In Summary
  • Serikali imesema wakati wowote itauza korosho ambazo awali zilikuwa zinunuliwe na kampuni ya Indo Power Solution baada ya kusitisha mkataba wa kampuni hiyo.

Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amewatoa hofu Watanzania kwamba wakati wowote watauza korosho baada ya kuachana na kampuni ya Indo Power Solutions Limited ya Kenya.

Ametoa majibu hayo leo Jumatano Mei 14,2019 wakati akijibu hoja za wabunge katika hotuba ya wizara yake ambapo ametangaza kuwa Serikali ilishaachana na kampuni huyo.

Hata hivyo Waziri ametetea kampuni hiyo ambayo ilikuwa inunue korosho ilifanyiwa upembuzi yakinifu na kubainika inastahiki kufanya biashara ndani ya Kenya, Afrika Mashariki na duniani.

Amesema mkataba wa kununua korosho nchini ulisitishwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kampuni hiyo kuonekana kuwa kizingiti cha kuendelea kuuza korosho nchini jambo ambalo Serikali haikukubaliana nayo.

Kwa mujibu wa waziri huyo, balozi wa Tanzania nchini Kenya pamoja na balozi wa nchi hiyo kwa pamoja waliifanyia uchunguzi kampuni hiyo na kuona inafaa lakini kuna baadhi ya Watanzania walianza kutoa maneno ambayo yalipelekea Serikali kusitisha mkataba.