In Summary

Mpaka sasa yeye mwenyewe hajaeleza ikiwa atang’atuka licha ya wito kutoka jumuiya ya kimataifa ya kumtaka aweke wazi kwamba hatagombea tena. Tshibala alisema Jumanne kwamba Kabila ataheshimu matakwa ya katiba.


Kinshasa, DR Congo. Waziri Mkuu wa DR Congo Bruno Tshibala amesema Rais Joseph Kabila hatawania tena muhula mwingine wa urais katika uchaguzi uliocheleweshwa sana kwa sababu anazuiwa na katiba iliyoweka ukomo wa mihula miwili ya utawala.

Kabila, ambaye muhula wa pili ulimalizika Desemba 2016, kikatiba hana sifa za kugombea urais katika uchaguzi wa Desemba 23, japokuwa wapinzani wake wanamshutumu kwamba anataka kung’ang’ania madarakani.

Mpaka sasa yeye mwenyewe hajaeleza ikiwa atang’atuka licha ya wito kutoka jumuiya ya kimataifa ya kumtaka aweke wazi kwamba hatagombea tena. Tshibala amesema Jumanne kwamba Kabila ataheshimu matakwa ya katiba.

"Uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa na wala Rais Kabila hatashiriki kwani atazingatia na kuheshimu maandiko ya katiba,” amesema wakati wa mahojiano kando ya Jukwaa la Kimataifa la Uchumi lililofanyika Montreal, Canada.

Kumekuwa na chuki nchi nzima dhidi ya kile baadhi wanakiona kuwa hatua ya Kabila kukataa kuachia madaraka baada ya muhula wake wa pili kumalizika Desemba 2016. Kabila aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya baba yake Laurent-Desire Kabila kuuawa.

Baada ya kufanyia marekebisho katiba alichaguliwa kidemokrasia kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na mara ya pili 211. Katiba inataka kiongozi kutawala vipindi viwili tu vya miaka mitano kila kimoja.

Wiki iliyopita, kiongozi wa upinzani Moise Katumbi aishie uhamishoni aliwahutubia maelfu ya wafuasi wake jijini Kinshasa, kupitia video na aliwahimiza kuungana pamoja dhidi ya Kabila.