In Summary
  • Simba iliyotumia zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 kufanya usajili, ilianza ligi hiyo kwa kishindo kwa kuikamua Ruvu Shooting mabao 7-0, Prisons ikaicharaza Njombe Mji mabao 2-1, Singida United ikapigwa mabao 2-1 na Mwadui huku Azam ikimaliza uteja kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndan

        Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania umeanza kurindima katika viwanja mbalimbali nchini, tayari mechi za mzunguko wa kwanza zimepigwa na kila timu imevuna ilichopanda.

Simba iliyotumia zaidi ya Shilingi bilioni 1.3 kufanya usajili, ilianza ligi hiyo kwa kishindo kwa kuikamua Ruvu Shooting mabao 7-0, Prisons ikaicharaza Njombe Mji mabao 2-1, Singida United ikapigwa mabao 2-1 na Mwadui huku Azam ikimaliza uteja kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda.

Mbeya City nayo ilianza kwa kicheko kwa kuifunga Majimaji bao 1-0 wakati Kagera Sugar ilianza vibaya kwa kufungwa bao 1-0 na Mbao FC ya Mwanza. Mtibwa Sugar pia ilianza vizuri kwa kuibugiza Stand United bao 1-0. Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ulikamilika jana kwa Yanga iliyocheza na Lipuli katika Uwanja wa Uhuru.

Kwa ujumla mabao 17 yalifungwa katika mechi saba za mzunguko wa kwanza zilizochezwa Jumamosi huku Emanuel Okwi wa Simba akifunga mabao manne katika mechi moja.

Ligi ya msimu huu imeonekana wazi kuwa itakuwa na ushindani kutokana na usajili uliofanywa na klabu hizo. Mbali na Simba kuvunja benki ili kujenga kikosi madhubuti, Singida United, Yanga pia zimetumia fedha nyingi kuimarisha vikosi vyao.

Yote tisa, kumi ni kwamba kuna mambo ambayo hayana budi kufanyiwa kazi kikamilifu ili kuepusha malalamiko na kuhakikisha mwisho wa msimu bingwa anapatikana kwa haki.

Mosi ni viwanja, hiki ni kilio cha miaka nenda rudi na inaonekana dawa yake itachukua muda kupatikana. Viwanja hivi vinamilikiwa na CCM. Ni vyema wasimamizi wa ligi wakaingia makubaliano ya kipindi fulani yatakayoviwezesha kuwa kwenye ubora unaotakiwa. Mara kadhaa baadhi ya viwanja kwa mfano, Nangwanda Sijaona cha Mtwara, Jamhuri cha Morogoro, Majimaji huko Songea maeneo ya kuchezea ni mabovu. Nani anawajibika kuhakikisha vinakuwa bora?

Pia suala la waamuzi. Msimu uliopita tulishuhudia waamuzi saba wakifungiwa kuchezesha soka kwa kushindwa kutafsiri sheria wawapo viwanjani. Baadhi ya waamuzi waliokutwa na rungu hilo ni Rajabu Mrope aliyechezesha mechi ya Mbeya City na Yanga iliyochezwa jijini Mbeya na Martin Saanya aliyechezesha mechi Simba na Yanga ya mzunguko wa kwanza.

Waamuzi saba kufungiwa ni jambo la kukaa chini na kutafakari, ni idadi kubwa inayotosha kujiuliza kulikoni?

Ni vyema waamuzi wakafuata miiko ya kazi yao, wasipendelee timu yoyote. Ni imani yangu wakitimiza wajibu wao, ligi yetu itakuwa na ushindani. Mwamuzi anayethamini na kujali taaluma na kazi yake, hawezi kujiingiza kwenye vitendo vya kupendelea timu yoyote.

Usimamizi, hili ni eneo jingine muhimu litakaloonyesha ni namna gani Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walivyo tayari kuona ligi inakuwa ya haki na mshindi anapatikana kwa matokeo ya uwanjani.

Katika msimu uliopita, tulishuhudia kamati za TFF zikipingana katika utoaji uamuzi jambo ambalo lilileta taswira mbaya katika uwajibikaji wa pamoja.

Ni wazi kuwa timu shiriki zina watu wao ambao wako kwenye kamati mbalimbali zilizoundwa na TFF, halitakuwa jambo la afya kwa viongozi hao kutumia kofia zao hizo kuzipendelea klabu zao kwa sababu ya mapenzi.Tutakuwa tunarudi kulekule tulikotoka.

Pia kumekuwa na tabia ya makocha kuwashambulia waamuzi pindi timu zao zinapofanya vibaya. Inawezekana ni kweli wanakosea lakini makocha wasitumie kichaka hicho kujificha. Waziandae timu zao ili zilete ushindani.

Mchambuzi ni mwandishi wa gazeti hili. 0654441793.