In Summary
  • Lakini furaha ya mama huyu mara nyingi hukumbana na changamoto nyingi kutokana na kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na uzazi hasa wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.

Uzazi ni jambo la kheri na kila mwanamke anatamani apate ujauzito hatimaye ajifungue salama na kurejea nyumbani akiwa na afya njema yeye na mwanawe.

Lakini furaha ya mama huyu mara nyingi hukumbana na changamoto nyingi kutokana na kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na uzazi hasa wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.

Inaelezwa vifo vya mama na mtoto au wote, husababishwa na matatizo ya afya au uzembe wa mjamzito au mkunga.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema matatizo mengi yanayosababisha vifo kwa wajawazito na watoto yanaweza kupungua kwa zaidi ya asilimia 80 kama mjamzito atahudhuria kliniki ya mama na mtoto kwa kipindi chote cha ujauzito wake na wakati ukifika akajifungulie katika vituo vya afya au hospitali.

Nini kinasababisha vifo hivyo?

Sababu kubwa zinazoainishwa na wataalamu ni pamoja na huduma duni, umbali wa vituo vya afya na maeneo watokayo wajawazito hasa maeneo ya pembezoni.

Pia uhaba wa wakunga na wajawazito kwenda kujifungulia kwa wakunga wa jadi wasio na utaalamu, pia uhaba wa vifaatiba.

Kwa mujibu wa takwimu za afya utafiti uliofanywa na Tanzania Demographic Heath Survey mwaka 2015-2016 (TDHS), zinaonyesha kila siku wanawake 30 hufariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi.

Hali hii inaweza kumtia mashaka kila mwanamke ambaye anatarajia kubeba ujauzito.

Wadau wanalizungumziaje tatizo hili?

Muungano wa Utepe Mweupe wa Uzazi Salama Tanzania unaojumuisha mashirika zaidi ya 25, unasema umejidhatiti kutoa elimu na vifaatiba ili kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama wakati wa kujifungua na hata katika makuzi ya mtoto.

Rose Mlay ni Mratibu wa Taifa wa Mtandao huo, anasema njia pekee ya kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua ni kwa kuhakikisha wajawazito wote wanahudhuria kliniki na wanajifungulia katika vituo vya Afya.

“Takwimu za vifo vya wajawazito na watoto sio nzuri licha ya juhudi zinazofanywa kuzuia, lakini bado hali ni mbaya. Na hii ni kwasababu bado watu wetu hawaoni umuhimu wa kuhudhuria kliniki wala kujifungulia katika vituo vya afya,” anasema Mlay.

Akinukuu TDHS za mwaka 2015/2016 Mlay anasema kila siku watoto 180 wanaozaliwa hufariki dunia na wale walio chini ya miaka mitano ni 268 kutokana na matatizo mbalimbali.

Mratibu huyo anasema kupata mimba katika umri mdogo pia kunachangia kwa kiasi kikubwa mama au mtoto kupoteza uhai wakati wa kujifungua.

“Takwimu hizi zinaonyesha asilimia 27 ya wasichana walio chini ya miaka 20 nchini wana watoto na wengine wana ujauzito jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mama na mtoto,” anasema Mlay.

Kwa upande wa wajawazito pekee, Mlay anasema wengi wao hufariki dunia wakati wa kujifungua.

Anasema katika hatua hiyo, wengi hujikuta wakipoteza maisha wao au watoto wanaowazaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua.

“Wengine vifo vyao huchangiwa na kupata maambukizi sugu ya bakteria na maradhi mengine ambayo hayakutibiwa vizuri wakati wa ujauzito au baada ya kujifungua au kupata kifafa cha mimba,” anasema Mlay.

Anasema pia utoaji mimba usio salama umetajwa kuwa sababu ya vifo vya wajawazito hasa katika nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila siku wanawake 830 hufariki duniani kutokana na matatizo wakati wa kujifungua na asilimia 99 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zinazoendelea.

Vifo hivyo vitazuiwaje?

Mama anapaswa kuanza kliniki mara tu anapogundua kuwa ni mjamzito na kufuata maelekezo yote anayopewa na wataalamu wa afya kwa wakati wote wa ujauzito.

