In Summary

Mwijage amesema tathmini inaonyesha kuwa katika kipindi cha kati ya Machi na Septemba 2018 hakukuwa na ongezeko kubwa la bei ya sukari nchini.

Dodoma. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema kusambaza sukari nchini kwa lengo la kushusha bei ya sukari hakutaleta matokeo chanya kwa sababu bei ya bidhaa hiyo inategemea gharama za uzalishaji, usafirishaji na kodi vigezo ambavyo si rahisi kuviepuka.

Hivi karibuni Mbunge wa Mpwapwa (CCM) George Lubeleje aliomba mwongozo wa Spika kuhusu bei ya sukari nchini kuwa ni kati ya 2,600 hadi Sh3, 000 kwa kilo wakati sukari imejaa katika maghala viwandani.

Akitoa kauli ya Serikali bungeni leo Septemba 13, 2018 kuhusu hali ya sukari nchini.

“Napenda kulihakikishia Bunge kuwa hakuwepo upandaji wa bei mkubwa sana ila mabadiliko ya kati ya Sh50 mpaka Sh150 kutegemea mkoa na mkoa,”amesema.

Amesema kwa wastani wa bei za rejareja nchini ya juu ilikuwa kati ya Sh2,669 kwa Mei mwaka 2018 na bei ya wastani ya chini ikiwa Sh2,594 kwa Agosti mwaka 2018.

Amesema tathmini hiyo pia inaonyesha kuwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Machi hadi Agosti mwaka huu kuhusu upatikanaji wa sukari Tanzania unaonyesha kuwa bidhaa hii inapatikana bila matatizo nchini.