In Summary

Aliyekuwa waziri wa Kilimo,  Dk Charles Tizeba amelishauri Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuendelea kutoa huduma bora ili lisirudi katika hali ya zamani lilipopewa sifa ya kuwa lenye kusitisha safari muda wowote.


Dar es Salaam. Aliyekuwa waziri wa Kilimo,  Dk Charles Tizeba amelishauri Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) kuhakikisha linaendelea kutoa huduma bora na za uhakika ili kuhakikisha halirudi lilikotoka.

Tizeba ambaye ni mbunge wa Buchosa ametoa ushauri huo leo Februari Mosi, 2019 wakati ATCL ikizindua kituo chake cha huduma na tovuti iliyoboreshwa.

Dk Tizeba alizungumza kwa niaba ya wasafiri wa mara kwa mara wa shirika hilo. 

"Tungependa huduma ziwe nzuri za uhakika na kuaminika muda wote. ATC (ATCL sasa) ilifikia hatua kirefu chake kikawa Any Time Cancellation (Kusitisha safari muda wowote) badala ya Air Tanzania Cooperation (Shirika la Ndege Tanzania)," amesema Dk Tizeba.

Hata hivyo aliupongeza uongozi wa sasa wa ATCL na Serikali huku akisema huduma zikiendelea kuboreshwa na kuwa katika kiwango kizuri abiria hawatasita kuendelea kutumia shirika hilo.

Awali, mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema kituo cha huduma cha shirika hilo sasa kimeongeza muda wa kutoa huduma hadi kufikia saa 14 kwa kuwa shirika hilo linaongeza safari za nje katika mataifa ambayo yanatofautiana muda na Tanzania.

"Bado tunaendelea na maboresho na tunatarajia kuongeza muda wa huduma hadi kufikia masaa 24 ili wateja wetu waliopo katika nchi tofauti waweze kutufikia muda wowote," alisema Matindi.

Aidha kupitia tovuti iliyozinduliwa leo mteja wa ATCL ataweza kufanya 'Self Service check' masaa matatu kabla ya safari na atakuwa na uwezo wa 'kubuku' hoteli katika mji au eneo analokwenda.