In Summary

Kashfa ya kuvujisha habari za siri imeelezwa kuwa imesababisha watu wengi kujiondoa mtandao wa kijamii wa Facebook

London. Matumizi ya habari yanazidi kuhama kutoka kwenye mitandao wa kijamii kama Facebook na kuhamia katika mtandao wa kutumiana ujumbe wa WhatsApp, kwa mujibu wa utafiti ambao matokeo yake yamechapishwa leo Alhamisi.

Utafiti huo pia umeonyesha wasiwasi mkubwa wa jamii ya kimataifa dhidi ya habari za uongo kwenye mitandao.

Ripoti ya taasisi ya Reuters Institute, ambayo iliangalia nchi 37 zilizo katika mabara matano, imebaini kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kupata habari, yameshuka kwa asilimia sita nchini Marekani kulinganisha na mwaka jana.

"Karibu sababu zote za kushuka zimetokana na kupungua kwa ugunduzi, kutuma na kubadilishana habari katika mtandao wa Facebook," alisema mwandishi mwandamizi wa ripoti hiyo, Nic Newman, ambaye ni mmoja wa wasisi wa tovuti ya BBC News.

Facebook ilipata pigo kubwa katika historia la jamii kupoteza imani nayo wakati kulipoibuliwa kashfa kubwa ya kukiuka faragha  mapema mwaka huu.

Kashfa hiyo ilisababisha watumiaji wengi duniani kujiondoa Facebook, na kutumia muda mwingi katika mitandao mingine kama WhatsApp na Instagram -- ambayo pia inamilikiwa na Facebook.

Taarifa hiyo ya mwaka 2018 inayoitwa 2018 Digital News Report ilibaini kuwa mtandao wa WhatsApp sasa unatumiwa kwa ajili ya habari kwa zaidi ya nusu ya watu waliohojiwa nchini Malaysia (asilimia 54) na Brazil (asilimia 48) na kwa zaidi ya theluthi moja nchini Hispania (asilimia 36)  na Uturuki (asilimia 30).

Ripoti hiyo, iliyotumia utafiti wa YouGov kwa zaidi ya watu 74,000 wanaotumia mitandao ya kijamii, ilibaini kuwa Instagram pia inazidi kuja juu barani Asia na Amerika Kusini, wakati Snapchat ilifanya vizuri barani Ulaya na Marekani.

Ripoti hiyo pia imebaini kuwa kiwango cha wastani cha kuamini habari kimeendelea kuwa asilimia 44 -- ongezeko dogo kutoka asilimia 43 mwaka jana. Hata hivyo, ni asilimia 23 tu ya waliohojiwa ambao walisema wanaamini habari wanazozikuta kwenye mitandao ya kijamii.

Habari za kweli au kughushi?

Zaidi ya nusu (asilimia 54) walikubali au walikubaliana sana kwamba wana shaka na kile kilichopo kwenye internet ni cha kweli au uongo.

Kiwango kilikuwa juu zaidi nchini Brazil ambako watu wenye shaka hiyo ni asilimia 85 na cha chini nchini Uholanzi ambako watu wenye hofu hiyo ni asilimia 30.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa watumiaji w amitandao ya kijamii wanaamini kuwa wanaotuma taarifa hizo mitandaoni au wamiliki wa majukwaa ndio wenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na tatizo la habari za uongo mitandaoni.

Asilimia 60 ya watu waliohojiwa kutoka barani Ulaya, asilimia 63 barani Asia na asilimia 41 nchini Marekani wanaamini kuwa serikali zao zingefanya jitihada zaidi kudhibiti habari za uongo.

Ripoti pia imebaini kuwa taarifa zilizo katika mfumo wa sauti (podcasts) zinakuwa maarufu kwa urahisi wa kupata habari, huku asilimia 33 ya waliohojiwa nchini Marekani na asilimia 18 nchini Uingereza wakitumia zaidi.

AFP