Pia, wajawazito wote wanapaswa kujifungulia katika vituo vya afya na waendelee kuhudhuria kliniki kwaajili ya mtoto hadi atakapofikisha miaka mitano.

Annua Mhogo ni Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoani Morogoro, anashauri wajawazito wapate mlo kamili wakati wote ili kulinda afya yake na ya mtoto aliyeko tumboni.

Mhogo ameionya jamii kuepuka ndoa na mimba za utotoni ili kuepuka vifo wakati wa kujifungua.

“Tunaendelea kutoa elimu ili wanandoa wote mke na mume waone umuhimu wa kuhudhuria kliniki kusudi wapate elimu itakayowasaidia kulea vyema mimba na wahakikishe mama anajifungulia kwenye kituo cha afya au hospitali,” anasema Mratibu huyo.

Kwanini wajawazito wengi hawajifungulii katika vituo vya afya?

Kutojifungulia katika vituo vya afya kumetajwa kuchangia vifo vya wajawazito na watoto kutokana na kuhudumiwa na wakunga wasio na utaalamu wala vifaa kwaajili ya kumuhudumia mama na mtoto akishajifungua.

Baadhi ya viongozi wa nchi zinazoendelea, wanakiri kwamba vituo vya afya vilivyopo ni vichache hivyo wajawazito wengi hasa wa maeneo ya vijijini hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

Mkazi mmoja wa Kijiji cha Ukwamani Wilayani Gairo, Michael Lyahuri anasema katika eneo analoishi kuna zahanati moja inayotegemewa na vijiji vitano.

Anasema mara nyingi wajawazito husafiri zaidi ya kilomita tano ili kuifikia zahanati hiyo hali inayowakatisha tamaa na kuamua kwenda kwa wakunga wa jadi kupta huduma.

“Wapo wanaopenda kuhudhuria kliniki lakini umbali unasababisha washindwe kufika,” anasema Lyahuri ambaye anatoka wilaya yenye kituo kimoja tu cha afya kinachotegemewa na wakazi zaidi ya laki mbili.

Umaskini unaelezwa kuwa kikwazo kingine kwa wajawazito kwenda kujifungulia katika vituo vya afya kwa kuhofia kutozwa fedha za kununulia vifaa vya kujifungulia pindi vikikosekana.

Rehema Kimoleta ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Afya eneo la Gairo, anasema lugha chafu za baadhi ya wakunga kwa wajawazito zinasababisha wakimbilie kwa wakunga wa jadi.

“Mimi nawashauri wauguzi wetu wajirekebishe kwani mimi nakutana na wamama wengi na nikiwauliza kwanini hawaendi kujifungulia hospitali wanalalamikia lugha chafu za wauguzi,” anasema Kimoleta.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Charles Peter, anapingana na sababu zinazotolewa kuhusu wajawazito kutohudhuria kliniki huku akiamini kuwa bado hawajapatiwa elimu ya kutosha.

“Mimi niseme tu tatizo kubwa linaloikabili jamii ni kukosa elimu sahihi inayohusu umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya afya, wakipata elimu watabadilika wenyewe,” anasema Peter.

Hata hivyo, anaiomba Serikali na mashirika binafsi kuhakikisha wananchi wote wa vijijini wanapata elimu kuhusu athari za kujifungulia kwa wakunga wajadi ili waweze kujifungulia katika vituo vya afya.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Dennis Ngalomba anasema Wilaya yake imeweka mpango maalumu wa kushirikiana na wakunga wa jadi kuwapa hamasa ya kuwapeleka wajawazito hospitali.

“Tumeshazungumza na baadhi ya wakunga wa jadi ambao tumekubaliana wakipata mjamzito anayetaka kujifungua wampeleke kituo cha afya kilicho karibu. Tutawarejeshea nauli yao na pia tutashirikiana nao kumzalisha mama aliyeletwa,” anasema Dk Ngalomba.

Anasema wameamua kuanza kuwarejeshea nauli zao wakunga watakaowaleta wajawazito vituo vya afya, kwa lengo la kutoa hamasa kwa wengine kujitokeza na kujifungulia hospitali badala ya nyumbani.