaliyo mazuri. Hii inajumuisha kuwa na majaji, waendesha mashtaka na wafanyakazi wa mahakama ambao wamepatiwa mafunzo vizuri na wenye ujuzi wa kushughulikia mashauri ya ukatili wa kijinsia. Pia ina maana kuwa na amri ya kuwalinda wanawake dhidi ya ukatili wa wakati huo au baadaye.

Sheria ambazo huongoza taratibu za mahakama zinaweza kuanzisha mazingira yanayojali jinsia, yakizingatia usiri na faragha. Hii inajumuisha kuruhusu wanawake wanaokabiliwa na ukatili wa kingono kutoa ushahidi kwenye vyumba vya faragha, pia na kuweka taratibu ambazo ni rafiki katika kutatua migogoro, maeneo maalumu ya waathirika, mahitaji ya ushahidi yaliyo rahisi.

Tunatoa wito kuongezwa idadi ya majaji wanawake ili kuifanya mahakama kuwa wakilishi zaidi kwa wanawake. Zaidi ya yote, tunahitaji ushirikiano zaidi katika mnyororo wa sheria, mafunzo na kubungua bongo ili kusaidia upatikanaji wa haki inayofanya kazi kwa wanawake wote barani Afrika. Bila kuruhusu upatikanaji wanaohitaji, hatuwezi kufikia shabaha yetu ya kuondoa umasikini na kuimarisha ustawi shirikishi.

** Prof Ibrahim Juma ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

* Sandie Okoro ni Makamu wa Rais Mwandamizi na Mshauri Mkuu wa Benki ya Dunia